Mkanda wa video uliosambazwa mitandaoni baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka juzi, unamuonyesha Rais John Magufuli akizungumza kwa uchungu dhidi ya usafirishaji mchanga wa madini nje ya nchi akiwa na marafiki zake.
Wakati huo, Magufuli hakuwa amechukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM na pengine hakuwa hata na nia ya kufanya hivyo, ndio maana mmoja wa rafiki hao alimuuliza sababu za kutochukua fomu ili atekeleze nia hiyo ya kupambana na usafirishaji mchanga nje ya nchi.
Pamoja na kwamba alikuwa Waziri wa Ujenzi, Magufuli alizungumza maneno hayo nje ya Bunge, lakini ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria walikuwamo wabunge wengi waliowahi kuzungumza suala hilo na hasa la sheria na mikataba ya madini kwa hisia kali, lakini walipuuzwa na wakati mwingine kuadhibiwa.
Zitto Kabwe, Tundu Lissu, John Mnyika, Dk Willibroad Slaa ni baadhi tu ya wabunge waliozungumza kwa nguvu dhidi ya upitishaji sheria kiholela na usiri wa mikataba ya madini, lakini wakaishia kuzomewa, kupingwa na wakati mwingine kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za Bunge na kukosa baadhi ya vikao kwa kujaribu kutetea rasilimali za Taifa.
Wapo waliofanya hivyo nje ya Bunge kwa kutumia harakati na Mahakama, lakini haikuwezekana.
Lakini uamuzi wa Rais Magufuli kuzuia usafirishaji mchanga nje ya nchi, kupitia upya sheria za madini na kuzipeleka upya bungeni, kushughulikiwa kwa mawaziri na watendaji wote waliohusika kusaini mikataba ya madini na kuwawajibisha wahusika wote ni kielelezo kuwa Rais ameanza kupaza sauti zilizopuuzwa ndani na nje ya Bunge.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa sakata la mchanga wa madini juzi, Rais alikubali mapendekezo yote ya kamati hiyo ambayo baadhi yalishawahi kutolewa na wabunge, viongozi mbalimbali na wanaharakati tofauti, lakini hatua hazikuchukuliwa.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kujenga kinu cha kuyeyushia mchanga, kuwawajibisha mawaziri, wanasheria na watendaji wote waliohusika katika kupeleka sheria bungeni na kusaini mikataba ya madini, kuendelea kuzuia mchanga usisafirishwe nje, kufuta utaratibu wa kupokea mrabaha wa asilimia 90 na Benki Kuu kufuatilia malipo ya fedha za kigeni ya mrabaha.
Kamati hiyo ilisema katika taarifa yake kuwa Acacia Mining, inayoendesha migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu inayozalisha mchanga huo, haijasajiliwa nchini na kwamba kwa miaka takriban 20 iliyochimba dhahabu, Tanzania imepoteza takriban Sh108 trilioni.
Udhaifu wa sheria na mikataba ya madini ulishaanza kuonekana muda mrefu.
Miaka 10 iliyopita, Zitto, Kiongozi wa ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, alizuiwa kuhudhuria vikao kwa miezi mitatu kutokana na kumtuhumu aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Naziri Karamagi aliusaini mkataba huo kinyume na taratibu.
Zitto, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alitoa hoja binafsi ya kutaka kuundwa kamati ya kumchunguza Waziri Karamagi kwa kusaini mkataba wa Buzwagi jijini London, kitu kilichopingwa na wabunge wengi, hasa kutoka CCM.
Mbunge huyo alihoji ni mikataba mingapi iliyosainiwa nje ya nchi, madhara ya kusainiwa nje ya nchi na kama unaonyesha kuwa ulisainiwa Dar es Salaam au London.
Pia alihoji ni kwa nini waziri alisaini mkataba huo kabla Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), halijatoa ruksa kama sheria za nchi zinavyoeleza.
Akijibu hoja hiyo, Karamagi alisema uamuzi wa kuuingiza mradi wa Buzwagi kwenye miradi ya kampuni ya Barrick Gold, ulihitajika kufanywa vinginevyo fursa ya uwekezaji katika mradi huo ingeweza kupotea na kuisababishia hasara Taifa.
Alisema maandalizi yote ya kusaini mkataba huo yalikamilika akiwa nje ya nchi na kumtuhumu Zitto kutumia Bunge kama jukwaa lake la kujipatia umaarufu kisiasa.
Karamagi alidai kuwa hoja hizo si za kweli na kwamba, japo alisaini mkataba nje kutokana na umuhimu, kila kitu kilizingatiwa.
Ndipo aliyekuwa Mbunge wa Mchinga (CCM), Mudhihir Mudhihir alipotoa hoja ya kutaka Zitto aadhibiwe kwa madai kuwa alilidanganya Bunge.
Mudhihiri alikariri kifungu namba 59 cha Kanuni za Bunge, Fasili ya 3 kinachosema kwamba “mbunge anaweza kutoa hoja ya kutaka mbunge mwingine aadhibiwe kwa kusema uongo unaolivunjia heshima Bunge”.
Baada ya uamuzi kutolewa kwamba zipigwe kura kuhusu kumsimamisha Zitto, baadhi ya wabunge, hususan wa kutoka kambi ya upinzani, walipinga.
Pamoja na Dk Slaa, ambaye alikuwa Mbunge wa Karatu (Chadema), kushauri Karamagi awasilishe nyaraka ili kukanusha hoja za Zitto, ushauri huo haukuzingatiwa.
Kabla ya uamuzi dhidi yake, aliyekuwa Spika wa Bunge marehemu, Samwel Sitta alimpa nafasi Zitto kusema dukuduku lake na badala yake alisema: “I am democrat na nipo tayari kwa maamuzi yoyote yale.”
Wakati anakaribia kumaliza muda wa adhabu hiyo, Rais Kikwete alimteua Zitto kuwa mjumbe wa Tume iliyoangalia upya sheria na mikataba ya madini.
Na juzi, Rais Magufuli amekubali pendekezo la kuchukuliwa hatua kwa wote waliohusika na mikataba hiyo, akiwamo Karamagi.
Lissu alivyopambana
Usumbufu kama huo amekumbana nao Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema.
Lissu, ambaye kitaaluma ni wakili, alianza kupambana na utaifishaji wa rasilimali za madini akiwa mwanaharakati, akipinga sheria za madini zilizopitishwa bungeni kwa maelezo kuwa zilikuwa na udhaifu, badala yake akaingia matatizoni.
Lissu alipinga sheria za madini ambazo ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Fedha ya 1997 iliyofuta kodi nyingi kunufaisha kampuni za kigeni za madini.
Pia, alipinga Sheria ya Uwekezaji Tanzania 1997 na Sheria ya Madini ya 1998 ambayo ilitamka kwamba mwenye miliki ya madini na fedha yote itokanayo na mauzo ya madini ni mwenye leseni ya kuchimba madini hayo.
Lakini alikumbana na fedheha. Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alisema wakati anazindua mgodi wa Bulyanhulu kuwa upinzani ni ujinga uliofichama katika kivuli cha taaluma.
Lissu na Dk Rugemeleza Nshala walikamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa uchochezi na kesi iliyodumu kuanzia Mei 2001 hadi 2008 ilipofutwa kwa kukosekana ushahidi.
Lissu pia alikuwa mmoja wa wabunge wa upinzani waliosusia kikao baada ya Serikali kuwasilisha kwa hati ya dharura miswada mitatu ya sheria kuhusu petroli na gesi.
Katika kupaza sauti hiyo ya Lissu na wenzake, Rais Magufuli, ingawa alionekana kumponda mbunge huyo wa Chadema, alimuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuunda jopo la kupitia sheria zote za madini na kuzipeleka bungeni zipitishwe.
Mnyika asombwa mzobemzobe
Matatizo hayo hayakumuacha Mnyika, Mbunge wa Kibamba kwa tiketi ya Chadema.
Katika Bunge la Bajeti lililopita, Mnyika, ambaye ni waziri kivuli wa nishati na madini, alisema sera ina upungufu na kwamba mbinu za Serikali kutumia misamaha kuvutia wawekezaji badala ya kuboresha huduma kama nishati, zinasababisha kupoteza fedha nyingi.
Katika Bunge linaloendelea, Mnyika alisombwa na askari wa chombo hicho alipobishana na Spika kuhusu mtu aliyetamka neno “Mnyika mwizi” kwa kutumia kipaza sauti wakati akitoa taarifa.
Alikuwa akitoa taarifa kwa Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliyesema wapinzani wanatetea wezi, lakini Mnyika akampinga kwa kusema Serikali imezuia mchanga wa madini kusafirishwa nje, lakini hadi wakati huo dhahabu ilikuwa inaendelea kusafirishwa nje na hivyo CCM ndiyo inashirikiana na wezi.
Wakati akitakiwa kukaa chini, sauti hiyo ikamwita mwizi na ndipo Mnyika alipochachamaa kutaka hatua zichukuliwe, badala yake akakumbana na amri ya Spika ya kutaka askari wamtoe, tena kinguvu.
Siku chache baadaye, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akawasilisha mapendekezo ya Bajeti yanayotaka dhahabu itozwe asilimia moja katika vituo vya ukaguzi vilivyo mipakani na viwanja vya ndege.
Dk Magufuli kabla ya kuwa Rais
Pengine mtu ambaye hakupata suluba kwa kuwa na mawazo dhidi ya uendeshaji wa biashara ya madini, ni Dk Magufuli na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Mkanda wa video uliosambaa mitandaoni unamuonyesha Magufuli akiwa na rafiki zake wakijadili masuala ya kitaifa na unaonyesha jinsi alivyokuwa akifuatilia suala la mchanga na jinsi anavyolipinga.
Ilikuwa ni baada ya kupata maelezo kutoka kwa mtaalamu aliyemwambia kuhusu mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi na ilipofikia suala la mchanga, Magufuli alimkatisha.
“Sasa hapo ndiyo tunaibiwa tena,” Magufuli anasikika, lakini Charles Kitwanga anamsihi bila mafanikio asikilize kwanza.
“Kwani Watanzania hapa tunashindwa kutengeneza smelter yenye temperature ya 1,500 ambayo ndiyo boiling point (kiwango cha juu cha joto la kuyeyushia) ya silver (fedha), ya copper (shaba) yakawa yanatoka tu huko kama maji,” anasema Magufuli.
Na Kitwanga alipomshauri achukue fomu kugombea urais ili atekeleze nia hiyo, Magufuli anamjibu kwa utani akisema: “Unajua ninachosema? Mimi watu watalimia meno.”
Lowassa kuhusu mikataba
Mwingine ambaye hajapata msukosuko kwa kuzungumzia mikataba ya madini ni Lowassa, ambaye alionyesha msimamo huo wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2015 akiwa anaiwakilisha Chadema.
Lowassa aliwahi kuahidi katika mikutano yake ya kampeni kuwa atapitia na kufuta mikataba yote ya madini iliyoingiwa kilaghai.
Pia aliahidi kuunda kamati maalumu ya kupitia mikataba hiyo ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali zilizopo nchini.
“Kuna malalamiko mengi. Nikiingia madarakani nitaunda tume ya kuchunguza jambo hili, ili nihakikishe tunapata zaidi kuliko mgeni. Pale ambapo mkataba umempendelea mgeni, nitafuatilia mbali na kuanza upya,” alisema Lowassa katika mkutano wa kampeni Geita.
Takriban miaka miwili baadaye, Rais Magufuli ameunda kamati mbili ambazo zimeona udhaifu katika mikataba na sheria.
Wasusia miswada mitatu
Sakata hilo pia lilihusisha kambi ya upinzani, ambayo katika Bunge la mwisho la Serikali ya Awamu ya Nne ilikataa kushiriki kupitisha miswada mitatu ya petroli na gesi iliyowasilishwa kwa hati ya dharura.
Kiongozi wao, Freeman Mbowe alisema: “Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya kuigeuza kuwa sheria.”
No comments:
Post a Comment