Katika siku za
hivi karibuni kumejitokeza kikundi cha watu wanaotumia vibaya jina la Jeshi la
Polisi kwa kujifanya ni Maafisa wa Jeshi la Polisi na kuwatapeli watu kwa
kigezo cha kuwapatia ajira.
Watu hao
wamesambaza taarifa kupitia mitandao ya kijamii inayosomeka ‘Vigezo sifa za kujiunga na Jeshi la Polisi’,
huku ndani yake ikitaja sifa ambazo kwa mujibu wa kikundi hicho ndizo
anazopaswa kuwa nazo mtu anayeomba nafasi ya kujiunga na Jeshi la Polisi.
Jeshi la polisi
linapenda kuwafahamisha wananchi kuwa taarifa hizo ni za uongo na zenye lengo
la kupotosha Umma kwa madhumuni wanayoyajua wao wenyewe. Pia zipo taarifa
ambazo hazijathibitishwa kuwa wapo watu wanaoombwa kutoa fedha na matapeli hao
ili waweze kuwapatia nafasi ya ajira hizo.
Wananchi
watambue kuwa Jeshi la Polisi lina utaratibu wake mzuri na wa wazi wa kuajiri. Pale
Serikali itakapotoa idhini ya kuajiri watumishi wapya utaratibu huo utatangazwa kwa wananchi ili waweze kuufuata kuomba nafasi
hizo.
Jeshi la Polisi
linawataka wananchi kutoa taarifa juu ya kikundi hicho kupitia kituo chochote
cha Polisi kilicho karibu nawe au ofisi za Serikali ili watu hao waweze
kukamatwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Wananchi
mnashauriwa kupata taarifa sahihi za Jeshi la Polisi kupitia website yake
ambayo ni www.policeforce.go.tz au
akaunti ya twitter www.twitter.com/tanpol
pamoja na Facebook www.facebook.com/tanpol
Imetolewa na:
Barnabas David
Mwakalukwa - ACP
Msemaji wa
Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya
Polisi,
S.L.P. 9141,
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake