ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 31, 2018

MIPANGO YA MATUMZI YA ARDHI KUNUSURU MISITU NCHINI


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo (aliyesimama) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Dkt. Stephen Nindi wakiongoza kikao cha pamoja kati ya NLUPC na TFS juu ya maandalizi ya upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi za Misitu inayosimamamiwa na Serikali Kuu.


Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu, Sera na Mawasiliano (DLCCP) wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bibi Albina Burra (kulia) pamoja na Watalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wakifuatilia kwa maokini mazungumzo kati ya taasisi zao.

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inatarajia kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 120 vinavyozunguka misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya NLUPC and TFS kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC Dkt. Stephen Nindi ameahidi kuwa taasisi yake itatoa ushirikiano wa kitaalamu kwa ajili ya kunusuru rasilimali za nchi wakati wowote kwa faida ya nchi na watanzania wote.

Naye Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa mipango hiyo ya matumizi ya ardhi inalenga kumaliza changamoto zote ya kuhifadhi misitu nchini kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo pamoja na kuwasaidia wanavijiji kuwa na matumizi rafiki ya ardhi yatakayosaidia kutunza misitu hiyo.
“Mpaka sasa zaidi 60% ya misitu iliyopo nchini haijahifadhiwa na lengo letu ni kuhakikisha misitu hiyo inahifadhiwa. Hivyo nawataka wataalamu wa Tume pamoja na Wakala kuhakikisha lengo hili linafikiwa kwa kuweka mikakati ya kitaaaluma kwa kuzingatia wakati uliopo,” alisema Professa Silayo.

Professa Silayo anasema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali yanayoelekeza kutatua migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo ya jirani na hifadhi kwa kushirikisha wadau katika kuhakiki mipaka ya maeneo ya hifadhi kwa kuweka alama za kudumu; kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi; na kuzingatia utawala wa Sheria katika kusimamia rasilimali za maliasili.

Mtendaji huyo anaongeza kuwa uharibifu wa misitu nchini ni mkubwa katika maeneo ambayo vijiji vimeanzishwa ndani ya misitu bila kufuata sheria na TFS imeendelea kuzuia upanuzi zaidi wa vijiji hivyo, na hadi sasa kuna vijiji 228 vinavyofahamika na miji kadhaa.

NLUPC na TFS wameunda kikosi kazi kitakachoandaa mikakati ya namna bora ya kufanya kazi hiyo ambapo wameanza kwa kupitia orodha ya misitu ya hifadhi yenye migogoro kwa kanda zote saba za TFS. Kanda hizo ni za Mashariki, Kaskazini, Kati, Kusini, Nyanda za juu Kusini, Ziwa na Magharibi.
  

No comments: