Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Maji Mijini, Clement Kivegalo.
Pia, Kamwelwe amemwagiza mkurugenzi wa utawala wa wizara hiyo, Barnabas Ndunguru kuwahamishia Dodoma watumishi 178 wa wizara ifikapo Januari 30, 2018 la sivyo atamchukulia hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20, 2018 jijini Dar es Salaam, Waziri Kamwelwe amesema jana Januari 19, alizivunja bodi za maji safi za Mkoa wa Arusha na Musoma baada ya kujiridhisha kuwa utendaji wao si mzuri.
“Juzi tu niliuondoa utendaji wa Lindi, kuna tatizo la utendaji wa wakandarasi hapa Dar es Salaam, Chalinze na tuna tatizo Kigoma, mamlaka za maji za miji ya mikoa zinasimamiwa na mkurugenzi wa maji mijini, hapa tuna idara kama tatu au nne zinasimamia utekelezaji wa miradi hiyo,” amesema Mhandisi Kamwelwe na kuongeza,
Waziri Kamwelwe amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyeko ziara mkoa wa Mara amebaini kasoro za utendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) na kuagiza hatua zichukuliwe ikiwamo kuchunguzwa watendaji wote.
“Kupitia ziara ya Waziri Mkuu imebainika yapo matatizo yanayomhusu mkurugenzi wa Muwasa, Gantara Said na wahusika wote ameeleza wafanyiwe uchunguzi, hivyo kuanza leo Januari 20, natengua uteuzi wake na nafasi yake itakaimiwa na Petro Muhoja wa Mamalaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza, namwagiza mkurugenzi wa mamalaka ya maji Mwanza, asaidie mamlaka ya maji Musoma ili waweze kufanya kazi,” amesema.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment