ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 28, 2017

Ripoti: Faru John alikufa kwa uzembe

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa kiongozi wa tume ya uchunguzi wa faru huyo ambaye pia ni Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, Dar es Salaam. (Picha na Fadhili Akida).
RIPOTI ya Uchunguzi kuhusu kifo cha Faru John imethibitisha kuwa amekufa, lakini kifo chake kilitokana na kutelekezwa na maofisa wa Hifadhi ya Ngorongoro hivyo akakosa matunzo, uangalizi wa karibu na kukosa matibabu pale alipoumwa akiwa katika kwenye pori la wawekezaji binafsi huko Sasakwa, Grumeti.

Uchunguzi huo uliofanywa na tume iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, umebainisha kuwa Faru John baada ya kuhamishwa kutoka Ngorongoro na kupelekwa Sasakwa, Grumeti alitelekezwa na maofisa wa Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kutofuatilia maendeleo ya afya ya mnyama huyo.

Aliitupia lawama Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake zinazohusika na uhifadhi wa wanyamapori kuwa walichangia kifo cha Faru John kutokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na kuwepo kwa mapungufu ya uongozi ndani ya taasisi hizo.

Alisema baada ya kupelekwa Grumeti, wahusika hawakurudi tena kumwangalia na hivyo alipougua hakutibiwa.. Kwa hali hiyo tume hiyo imeshauri serikali kuwachukulia hatua za wajumbe wote wa kamati ya uongozi na wale wa Kamati ya Ufundi wa Hifadhi ya Ngorongoro.

Pia ripoti hiyo aliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, imeishauri serikali kumchukulia hatua mtu aliyetajwa kwa jina moja la Dk Kileo wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kuwa ndiye alikuwa na jukumu la kuhakikisha Faru John anakuwa na afya nzuri, lakini badala yake alimtelekeza huko Grumeti.

Uthibitisho wa kifo

Profesa Manyele alisema sampuli 45 zilichukuliwa kwenye mzoga wa Faru huko Sasakwa, Maabara ya Hifadhi ya Ngorongoro na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), sampuli za uchunguzi kutoka Taasisi ya Wanyamapori (TAWIRI) na Tanapa.

Alisema pia walichukua kipande cha pembe cha Faru John kilichokatwa wakati wa kumwekea ‘transmitter’ na ambacho hakikuwasilishwa kwa Waziri Mkuu, sampuli za pembe mbili kutoka hifadhi ya nyara iliyoko Dar es Salaam.

Alitaja aina ya sampuli hizo kuwa ni mifupa ambayo ni fuvu na mzoga uliokuwa Sasakwa Grumeti, pembe mbili zilizochukuliwa Dar es Salaam na pembe moja iliyochukuliwa Ngorongoro, damu kutoka maabara ya Ngorongoro na SUA, ngozi kutoka kwenye mzoga Sasakwa na kinyesi kilichokaushwa kutoka SUA.

Alisema baada ya sampuli hizo kupelekwa Afrika Kusini katika Chuo Kikuu cha Pretoria, maeneo ya ulinganishaji wa vinasaba na mfanano ulikuwa asilimia 100.

“Mzoga, fuvu, pembe zote tatu, damu zote ni za faru John. Pembe alizowasilisha Waziri wa Maliasili na Utalii zilikuwa za Faru John, damu zilizokusanywa zilikuwa za Faru John...Faru John alikufa Sasakwa, Grumeti,” alisema Profesa Manyele.

Licha ya sampuli, tume hiyo iliwahoji watumishi na watu wengine wapatao 18 ambao pia walithibitisha kifo cha Faru John.

Matokeo ya uchunguzi

Alisema licha ya kuwepo mawasiliano kati ya wizara na taasisi zake, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda Grumeti.

Tume hiyo imeshauri hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mhifadhi wa NCCA kutokana na mapungufu ya kiutendaji ya kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali.

“Tume inashauri taratibu za kuhamisha wanyama walio katika hatari ya kutoweka ziwekwe bayana, zianishe kwenye ikanuni na sheria,” alieleza Manyele na kuongeza kuwa, tume hiyo ilibaini kutokuwepo na mkataba rasmi kati ya serikali na mwekezaji unaonesha mnyama ametoka serikalini na kwenda kwa mwekezaji.

Migogoro ya wafanyakazi

Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa wakati wa sakata hilo la Faru John, NCCA iliingia kwenye migongano na baadhi ya wafanyakazi wake ambao walikuwa wanasimamia maslahi ya taifa katika kuhifadhi wanyamapori.

Alishauri serikali iunde tume huru kuchunguza migogoro ya kimaslahi kati ya watumishi wa NCCA dhidi ya uwekezaji ndani ya hifadhi na hatua stahiki zichukuliwe.

“Tunashauri serikali ifanye tathmini ya kina kuona kama uongozi uliopo kwa sasa NCAA unajitosheleza kuendelea kuongoza taasisi hiyo kwa maslahi mapana ya taifa,” alisema Profesa Manyele.

Ongezeko la mifugo, watu

Tume hiyo pia ilionya kuwa ongezeko la watu ambalo kwa sasa linafikia watu 90,000 walioko kwenye hifadhi ya NCAA kutoka watu 8,000 mwaka 1959 ni mwanya wa majangili kujipenyeza na kujificha.

Alisema ni hatari kwa baadhi ya wanyama kutoweka na kupotea. Tume imeshauri tathmini ya kina ifanyike ili kubaini athari zinazojitokeza kutokana na ongezeko la watu na mifugo NCCA.

Alisema sheria hiyo ipitiwe upya na kuona umuhimu wake kwa sasa.

Uwekezaji hatari

Katika ripoti yake alisema uwekezaji uliofanywa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ni hatari kutokana na maamuzi yake kufanywa na wizara peke yake.

Alisema matokeo yake uwekezaji wa ujenzi wa Ndutu Lodge umefanywa katika maeneo ya mapitio ya wanyama na ujenzi huo ulifanyika bila kufanyika kwa Tathmini ya Athari za Kimazingira (EIA).

Imeshauri ujenzi wa Ndutu Lodge uchunguzwe upya. Pia uchunguzi wa aina hiyo ufanyike kwenye maeneo mengine ya hifadhi za taifa.

Udhibiti wa ujangili

Alisema tume yake inashauri kufanyike utambuzi wa wakazi halali ndani ya kreta ya Ngorongoro na maeneo mengine ya Serengeti na kuzuia uhamiaji katika maeneo hayo.

Pia ameshauri kuanzishwa na kuimarisha maabara ya DNA ya wanyama chini ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kutoa msaada kwa vyombo ya haki jinai katika kupeleleza na kuchunguza kazi zinazohusiana na ujangili.

Wameshauri pia kuimarisha vikosi vya kuzuia ujangili kwa kushirikisha jeshi la wananchi, kwa namna itakavyoonekana inafaa.

Lakini wameonya pia kuwa mwingiliano kati ya mifugo na wanyamapori kunatoa mwanga wa majangili kutumia nafasi hiyo kufanya uhalifu. “Tume inashauri kuwepo udhibiti wa sheria kali ya kuzuia mifugo katika maeneo ya hifadhi,” alisema.

Aliongeza kuwa vibali vya uwindaji vya wanyama wanaoelekea kutoweka vifutwe. Sheria ipitiwe ili kuzuia vibali hivyo.

Viwanja vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi vifanyiwe tathmini ya kina juu ya manufaa ya uwepo wake, usimamizi na uendeshaji wake ili kulinda maslahi ya taifa.

Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ilipuuza maoni ya wataalamu wakati wa kufanya maamuzi. Pia tume hiyo imekosoa maamuzi makubwa ya kitaifa kufanywa na mkurugenzi wa wanyamapori peke yake.

Kauli ya Waziri Mkuu Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na tume hiyo na kuyatangaza kwa umma.

“Ripoti hii ni ndefu sana, ngoja tukaisome, matokeo tutakayochukua tutayatangaza kwa umma,” alisema Majaliwa.

HABARI LEO

No comments: