Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya maonesho ya kilimo ya Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017. (Picha zote na Mathias Canal)
Serikali imeongeza uzalishaji katika mazao makuu ya chakula hususani
mahindi, mchele, mtama, uwele, na mikunde jambo linalopelekea
kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 100.
Aidha, Uzalishaji mwingine umeongezeka kwenye mazao ya jamii ya mizizi kama muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo.
Hayo yamesemwa jana tarehe 01/08/2017 na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo
na Uvuvi, Mhe. Wiliam Tate Ole Nasha (Mb) wakati akizungumza na wakulima
wadau wa kilimo Mifugo na Uvuvi na wananchi kwa ujumla wakati wa
uzinduzi wa sikukuu ya wakulima – nane nane, Maonesho yenye kauli mbiu
ya “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili
kufikia Uchumi wa Kati” yanayofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa maonesho
ya kilimo wa Ngongo Mkoani Lindi.
Alisema kuwa Katika mwaka
2015/2016 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa
ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2014/2015. Mchango mkubwa katika
Pato la Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine
za kiuchumi.
Mchango huo mkubwa ni Kwa kuwa asilimia kubwa ya
Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, hivyo kilimo
kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umaskini.
Mhe Nasha Alisema kuwa uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi umeimarisha
zaidi usalama wa chakula na lishe nchini, ambapo katika mwaka 2015/2016
uzalishaji wa chakula ulikuwa ni tani milioni 16.2 ikiwa ni ongezeko la
tani milioni 0.7 (sawa na 4.5%) ikilinganishwa na tani milioni 15.5
mwaka 2014/2015.
Uzalishaji wa mazao ya nafaka umeongezeka
kutoka tani milioni 8.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 9.5 mwaka
2015/ 2016 ikiwa ni ongezeko la tani milioni 0.6 (sawa na 6.7%).
Uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka tani milioni 5.9 mwaka
2014/2015 hadi tani milioni 6.1 mwaka 2015/2016 sawa na ongezeko la tani
milioni 0.2 (sawa na 3.4%). Uzalishaji wa mchele uliongezeka kutoka
tani milioni 1.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 2.2 mwaka 2016 sawa
na ongezeko la tani milioni 0.3 (sawa na 15.8%).
Vilevile,
uzalishaji wa mazao ya chakula yasiyo nafaka umeongezeka hadi kufikia
tani milioni 6.7 ikilinganishwa na tani milioni 6.6 kwa mwaka 2014/ 2015
ikiwa ni sawa na ongezeko la tani milioni 0.1 (sawa na 1.5%).
Kwa ujumla uzalishaji wa mazao ya chakula ukilinganishwa na mahitaji ya
tani milioni 13.2 ya chakula na matumizi mengineyo katika mwaka
2016/2017 unaonesha kuwepo kwa ziada ya tani milioni 3.0 za chakula.
Kutokana na hali hiyo Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 123
ambayo ni ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na asilimia 120 ya
mwaka 2015.
Katika mwaka 2016/2017 idadi ya mifugo nchini
imefikia ng’ombe milioni 28.44, mbuzi milioni 16.67 na kondoo milioni
5.01. Pia, wapo kuku wa asili milioni 37.43, kuku wa kisasa milioni
34.5, nguruwe milioni 1.85 na punda wapatao 572,357. jumla ya mitamba
634 ilizalishwa kutoka mashamba ya Serikali na Kampuni ya Ranchi za
Taifa - NARCO ikilinganishwa na mitamba 646 iliyozalishwa mwaka
2015/2016. Aidha, jumla ya mitamba 10,820 ilizalishwa na Sekta binafsi
na kusambazwa kwa wafugaji wadogo nchini ikilinganishwa na mitamba
10,803 iliyozalishwa mwaka 2015/2016.
Mhe Nasha alisema kuwa
Vituo vya Kanda vimeendelea kuimarishwa kwa kupatiwa vitendeakazi,
ukarabati wa miundombinu na mitambo ili kuhakikisha upatikanaji wa
huduma ya uhimilishaji wakati wote.
Jumla ya dozi 100,000 za
mbegu bora za mifugo zilizalishwa ikilinganishwa na dozi 80,000 mwaka
2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390
mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake