Advertisements

Monday, July 3, 2017

BANDARI DAR SASA HABARI NYINGINE

Rais John Magufuli akipewa maelezo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko kuhusu hatua za uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam wakati akiweka jiwe la msingi la Mradi wa Uboreshaji wa bandari hiyo. Kutoka kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke. (Picha na Fadhili Akida).
BANDARI ya Dar es Salaam ambayo ndio lango kuu la biashara nchini, inatarajia kuongeza uwezo wake wa kupokea meli kubwa na mizigo kutoka tani za sasa milioni 18 hadi kufikia milioni 28 ndani ya miaka saba ijayo.

Mafanikio hayo yanatokana na Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DSMGP), uliozinduliwa rasmi jana na Rais John Magufuli unaolenga kuiboresha zaidi bandari hiyo kuanzia idadi ya gati zake, kina cha bandari hiyo na barabara zake. Mradi huo ambao awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika baada ya miezi 28, utaiwezesha bandari hiyo kuhudumia kikamilifu nchi takribani saba ambazo ni Malawi, Burundi, Zambia, Rwanda, Uganda, Somalia, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Baada ya mradi huo kukamilika, bandari hiyo sasa itapitisha meli kubwa zenye urefu wa zaidi ya mita 300 tofauti na sasa ambako meli zinazohudumiwa ni zile zenye urefu wa mita 240 na kushusha mizigo kwa kuzingatia muda kwa kuwa itakuwa na gati zinazofanya kazi kwa uhakika zikiwemo gati maalumu kwa ajili ya kushushia mizigo. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko kwa sasa bandari hiyo ina uwezo wa kuhudumia tani milioni 18 za shehena na jumla ya gati 12 za kuhudumia shehena ya aina mbalimbali.

“Kati ya gati hizi, gati namba moja hadi nne zinahudumia mizigo ya kawaida, gati namba tano hadi saba zina uwezo wa kuhudumia shehena ya kontena zaidi ya 200,000 kwa mwaka chini ya usimamizi wa TPA na gati namba nane hadi kumi na moja zinahudumia kontena kupitia kitengo kinachoendeshwa na kampuni binafsi ya Tanzania International Container Terminals Services (TICTS) yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya kontena 400,000 kwa mwaka,” alifafanua Kakoko.

Kihistoria, mradi huo wa DSMGP ulianzishwa na serikali tangu mwaka 2009 baada ya kubaini kuwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam hautakidhi mahitaji makubwa ya kuhudumia shehena siku za usoni bila kufanya maboresho makubwa. Hali hiyo ilitokana na ukweli kuwa ukarabati wa bandari hiyo haujafanyika kwa muda mrefu kwani ujenzi wa kwanza ulifanyika katika miaka ya 1940 na 1950 na ulihusisha ukarabati mkubwa katika gati namba moja hadi saba na uchimbaji wa kuongeza kina cha lango la bandari mwaka 1998.

Baada ya hapo bandari hiyo imeendelea kutoa huduma ikiwa na lango lenye kina cha wastani wa mita 12 na upana wa mita 134. Hali hiyo imesababisha bandari kuhudumia meli ndogo zenye urefu wa wastani wa mita 243. Hata hivyo, Kakoko alisema mradi huo ukikamilika miezi 28 ijayo, itakuwa imeongeza uwezo wa kuhudumia shehena kutoka tani milioni 14 za sasa hadi tani milioni 28 ifikapo mwaka 2022 badala ya tani milioni 18 ambazo zingekuwa kikomo cha bandari ya sasa kama isipoendelezwa zaidi.

Aidha, itatoa huduma kwa viwango vya kimataifa kwa kuijenga, kuiwekea vifaa na mitambo ya kisasa na kujenga mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Mradi huo wa DSMGP una miradi midogo midogo ndani yake ipatayo 25 ambayo imegawanywa katika maeneo makubwa sita ambayo ni tafiti na usanifu na upanuzi na uimarishaji wa gati namba moja hadi saba kwa kuongeza kina kutoka mita 10 za sasa hadi mita 14.5.

Pia mradi huo utahusisha ujenzi wa gati ya kuhudumia magari, uchimbaji na upanuzi wa mlango wa kuingilia/kutokea meli na eneo la kugeuzia meli, kuongeza mashine za kukagua mzigo, milango ya kutolea shehena na mizani, pamoja na kuongeza tija na matumizi makubwa ya Tehama. Aidha, pia utahusisha kuchimba zaidi kina cha bahari kutoka wastani wa sasa wa mita 10.2 hadi mita 15.5 kwa urefu wa kilomita nane na kupanua upana wa lango kutoka mita 140 kwenda mita 170.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA alifafanua kuwa bandari hiyo ilipitisha tani milioni 13.8 kwa mwaka jana likiwa ni ongezeko kutoka tani milioni 13.1 za mwaka 2013, na tani milioni 10.4 mwaka 2011 ikionesha ukuaji wa wastani wa asilimia tisa kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kwamba wingi wa mizigo unaweza kuongezeka mara dufu kutoka tani milioni 14 za sasa hadi tani milioni 38 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alipozungumzia mradi huo utakaoagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 481 sawa na zaidi ya Sh bilioni 900 kabla ya kuuzindua, alisema bandari hiyo ni muhimu kuboreshwa kwa kuwa ina mchango mkubwa wa maendeleo ya ustawi wa Tanzania. Alisema pamoja na kwamba Tanzania ina bandari nyingine, lakini Bandari ya Dar es Salaam ndio kubwa kwa kuwa asilimia 90 ya mizigo inayoingia nchini inapitishiwa katika bandari hiyo.

Alisema mradi huo ni muhimu kutokana na ukweli kuwa hali ya sasa ya bandari hiyo si nzuri kwani pamoja na kuwa na gati 12, lakini kati ya gati hizo gati saba kina chake kilishuka na hivyo kuwa na uwezo wa kuegesha mitumbwi tu badala ya meli. Alisema hali hiyo ilichangia meli nyingi kuchukua muda mrefu zinapowasili nchini kushusha mizigo yake kwani ilibidi zisubiri kwa muda mrefu kwa kuwa hakukuwa na gati za kutosha.

“Lakini tumeshajua wafanyabiashara sasa wanakwenda na muda, hivyo kupitia mradi huu hawatakuwa na sababu ya kwenda kwingine zaidi ya kuja kwetu,” alieleza. Alisema bandari hiyo ambayo kwa sasa inahudumia nchi zaidi ya saba zilizopo kwenye maeneo yasiyo na bahari, pia itahudumia watu zaidi ya milioni 500 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Rais alisema mradi huo, utagharimiwa na serikali kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 64, Benki ya Dunia iliyotoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 345 na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) lililotoa msaada wa dola za Marekani milioni 12. Dk Magufuli alisema pamoja na mradi huo, Serikali ya Awamu ya Tano pia imedhamiria kuboresha miundombinu ya usafiri ikiwemo bandari za Tanga na Mtwara, Tanganyika na Nyasa na ujenzi wa viwanja vya ndege.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia, alisema ufadhili wa mradi huo utaiwezesha bandari hiyo ambayo ni muhimu pia kwa nchi za jirani hna Tanzania, kukuza uwezo wake, kuinua biashara na kutengeneza ajira. Alisema kutokana na mizigo kuchukua muda mrefu bandarini, hasara ya kiasi cha Dola za Marekani 200 hadi 400 iliyotokana na ucheleweshaji huo, sasa itaokolewa. Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema upanuzi wa bandari hiyo utabadili ufanisi wake na kuuboresha zaidi.

Profesa Mbarawa alisema pamoja na bandari hiyo, pia serikali inatekeleza miradi katika bandari zake mbalimbali ikiwemo kufunga vifaa vya kisasa na kuboresha bandari za maziwa makuu ili kusaidia bandari nyingine katika kusafirisha kiurahisi shehena. Naye Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke alisema mradi wa DSMGP utatekelezwa kwa sehemu ya programu kubwa inayoendelea kwa maendeleo ya jumla ya Bandari ya Dar es Salaam kwa ufadhili wa wabia kadhaa wa maendeleo.

Balozi Cooke alisema Serikali ya Tanzania inachangia Dola za Marekani milioni 63 kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania, huku Taasisi ya Trade Mark East African ikifadhili maboresho katika ufanisi wa maeneo na utendaji wa Bandari. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza inatekelezwa na Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi wa Mradi, Kampuni ya China Harbour Engineering Company-(CHEC) na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 28.

HABARI LEO

No comments: