Advertisements

Friday, June 16, 2017

SIKIO LA KUPANDIKIZA LIMEMUEPUSHA MTOTO AGNES KUWA KIZIWI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
NI jambo la kawaida watoto kukusanyika na kucheza kwa furaha michezo mbalimbali kwa pamoja, kitendo hicho huwasaidia pia kujifunza kwa urahisi vitu vingi ikiwamo lugha.
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mtoto Agnes Stephano mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.

Mtoto huyu kila alipokuwa akicheza na watoto wenzake alionekana mtulivu muda mwingi huku akiwa haelewi jambo lolote.
Hali hiyo ilimpa wasiwasi mama yake, Maria Buganda ambaye anasema aliamua kumfikisha hospitalini kwa uchunguzi.
“Alionekana tofauti kabisa na watoto wenzake ambao muda wote waliwasiliana vema na kufurahi lakini yeye hakuweza kabisa.

“Hata akiitwa jina lake haitiki, kitu kikidondoka chini hashtuki, hapo nilihisi kuna jambo linamtatiza nikaamua kumfikisha hospitalini,” anasema.
Maria anasema awali alimpeleka katika Hospitali ya Regency ambapo madaktari walimchunguza na kumshauri ampeleke Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
“Nilikubali ushauri wao, waliniambia Muhimbili nitapata matibabu sahihi, nilipofika hapa walimfanyia vipimo vya awali, wataalamu walimpigia ngoma, makofi na vitu vya namna hiyo lakini hakusikia chochote,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo alifanyiwa kipimo kingine cha EBR ambacho ni maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwenye ubongo kubaini kama kuna tatizo.
“Kwa kutumia kipimo hicho, wataalamu walipima hadi nyuzi 90 ambacho ni kiwango cha mwisho cha kipimo lakini hawakubaini kama ana uwezo wowote wa kusikia,” anasema.
Anasema alipofika hospitalini hapo alipata taarifa kwamba kuna watoto watapata fursa ya kufanyiwa upasuaji wa kupandikizwa vifaa vya usikivu jambo ambalo lilimpa faraja.
“Lakini matumaini ya mtoto wangu kuweza kusikia tena yaliyeyuka baada ya kuambiwa kwamba haitawezekana kufanyiwa upasuaji kwani tulikuwa tumechelewa na orodha ilikuwa imeshapangwa,” anasema.
Maria anasema wakati akijandaa kuondoka kwenda nyumbani kwake, daktari mmoja alimpa habari njema.
“Alinitaka nisiondoke, kwamba madaktari baada ya kukaa na kujadili waliridhia kumfanyia upasuaji mtoto wangu kwani umri wake ni mdogo na ndiyo unaofaa kupata tiba,” anasema.
Anaongeza; “Furaha yangu ilirejea upya, tayari mwanangu amefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa kifaa hicho, maendeleo yake ni mazuri ingawa bado hajaweza kusikia kwani wamenieleza mashine itawashwa baada ya mwezi mmoja.
“Wataalamu wamenieleza kwa kuwa amefanyiwa akiwa katika umri sahihi itakapowashwa itakuwa rahisi kwake kuongea hata kabla ya miaka minne,” anasema.
 Agnes alipatwa na nini?
Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa Muhimbili, Edwin Liyombo anasema Agnes alizaliwa na tatizo la usikivu.
 Jinsi sikio lilivyo
Dk. Edwin anasema sikio ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu, ndicho ambacho humuwezesha kusikia sauti mbalimbali.
Anasema ili mtu aweze kusikia mawimbi ya sauti husafirishwa kutoka katika sehemu ya nje ya sikio kwenda sehemu ya kati kisha sehemu ya ndani ya sikio.
Anasema mawimbi hayo yanapotoka sehemu ya nje huingia sehemu ya kati kwenye ngoma ya sikio kisha huenda katika sehemu ya ndani ya sikio ambako kuna kiungo kiitwacho kitaalamu cochlea.
Anafafanua kwamba cochlea ni kiungo maalumu kilichopo ndani ya sikio ambacho hukaa kwenye mfupa.
Dk. Liyombo anasema kiungo hicho ndicho ambacho humuwezesha binadamu kusikia mawimbi hayo ya sauti na kupeleka taarifa kwenye ubongo wake.
“Ndani ya cochlea kuna seli ndogo ndogo ambazo hizo zikifa binadamu hawezi kusikia kabisa katika maisha yake yote na hadi sasa hakuna dawa ya kutibu tatizo hilo,” anasema.
 Nini huua seli hizo.
Dk. Liyombo anasema zipo sababu nyingi zinazochangia mtoto kuzaliwa na tatizo hilo, ikiwamo matumizi holela ya dawa zenye kemikali kali.
“Kwa mfano, dawa ya kutibu malaria ya quinine na gentamicin ambayo hutumika kutibu ugonjwa wa UTIkwa mjamzito kuzitumia pasipo ushauri wa daktari, kitendo hicho huchangia kwa asilimia kubwa mtoto kuzaliwa na tatizo la usikivu (kiziwi),” anasema.
Anasema ndiyo maana wataalamu wa afya hushauri wajawazito kuhudhuria kliniki kipindi chote cha ujauzito ili wapate ushauri sahihi.
 Takwimu za WHO
Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba katika kila watoto 1000 wanaozaliwa, watoto wawili au watatu huzaliwa wakiwa na tatizo kubwa la usikivu. 
Hali ilivyo Muhimbili
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru anasema kila mwaka inakadiriwa watoto 200 huzaliwa wakiwa na tatizo hilo.
“Tangu mwaka 2003 hadi sasa wagonjwa 50 pekee ndiyo ambao wamenufaika na mpango wa ufadhili wa serikali na walikwenda kupata matibabu nchini India,” anasema.
 Mkakati
Profesa Museru anasema ili kuwezesha watoto wengi kunufaika na huduma hiyo, serikali iliiagiza hospitali hiyo kuhakikisha inaanzisha huduma hiyo nchini.
“Kila mwaka tulikuwa tunafadhili wastani wa watoto 15 ambao walikwenda nchini India maana yake watoto 185 walibaki wakiwa na tatizo hili, ni idadi kubwa mno,” anasema. 
Matibabu ni ghali
Anasema kila mwaka serikali ilitumia kati ya Sh bilioni 1.2 hadi 1.4 kufadhili matibabu ya watoto hao.
“Kila mtoto aligharimu kati ya Sh milioni 80 hadi 100 kufanikisha matibabu ya kupandikizwa kifaa maalumu cha kumsaidia kusikia,” anabainisha.
 Mkakati wa Muhimbili
Naye Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema tangu mwaka 2003 hadi sasa watoto 50 ndiyo wamepata huduma hiyo nje ya nchi.
“Huhitaji ni mkubwa, ili kufanikisha huduma kutolewa nchini, tumetumia Sh bilioni 13.664 kuboresha miundombinu ya utoaji huduma,  ununuzi wa vifaa na kusomesha wataalamu nje ya nchi,” anasema.
Anasema ili kufanikisha hilo, walikopa Sh bilioni 7.2 kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), walipata ufadhili wa Sh milioni 600 kutoka Abbott Fund, ruzuku ya maendeleo kutoka Serikalini Sh bilioni tatu na walitumia fedha kutoka vyanzo vya ndani vya hospitali Sh bilioni 2.860.
 Kauli ya wizara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema sasa watoto wengi watapata huduma ya upasuaji kwani inapatikana nchini.
“Watoto wanaozaliwa na tatizo wote tuna uhakika watapata huduma na kwa hatua hii maana yake tutapunguza idadi ya watoto wanaokwenda kusoma katika shule za viziwi,” anasema.
Anaongeza; “Muhimbili wamenieleza kuanzia Juni 5 hadi 6, mwaka huu wataalamu wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka India na Misri wamewafanyia upasuaji watoto watano na kuokoa kati ya Sh milioni 250 hadi 300 ambazo zingetumika iwapo tungewapa rufaa kwenda nje ya nchi.
 Rufaa nje ya nchi yafutwa
Waziri Ummy anasema kuanzia sasa serikali haitapeleka mgonjwa yeyote nje ya nchi atakayehitaji kufanyiwa upasuaji huo.
“Huduma ipo nchini, badala ya Sh milioni 80 hadi 100 gharama itakuwa Sh milioni 36.9 kwa mtoto mmoja hii ni sawa na punguzo la asilimia 60,” anasema.
Anasema kiasi hicho cha fedha kitawezesha serikali kununua vifaa hivyo (cochlea implant) ambavyo hugharimu kiasi cha Sh milioni 31.2 kwa kila mgonjwa mmoja.
Anasisitiza; “Ikiwa kuna watoto watakaohitaji matibabu ya kibingwa zaidi tutawakusanya na kuweka kambi maalumu kisha tutaleta wataalamu kutoka nje ya nchi waje wawafanyie upasuaji hapa hapa.
 Ushauri
Waziri Ummy anawashauri wazazi kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao na kuwawahisha hospitalini pindi wanapogundua kasoro.
“Ipo kasumba ambayo inabidi tuachane nayo, tubadilike, yaani unakuta mtoto anachelewa kuongea wazazi wanasema hata babu au bibi yake alichelewa kuongea.
“Kumbe ni tatizo la usikivu, wataalamu wanaeleza kwamba mtoto akiwa na tatizo hili hawezi kuzungumza mapema kwa sababu anashindwa kujifunza lugha, hasikii, ni vema wawahishwe hospitalini wapate matibabu,” anasema.
 Tanzania yavunja rekodi
Anasema kuanza kwa huduma hiyo nchini kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya.
MTANZANIA

No comments: