Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godyfrey W. Zambi akisaini Kitabu cha wageni katika Maonesho ya Nanenane.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey W. Zambi akitoa maagizo kwa Wakala wa Vipimo kusimamia matumizi ya vipimo sahihi katika msimu wa ununuzi wa mazao.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey W. Zambi akipewa Maelezo na Afisa Vipimo juu ya Mizani ya iliyoundwa na Watanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godyfrey Zambi akielezwa athali za kutumia vipimo batili (kangomba)
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godyfrey Zambi akipewa Maelezo na Afisa Vipimo namna ya kutambua mawe sahihi ya Mizani yaliyo hakikiwa na Wakala wa Vipimo
Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi amepiga marufuku kutumia kipimo kinacho tumiwa na baadhi ya wanunuzi wa mazao katika mkoa huo maarufu kama Kangomba ambacho kimeonsha kutokuwa rafiki wa mkulima.
Zambi ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la wakala wa vipimo nchini (WMA), katika maonesho ya nane nane ambayo kitaifa yanafanyika katika mkoa wa Lindi kwenye viwanja vya Ngongo.
Akizungumza katika banda hilo, amewataka Wakala wa Vipimo kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali, ili wakulima na Wananchi kwa ujumla waweze kunufaika na mazao wanayolima pindi waendapo kuyauza wakati wa msimu.
Ameongeza kuwa, maafisa wa vipimo ni muhimu kwa kushirikiana na maafisa waliopo katika ofisi za wakuu wa mikoa katika kuhakikisha wakulima hawapunjwi pindi waendapo kuuza mazao yao kwakuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, huchezea mizani yao kwa lengo la kuwapunja wakulima kwa lengo la kupata faida zaidi.
Awali wakitoa maelezo kuhusu kangomba maafisa wa wakala wa vipimo walimuelezea mkuuhuyo wa mkoa namna kangomba inavyowapunja wakulima, kwa kuwa siyo kipimo sahihi kinachopaswa kutumika kununulia mazao.
Kufuatia maelezo kutoka kwa wakala wa vipimo ndipo ikamalazimu mkuu huyo wa kutoa tamko kali dhidi ya wale wote wenye kutumia kangomba katika kuuza au kununua mazao ya wakulima.
“Lazima tuelewe falasafa ya Rais wetu, anataka mapinduzi ya viwanda lakini mwenye kuzalisha malighafi ni mkulima hivyo lazima, katika mazao yake aone faida, vinginevyo atauchukia ukulima na kukatishwa tamaa”, alinukuliwa mkuu wa mkoa.
Wakala nchini imekuwa na jukumu la kuwapa wakulima elimu ya matumizi sahihi ya mizani iliyo hakikiwa na kutambua alama zinazowekwa kwenye vipimo vilivyohakikiwa na Wakala ambazo ni stika maalum, pamoja na kugongwa nembo ya Taifa na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika. Mfano kwa mwaka huu 2017, itasomeka namba 17.
Kwa upande wake Afisa Vipimo wa mkoa wa Lindi bw. Nyagabona Mkanjabi alisema, wamejipanga vizuri katika kusimamia matumizi ya vipimo sahihi na kuhakikisha mizani zote zinazotumika katika vyama vya ushirika vya msingi zinakaguliwa kabla ya misimu ya kuuza mazao kuanza huku aki wahakikishia kaguzi mbalimbali za kustukiza zinafanyika kipindi cha msimu wa kuuza mazao unapofika.
Pia, amewakaribisha viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi pamoja na wananchi wote kutembelea banda la wakala wa vipimo katika maonesho ya nanenane mkoa wa Lindi na kujionea Mizani mbalimbali zinazopaswa kutumika katika ununuzi wa bidhaa mbali mbali na mazao ukiwemo mzani wa digital wa tani 2 ambao unapima bidhaa/mazao na kutoa risiti hapo hapo
Akizungumza pembeni mwa mkutano huo, kaimu Afisa Vipimo mkoani hapo, Andrew Mbwambo ametoa wito kwa Wakulima, wafanyabiashara na Wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya kuchezea vipimo kwani kwa sasa adhabu ni kubwa baada ya Sheria ya Vipimo Sura namba 340 na Mapitio yake ya mwaka 2002 kufanyiwa marekebisho mwaka 2016.
Kila mwaka wakala wa vipimo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inashiriki maonesho mbalimabali ikiwapo ya Nanenane huku wakiwa na jukumu la kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wakulima na wanunuzi wa mazao na umuhimu wa kutumia vipimo sahihi.
Maonesho ya Nane nane kitaifa yamefanyika mkoani Lindi kwa mara ya tatu mfululizo huku yakiongozwa na kaulimbiu “Zalisha kwa tija mazao na biadhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa kati”.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake