Monday, July 31, 2017

WANAWAKE TUMIENI FURSA YA MIKOPO YA SERIKALI’

Na Mussa Mbeho,Tabora
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dk Thea Ntara  amewataka wanawake wajasiriamali mkoani humo kuchangamkia fursa mbalimbali   za mikopo  zinazotolewa na serikali ili kuweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuachana na Tabia ya kuwa tegemezi kwa waume zao  
Dk Ntara ametoa wito huo  katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake kuinuana kiuchumi katika halmshauri ya  Nzega Mji  lililofanyika katika ukumbi wa pick poit Pub wilayani Nzega.

Amesema wanawake  wote wajasiriamali mkoani humo  wanatakiwa kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashuri zao kwa kuunda vikundi mbalimbali ambavyo vitaweza kukopesheka kirahisi ili kuweza kuwasaidia kujikomboa na suala zima la umasikini kwa kuendeleza biashara zao.
Dk Ntana Ameongeza kuwa  mwanamke hapaswi kukata tamaa katika  mambo mbalimbali ya kimaendeleo  hasa kupitia biashara yake na kuwashauri kuongeza  ubunifu  ili kuweza kupata wateja wengi hali ambayo itasaidia kuza vipato vyao.

Aidha Dk Ntara ameyataka mabenki yote mkoani humo kutoa mikopo yenye riba nafuu ambayo itasaidia wanawake wengi kukopesheka na hatimae kujikomboa kiuchumi  kupitia biashara zao.
Hata hivyo  Dk Ntara amewaomba  wanawake wote mkoani humo  kuendelea  kushirikiana na serikali katika mapambao ya dawa za kulevya pamoja na mimba za utotoni kwa kuwataja wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili sharia  iweze kuchukua mkondo wake.


Nae Mkuu wa wilaya ya Nzega bwana Godfrey Ngupura amewashauri wanawake kuacha tabia ya kuwa waoga katika kutafuta fursa na badala yake wajiamini kwa kile wananchokifanya huku akiahidi kuendelea kuwa nao bega  kwa bega katika kuwasaidia kujikwamua kiuchumi wanawake wote wilayani humo.

Kwa upande wake afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya  nzega mji  Bwana  Godson Halee amesema kuwa lengo la kuzinduliwa kwa jukwaa hilo ni kuwawezesha wanawake kukutana pamoja na kujadili fursa walizonazo katika suala zima la kujikwamua kiuchumi huku akibainisha kuwa katika msimu mpya  wa fedha wa 2017/2018 halmashauri hiyo imetenga jumla ya shilingi milioni 124 ili kuweza kuvikopesha vikundi vya wajasiriamali wanawake na vijana  katika halmashauri hiyo.
Uzinduzi wa jukwaa hilo la wanawake kuinuana kiuchumi Umekwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa nafasi ya mwenyekiti.katibu na mtunza hazina ambao watasaidia kusimamia shughuli zote za jukwaa hilo katika halmashauri ya Nzega Mji.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake