Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameaondoa maombi yake dhidi ya Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kuhusiana na shtaka la ugaidi dhidi yake.
DPP alikuwa amefungua maombi Mahakama ya Rufani akiomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio kuhusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
Maombi hayo ya DPP yalitarajiwa kusikilizwa leo Ijumaa, Agosti 11 na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mussa Kipenka, lakini DPP akaamua kuyaondoa kabla ya usikilizwaji.
Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka ameieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na maombi hayo.
Kutokana na nia hiyo ya DPP, wakili wa mjibu maombi, Richard Rweyongeza amesema kuwa hana pingamizi dhidi ya nia ya DPP kuyaondoa maombi hayo na Jaji Kipenka akatoa amri ya kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Awali, Lwakatare na mwenzake walikuwa Ludovick Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka manne likiwemo la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi kwa lengo la kumdhuru kwa sumu aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.
Mashtaka mengine yalikuwa ni ya ugaidi, wakidaiwa kuandaa mikutano ya kupanga makosa ya kigaidi na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo, Lwakatare kupitia kwa mawakili wake walifungua maombi Mahakama Kuu wakipinga mashtaka hayo yaliyokuwa yakiangukia katika Sheria ya Ugaidi.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri ilikubaliana nayo na akamfutia Lwakatare mashtaka hayo ya ugaidi na hivyo kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama ambalo haliangukii katika sheria hiyo ya ugaidi.
DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ndipo akafungua maombi ya kibali kufungua maombi nje ya muda, ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia mashtaka hayo ya ugaidi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake