Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo akifunga
Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha
wataalam watambuzi hao mjini Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu (Elimu ya Watu Wazima),
Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kassim Kaoneka akitoa neno la awali kabla ya kumkaribisha
mgeni rasmi.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo (kushoto)
akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu (Elimu ya Watu
Wazima), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kassim Kaoneka.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto
wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha wataalam watambuzi hao
mjini Morogoro.
KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo
amefunga Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha
wataalam watambuzi hao mjiniMorogoro.
Akitoa hotuba yake, mbele ya walimu, maafisa ustawi
wa Jamii na baadhi ya madaktari, Mkongo amesema ana imani kubwa na wataalamu
hao ambao wamepatiwa mafunzo ya kubaini kwa kutumia vifaa maalum kuwa watafikia
malengo ya kazi waliyoelekezwa na Serikali ili kuboresha huduma ya elimu bora
kwa watoto wenye mahitaji maalum nchini.
“Ni matumaini yangu baada ya mafunzo haya kuwa kila
mmoja wenu atakuwa na ujuzi wa
kutosha kutumia vifaa maalum kuwabaini watoto wenye
changamoto za uoni hafifu, ujongeaji wa viungo vya mwili, usikivu, changamoto
nyingine ambazo hutegemea hali ya afya na mazingira,”Amesema.
Amesema Watoto hao wanatarajiwa kutoka rika la
miaka minne hadi sita na kwamba wataalam hao watatoa ushauri wa kitaalam na
kitabibu kwa wazazi na walezi wa watoto hao, na walimu wa watoto watakaobainika
hivyo ni vema wakaifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi mkubwa ili malengo ya
Serikali yatimie.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Morogoro amesisitiza kuchukuliwa
kwa hatua zinazostahili kwa watoto watakao bainika ili wapatiwe huduma
kulingana na hali waliyonayo na mahitaji yao halisi.
“Ninasisitiza kuwa watoto watakaobainika kuwa na
matatizo yanayohitaji matibabu, wazazi au walezi waelekezwe kuwapeleka katika
vituo vya afya kwa matibabu au uchunguzi zaidi, baada ya uchunguzi mzazi au
mlezi ashauriwe kumwaandikisha mtoto katika shule jumuishi, kitengo au shule
maalum iliyokamilika kulingana na aina ya mahitaji maalum aliyonayo mtoto,”amesema.
Amesema Watoto wote wanahitaji kupatiwa elimu iliyo
bora ili kujenga uhusiano unaokubalika katika jamii na kuandaa mazingira
yanayotawala maisha yao ya kila siku ili kuirahisishia Serikali kuandaa,
kupanga na kutekeleza mipango sahihi kulingana na aina ya mahitaji yao na
kupata elimu iliyo bora.
Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu
(Elimu ya Watu Wazima), Ofisi ya Rais TAMISEMI Kassim Kaoneka, akitoa maelezo
ya awali kumkaribisha mgeni rasmi, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ya siku
sita ni pamoja na kupata uelewa wa pamoja ili kupata vigezo vya kuwatambua
watoto wenye uhitaji maalum katika kada mbalimbali kama watoto wasioona, wasio
sikia, watoto wenye ulemavu wa viungo, watoto wenye changamoto za ufahamu,
pamoja na ulemavu wa akili.
Zoezi la kuwabaini wototo wenye mahitaji maalum
linakusudiwa kuanza nchini kote kwani vifaa vyote kwa ajili ya utambuzi tayari
vimekwisha gawiwa katika ofisi za Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Aidha, Kaoneka amesema Mpango wa kuwabaini wototo
hao unaenda sambamba na Mpango wa kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ambao upo
chini ya Programu ya LANES inayoratibiwa na kutekelezwa kwa pamoja kati ya
Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wataalam hao,
Salvatory Kitogwe amesema jumla ya washiriki wote ni 314 ambao wanatoka katika
mikoa mbali mbali na wao kama wataalam
wanasisitiza kufika kwa taarifa mapema mikoani na
wilayani ili kufanya zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum kuwa rahis
na kulifanya kwa ufanisi.
Mapema kabla ya Mafunzo hayo Mhe.Kassim Majaliwa,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mpango huo sambamba na
ugawaji wa vifaa maalum vitakavyotumika na pia aliagiza utekelezaji wake
ufanyike mapema iwezekanavyo ili Serikali ipange mipango yake na kuitekeleza
kwa wakati.
No comments:
Post a Comment