Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu na Kishapu mkoa wa Shinyanga,mto huo ni tegemeo kubwa la wananchi wa wilaya ya Kishapu kutokana na uhaba wa maji.
Wakati nchi ya Tanzania ikiadhimisha wiki ya maji,imeelezwa kuwa wanawake wengi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji hivyo kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kikamilifu.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu na Maswa mkoa wa Simiyu kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika mpaka sasa hali inayowafanya kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea wilayani humo wananchi wa vijiji vya Nyenze na Ng’wang’holo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani humo walisema maji ni changamoto kubwa inayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwani wanatumia muda mwingi kutafuta maji.
Walisema licha ya kuishi karibu na mgodi wa almasi wa Williamson wanalazimika kutembea umbali takribani kilomita tano kufuata maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu na wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Akielezea changamoto hiyo,mkazi wa kijiji cha Nyenze Agnes Daudi alisema akina mama ndiyo waathirika wakubwa kwani wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji na mara nyingi huamka kila siku majira ya saa 11 alfajiri kwenda katika mto huo na kurudi nyumbani saa 4 asubuhi.
“Licha ya kutumia muda mwingi kufuata maji,hayo maji yenyewe ya mto Tungu siyo salama kwani yanatumiwa pia na wanyama kama fisi na watu wengi kijijini huwa hawachemshi maji wanakunywa hivyo hivyo”,alieleza Daudi.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo,wanawake wapo hatarini kushambuliwa na wanyama aina ya fisi ambao wamekuwa wakikutana nao mara kwa usiku wanapofuata maji mtoni.
Naye Anastazia Lutamla walisema maji yamesababisha migogoro katika ndoa kwani wanaume wamekuwa wakiwatuhumu wake zao kuwa wanachelewa kurudi nyumbani kwa kisingizio cha maji.
“Wanawake wanakumbana na changamoto nyingi njiani ikiwemo kubakwa,wasukuma ni waoga wengi wamekuwa hawasemi vitendo wanavyofanyiwa wakiamini kuwa ni fedheha mbele ya jamii”,aliongeza Lutamla.
Grace Maige mkazi wa kijiji cha Ng’wang’holo aliiomba serikali na mgodi wa almasi wa Williason,Karspian na El-Hilal vilivyo karibu na vijiji hivyo kuimarisha ujirani mwema kwa kuwapatia huduma ya maji wananchi kwani wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu sasa.
Naye Tungu Magega ambaye jina lake linatokana na mto Tungu ambapo alizaliwa wakati mama yake akichota maji katika mto huo mwaka 1949 alisema vijiji vinavyozunguka mgodi wa Williamson vilipaswa hudumiwa na mgodi huo hata kwa kuwachimbia visima tu.
“Nilizaliwa mwaka 1949,nipo katika kijiji hiki cha Nyenze tatizo la maji ni changamoto kabla na baada ya uhuru,tunaomba serikali itusaidie kuondoa tatizo hili,kama mgodi umeshindwa kutuhudumia,basi tunaomba hata maji kutoka ziwa Victoria yaje kijijini kwetu”,alieleza Magega.
Afisa Mtendaji wa kata ya Mwadui Lohumbo James Limbe alisema ni kweli kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya maji na kwamba jitihada wanazofanya sasa ni kuboresha visima vilivyopo katika baadhi ya vitongoji vilivyoharibika wakati wakisubiri maji kutoka ziwa Victoria kufika katika kijiji hicho.
Limbe alisema wanawake katika kata hiyo wanapoteza muda mwingi kwa badala ya kufanya shughuli zingine za maendeleo kwa kufuata maji katika mto Tungu ambayo hata hivyo siyo salama kwa maisha ya binadamu.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba alisema suala la ukosefu wa maji lipo kwa wilaya hiyo ni kame lakini serikali inafanya jitihada za kuwapatia maji wananchi ambapo tayari bomba la maji kutoka Ziwa Victoria yameshafika katika mji wa Mhunze wilayani humo.
“Siyo kweli kuwa wananchi wote wanatumia maji ya mto Tungu,wengine wana visima,mabwawa,hivi sasa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria unaendelea Kishapu,ukikamilika tutapata maji, tatizo ni upatikanaji wa pesa”,alieleza Nyabaganga.
“Kadri tutakavyopata pesa tutapeleka maji vijijini,tumeanza na mji wa Mhunze,kila kijiji palipopita bomba tumeweka toleo la maji,tenki letu lipo mbioni kukamilika,bomba tayari limeshatandazwa”,aliongeza Talaba.
Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa mto Tungu
Watoto wa kike wakipeleka mifugo yao kunywa maji katika mto Tungu huku mwananchi akiendelea kufua nguo
Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akitoka mto Tungu kuchota maji ya kunywa
Haya ni mashimo yaliyofukuliwa pembezoni mwa mto Tungu ambapo maji hujichuja kutoka kwenye mto na kuingia kwenye mashimo hayo na wananchi kuchota maji hayo kwa ajili ya kunywa
Shimo lililofukuliwa pembezoni mwa mto Tungu
Mchungaji wa mbuzi,ng'ombe akipeleka mifugo yake mto Tungu
Wananchi wakifua nguo katika mto Tungu
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
2 comments:
Hatari lakini Kama sikosei huko si ndiko yanapo toka makontena ya mchanga wa dhahabu kwenda nje? Kama ndio huko au huo mkoa tunaambiwa kwa muda wa miaka 20 sasa kumekuwa na usafirishaji huo na hao wasafirishaji wanasema wanafanya kazi ya bure kwa sababu wanachokipata ni kidogo. Kama kweli wanachokipata ni kidogo waendelee kufanya kazi hiyo kwa hasara kwa zaidi miaka 20? Tunaposema watanzania ni watu hovyo hasa wale wanaojiita wasomi na vyombo vya habari sio tuna tania. Bora mtanzania wa kawaida atakwambia la maana. Wameendekeza kuchapana mipasho na kushughulikia udaku wakati kuna taarifa za maana za kuwahabarisha watanzania. Kwa miaka 20 watu wanatorosha utajiri wa nje ya nchi wakiwaacha watanzania wakipiga stori za kipuuzi na umasikini wao wa hali na akili. Sio siasa wala si mapenzi lakini waache watu waseme watakavyosema hakuna kama Maghufuli na itachukua muda kwa Tanzania kumpata kiongozi Kama yeye.
So strange how "wanawake" are going through this, not wananchi. I want to see what will happen when one day "wanawake" wataamua kugoma.
Post a Comment