ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 30, 2017

LISSU AOMBA KWENDA IKULU

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amesema uongozi wa chama hicho umemwandikia Rais John Magufuli kutaka kukutana naye Ikulu ya Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha rasmi na kufanya mazungumzo.
“Ni mkutano baina ya Rais na rais,” alisema Lissu katika mahojiano na gazeti hili alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alichaguliwa kuwa rais wa chama hicho mapema mwezi huu, na Rais ni mmoja kati ya viongozi kadhaa waliowaandikia kuomba kukutana nao.
Aliwataja wengine kuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na marais wawili wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
Alisema tayari Jaji Mkuu ameshakubali ombi lao.
Kuhusu ombi lao kwa Rais Magufuli, Lissu alisema atatumia fursa hiyo vizuri, iwapo watakubaliwa.
“Nikifika nitaanza kwa kumshukuru Rais kwa kuwafundisha Watanzania maana ya utawala wa sheria, uhuru wa mawazo, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa Mahakama na Bunge,” alisema Tundu Lissu.
Lissu alifafanua baadaye kuwa Rais Magufuli amefumbua wengi macho kujua vitu hivyo kutokana na jinsi anavyoendesha nchi, ndio maana atamshukuru.
“Tumeomba appointment na Rais Magufuli tuzungumzie utawala wa sheria,” alisema Lissu.
“Leo ni Jumatano? Barua tulimpelekea Jumatatu. Tutaenda kujitambulisha na kuzungumzia utawala wa sheria na mwelekeo wa taifa hili. Ni between presidents. Tuna imani kwamba atatukaribisha. Tutamweleza maoni yetu, pale tunapoona amekosea tutamweleza na pale anapoona tuna matatizo atatueleza.”
Alisema wanajua kuwa Rais ana shughuli nyingi, lakini wanatarajia atatenga muda kwa ajili yao.
“Tunafahamu yuko busy, lakini kama anaweza kuangalia Shilawadu, atakuwa na muda hata nusu saa au saa nzima ya kuongea na kiongozi wa chama cha mawakili wa Tanganyika,” alisema.
Lakini akaonyesha jinsi alivyopania kueleza matatizo anayoyaona katika utawala wa sasa.
“Nakwenda kumpa vidonge vyake, kabisa! Wala sitammezea. Nitamwambia kwa heshima zote kwamba Mheshimiwa Rais, sisi kama mawakili wa Tanganyika tuna wasiwasi mkubwa na mwelekeo wa Serikali yako,” alisema.
“Wamenituma nikueleze mwelekeo na matendo ya Serikali yako. Unatawala vibaya, nje ya Katiba, wameniambia nije nikwambie ujirekebishe. Nakwenda kumsimanga tu. Halafu tukitoka pale namwambia Mheshimiwa Rais tupige picha, wajue nilikuja.”
Alisema iwapo Rais hatakubali kuwaalika, ataueleza umma.
“Atakuwa amenirahisishia, nawaita waandishi wa habari nawaambia. Tulimwambia Bwana mkubwa tumsalimie na tumweleze kwamba haturidhiki na utawala wake, yeye amekataa amekimbia,” alisema Lissu.
Hata hivyo, mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa amemtaka Lissu kusubiri taratibu za kiutawala.
Msigwa alimshangaa Lissu kwa kitendo chake cha kuzungumza katika vyombo vya habari ilhali anajua utaratibu wa kiutawala.
“Yeye kama ameandika barua barua si asubiri majibu? Muulizeni inakuwaje kabla hajapewa majibu anaenda kutangaza katika vyombo vya habari? Si asubiri utaratibu wa kiutawala,” alisema Msigwa.
Lissu alisema ofisi nyingine walizopeleka maombi kama hayo ni ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi alisema hana taarifa juu ya barua hiyo kwa kuwa tangu ateuliwe hajaingia ofisini.
“Nimekuwa katika vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, hivyo sina habari hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Profesa Kabudi alisema inawezekana ni kweli rais huyo wa TLS amewasilisha barua hiyo ofisini kwake lakini yeye bado haijamfikia.

1 comment:

Anonymous said...

Ndugu Tundu Lissu kwa msemo wa wenzetu wazungu naona ni "Power hungry". Wewe kama "Rais" wa TLS ni upuuzi kujilinganisha na kiongozi wa dola "Rais" JPM. Give me a break sir! JPM alichaguliwa na mamilioni ya Watanzania, wengi wakiwa vijijini. Wewe umechaguliwa kwa kura takribani 1,600 kuongoza wanachama wapatao 6,000 wengi mkiwa mnakula bata mijini. Kwa uwiano huu, wewe usingethubutu hata kujilinganisha na Rais wa Jamhuri, kwani kufanya hivyo ni hatari na upotoshaji maana itawezekana siku moja, Rais wa chama cha Wavuvi, Rais wa Darasa la Nne katika shule ya msingi kule kijijini kwangu n.k. nao wataanza kujigamba na kujiona wako sawa na JPM. Mimi kama mdau, nimechoshwa na kelele zisizotuletea tija. Pigeni kelele za kutuletea maendeleo ya kiuchumi. Babu na Nyanya zetu kule vijijini waliompigia kura JPM kwa wingi wapo poa, maana huduma muhimu zimeongezeka na maisha yao kimaendeleo yanamwelekeo mzuri. Ningemshauri Rais JPM kutowasikiliza na kupoteza muda na hawa wapiga kelele (cry babies) ambao hawatuletei maendeleo yeyote.