TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Kitaifa ya Mhe. Abdel Fattah
Al Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini
Kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi,
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri atafanya Ziara ya Kitaifa nchini Tanzania wiki
ijayo. Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi nchini
Tanzania tangu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie madarakani.
Lengo la ziara hii ni kuimarisha na kukuza zaidi
mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya nchi
hizi mbili, ziara hii pia itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala
mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Rais Al Sisi atawasili nchini kupokelewa na
mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Rais Al Sisi mchana atakuwa na
mazungumzo (tete-a-tete) na mwenyeji wake kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi
(official talks) na baadae jioni Mheshimiwa Rais Al Sisi atahudhuria dhifa ya
kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake.
Tanzania na Misri zina mahusiano mazuri ya
kidiplomasia ya muda mrefu ambayo yamezidi kuimarika hasa katika miaka ya
karibuni. Ushirikiano huu unatokana na misingi ya mahusiano na mashirikiano ya
karibu sana kati ya Marehemu Baba wa Taifa na muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi mashuhuri wa Misri na
muasisi wa Jamhuri ya Taifa la Kiarabu
ya Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser. Uhusiano wa nchi hizi mbili umejengwa
katika misingi ya ushirikiano na maelewano katika Nyanja za kijamii, kiuchumi,
kisiasa, kiulinzi na kiusalama pamoja na medani za siasa za ushirikiano
kimataifa, kutetea haki za binadamu, kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika,
ukombozi wa Bara la Afrika na kupinga ukoloni, dhuluma na aina zote za
ukandamamizaji duniani. Uhusiano huu umejengwa katika Nyanja zote za uhusiano
katika sekta za huduma za kijamii na kiuchumi zikiwemo elimu, afya, kilimo,
mawasiliano, usafiri, ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa.
Misri ni nchi ya pili yenye uchumi mkubwa Barani
Afrika. Takwimu za mwaka 2016, zinaonesha kwamba pato la taifa (GDP) la Misri
lilikuwa Dola za Kimarekani Billioni 266.213. Sekta kubwa kabisa katika uchumi
wa Misri ni sekta ya huduma ( huduma za benki, mawasiliano, usafirishaji na
utalii) ambayo inachangia takribani asilimia 52.5 kwenye GDP. Viwanda
(manufacturing) inachangia asilimia 36.3, na kilimo asilimia 11.2.
Tanzania na Misri zinashirikiana katika ngazi za
taasisi za serikali ambazo ni Taasisi ya Udhibiti wa utawala ya Misri
(Administration Control Authority of Egypt) ambayo inashirikiana na Taasisi ya
kupambana na kuzuia Rushwa ya Tanzania (TAKUKURU), Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja zimesaini makubaliano ya
Ushirikiano na Hospitali ya El Shatby ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini
Misri, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina mashirikiano ya
kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa Shahada za juu za uzamili na
uzamivu na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri, Jeshi la Wananchi wa Tanzania
kupitia SUMA JKT wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya Polyserve
ya Misri .
Aidha, kutokana na takwimu za kituo cha Uwekezaji
(TIC) kimesajili jumla ya miradi nane kati ya mwaka 1990 hadi 2017, miradi hii
ina jumla ya thamani ya Dola za Kimarekani 887.02 na kutoa ajira zipatazo 953,
uwekezaji huo ni katika maeneo ya Kilimo, viwanda(mbao, mbolea, madini, dhahabu
na shaba) na sekta ya Huduma.
Hivyo ziara hii ina umuhimu mkubwa sana hasa katika
wakati huu ambapo msisitizo wa Serikali ni katika kujenga uchumi wa viwanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dar es Salaam
11 Agosti, 2017
|
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake