Katibu Tawala wa wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Adam Bibangamba ( aliyesimama) akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mjadala wa elimu juu ya njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa wanawake wajawazito na kupinga mimba za utotoni wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika kata ya Ukwamani , wilayani humo. ( Picha na John Nditi).
Mkazi wa Kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo akichangia mada
Baadhi ya wananchi wa kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro wakisiiliza na kusoma vipeperushi vya elimu ya njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi vya akina mama wajawazito na kupinga mimba za utotoni, wakati wa mjadala wa uelimisghaji jamiii siku ya utepe mweupe iliyofanyika kwenye kata hiyo.
Wazee wa kata ya Ukwamani, wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro ( mstari wa mbele ) wakiwasikiliza wataalamu wa afya ( hawapo pichani) wakati wa utoaji wa elimu ya njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa akina mama wajawazito na kupinga vita kujifungulia kwa wakunga wa jadi na mimba za utotoni, wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika kwenye kata hiyo.
Mfanyakazi wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania, Lucy Nzuki ( mwenye kushika karatasi ) akiandika dodoso kwa mmoja wa wakazi wa Kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo , mkoa wa Morogoro wakati wa utoaji wa elimu ya njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa wanawake wajawazito na kupinga mimba za utotoni wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika kwenye kata hiyo wilayani humo.
Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania , Rose Mlay ( kushoto) akibadilishana mawazo na Mganga mkuu wa wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro , Dk Dennis Ngalomba ( kulia) na watendaji wengine wa wilaya hiyo mara baada ya kumalizika kwa majadiliano kati ya wananchi na wataalamu namna ya njia bora ya kupunguza vifo hivyo wakati wa utoaji wa elimu wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika kata ya Ukwamani , wilayani humo , majadiliano hayo yalikuwa na ujumbe wa “ Vifo vitokanavyo na uzazi havivumiliki “ Wajibika.
Na John Nditi, Gairo
WANAWAKE wajawazito 2,600 sawa na asilimia 27 kati ya 9,577 waliojifungulia zahanati na vituo vya afya kwa mwaka 2017 katika halmashauri ya wilaya ya Gairo , mkoani Morogoro walibainika kuwa chini umri wa miaka 20.
Hali hiyo ilisababisha kujitokeza kwa vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi unaochagiwa na uchungu mkali, kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua na kifafa cha mimba.
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto wa wilaya ya Gairo, Edifonzia Mhafigwa alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa katika mkutano wa kujadili utoaji wa elimu kuhusu kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi kwenye siku ya Utepe Mweupe ambayo kimkoa ilifanyika katika kata ya Ukwamani , wilayani humo.
Mbali na changamoto hiyo, wanawake wajawazito waliojifungulia kwa wakunga wa jadi kwa mwaka 2017 walifikia 1,270 , waliojifungulia njiani ni 108 , waliojifungulia nyumbani ni 180 na kwenye Zahanati walikuwa ni 3,482.
Alisema , jambo hilo linachangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo ya wanawake wajawazito kushindwa kuhudhuria kliniki kwa wakati ama kuchelewa kufijkishwa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua .
Naye Mratibu wa Afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Morogoro, Annua Mhogo alisema kuwa , mkoa huo una vituo 341 vya huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto (RCH), Vituo vinavyotoa elimu ya uzazi wa mpango 282 na vituo vya kujifungulia ni 298.
Mhogo alisema , watoto waliozaliwa kwa mwaka 2017 walikuwa ni 73,232 , ambapo vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa ni 1,335 wakati vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua ama baada ya kujifungua walikuwa ni 80.
Alisema takwimu za kimkoa zinaonesha kuwa wilaya hiyo inaongoza kuwa na idadi ya akina mama wanaojifungulia kwa wakunga wa jadi na mimba za utotoni ambao wanaozeshwa wakiwa bado na umri mdogo.
Naye Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania , Rose Mlay aliishauri Serikali kuendelea kuongeza wataaamu wa sekta ya afya wakiwemo wauguzi wenye ujuzi hasa kwenye zahanati vijijini ili kupunguza vifo hivyo.
Mlay pia aliwataka wanaume kuwajali wake zao wanapokuwa wajawazito kuwasindikiza kliniki ili elimu itakayotolewa na wataalamu wa afya hasa waauguzi iwe ni chachu ya kuhakikisha usalama wa mama na kiumbe kilichomo tumoni mwa mama mjamzito ili awezefungue salama katika vituo vya afya ama zananati yenye mtaalamu.
Nao baadhi ya wakazi wa Gairo ,Elieza Ernest ,Julieti Sangara , Lucia James pamoja na Andason Ndajiro kwa nyakati tofauti walisema ukosefu wa zahanati za kutosha katika vijiji vingi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito.
Walisema , hali hiyo inawalazimu kutembea umbali mrefu kuzifuata zahanati na vituo vya afya kuhudhuria kliniki wakati hawana kipato cha kuwawezesha kugharamia usafiri.
Hivyo walishauri , halmashauri ya wilaya ya Gairo kuweka utaratibu wa kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pamoja na kuwasambaza wauguzi na madaktari wa kutoka na vitendea kazi na dawa .
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Dk Dennis Ngalomba alisema, halmashauri hiyo ina vijiji 50 na kata 18 ambapo kulingana na sera ya afya ya kila kata iwe na kituo cha afya, upungufu ni vituo 17 , wakati zahanati zilizopo ni 24 na upungufu ni 26.
Hata hivyo alisema , jukumu la wananchi ni kuanzisha maboma na halmashauri itaendelea kumalizia kupaua hadi hatua ya kusajili zanahati na vituo vya afya juhudi ambazo zinaendelea kutekelezwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment