Advertisements

Monday, October 22, 2018

Naibu Mkurugenzi UNEP azungumzia kujitambua kupata mafanikio

 Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Bi. Joyce Msuya akizungumza viongozi wanawake vijana kwenye mdahalo ambapo aliutumia kuhamasisha wanawake wengine kujituma uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Bi. Natalie Boucly. 
 Mkurugenzi wa uendeshaji wa Doctors’ Plaza, Bi. Sophia Byanaku akiuliza swali kwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Bi. Joyce Msuya (hayupo pichani) wakati wa mdahalo maalum kwa viongozi wanawake vijana ambapo walipata fursa ya kuhamasishwa kujituma na kujitambua uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya viongozi wanawake vijana walioshiriki kwenye mdahalo ulioendeshwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Bi. Joyce Msuya (hayupo pichani) ambapo aliutumia kuhamasisha wanawake wengine kujituma uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam
Baadhi ya viongozi wanawake vijana wakiuliza maswali kwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Bi. Joyce Msuya (hayupo pichani) wakati wa mdahalo maalum uliotumika kuhamasisha wanawake wengine kujituma na kujitambua ambapo umefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Bi. Joyce Msuya katika picha ya pamoja na viongozi wanawake vijana mara baada ya kumalizika kwa mdahalo huo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. 

Na Mwandishi wetu
SUALA la kujitambua na kutambua nini mahitaji yako ni moja ya chanzo cha mabadiliko yanayohitajika katika maisha, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira-UNEP, Joyce Msuya amebainisha.
Alisema hayo akizungumza na wanawake mbalimbali waliofika kusikiliza historia yake na jinsi alivyoweza kumudu maisha ya mama, mke na mfanyakazi katika mashirika mbalimbali ya kimataifa na kupanda ngazi.
Aidha alisema pamoja na kujitambua mtu anatakiwa kufanya kazi kwa kuwajibika, kujisukuma zaidi katika kazi na kufanya maamuzi ya kushirikisha familia hasa patna.
Msuya ambaye alianza kazi ya UNEP mwaka huu mwezi wa nane baada ya kupitia Benki ya dunia na mashirika mengine kadhaa alisema mfumo wa Tanzania wa shule, malezi ndiyo iliyofanya kuunganisha nguvu, uwezo na ujasiri wa kuweza kufanya mambo ambayo yamemfanya kupata nafasi kubwa zaidi.
Alisema mfumo wa Tanzania wa maisha umekuwa msukukumo mkubwa kwake kwani  aliweza kuishi na watu tofauti na kuvumilia huku akitekeleza wajibu wake kwa kujiongeza zaidi.
Alisema kutokana na juhuzi za wazazi wake katika kusimamia malezi aliweza kupata maarifa zaidi ya kuishi kwa kuhudhuria shule za umma za Forodhani, Jangwani na Weruweru kisha kuchukua mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT) Mafinga na kumalizia mafunzo hayo Mlalakua.
“Ukweli ni kuwa wazazi wangu walitaka tuishi maisha ya kawaida kama watanzania wengine ndiyo maana walinipeleka shule za bweni na kuhakikisha naenda jeshini. “ alisema Mkurugenzi huyo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Anasema malezi ya kujitegemea yamemfanya awe na uwezo wa kufanya bajeti hali ambayo ilimwezesha kuishi vyema Scotland na hata alipoenda kuchukua shahada yake ya pili nchini Canada.
“Kusema ukweli  Baba na mama walinitengenezea mfumo mzuri wa kuishi hasa pale walipojenga na kunihimiza kufanya kazi na kusoma wakati nikiwa mdogo.” Alisema Msuya.
Anasema amevuka vigingi vingi hasa kwenye muwashawasha wa masomo lakini kama walivyo watu wote alifanya maamuzi makini kuzingatia ushauri na kile anachokipenda.
Akiulizwa nini hasa kinamsukuma, alisema kwamba familia ni kitu muhimu kwake na kwamba amefanya mambo mengi akiwa na familia yake kuanzia mume wake ambaye wamo katika ndoa kwa miaka 20 na kujaliwa kuwa na watoto wawili.

Alisema kupitia familia na haja ya kukuza familia bora ilimfanya kubadilisha kazi kwa kuangalia hali ya baadae ya familia, kitu ambacho anaamini kwamba kimemsaidia sana kusonga mbele katika kupata nafasi za juu kila mahali alipojaribu,
Pamoja na kuzungumzia mafanikio yake ikiwamo jinsi alivyopanda madaraja mbalimbali, Msuya alisema kwamba ipo haja ya watu  kumeza kiburi chao na kujifunza kutoka kwa wengine namna ya kufanya mambo ili yaendane na mahitaji ya kitaaluma.
Aidha ili kuwa na maendeleo alitaka watu kutokata tamaa na kuridhika kwani kuridhika kunasababisha kudumaa kwa safari ambayo inatakiwa kwenda kasi na kuwa ya mafanikio.
Aidha alisema mazungumzo baina ya patna na familia nzima, na kuwa wazi inasaidia sana kufanya mambo yaweze kwenda kama yanavyotakiwa ili kila mmoja ajue kwanini ni lazima kufanya maamuzi fulani katika familia.
Alisema maamuzi yake ya kwenda China na Korea yamesaidia kuendelea kuwa na familia iliyo pamoja.
Pamoja na kuhimiza uhai wa familia kujituma, kuwajibika, kuwa wazi na kujitambua pia amewataka wanawake kujua majukumu yao kama mke, kama mama na kama mfanyakazi.
Alisema pamoja na majukumu yake huwa anafurahi kuwa mke nyumbani na pia kuwa mama.
“Watu wakitarajia wewe kufanyakazi kwa asilimia 100 wape asilimia 200” alisema Msuya huku akisisitiza watanzania wawe na njaa ya kufanya vyema zaidi kwa kujifunza na kutekeleza.
Mkuu huyo wa UNEP pamoja na kufanya mazungumzo hayo pia alifanya ziara katika shule ya Jangwani.
Alisema nafasi za juu zinaweza kupatikana kwa kukazania elimu, kujituma kwabidii na kujifunza kutoka kwa wengine hasa nchi zilizoendelea.
Alisema wakati yeye anasoma hapakuwepo na nafasi kubwa kwa wasichana lakini kwa sasa nafasi zipo wazi na wakijipanga vyema watakuwa miongoni mwa watu wanaoendesha uchumi na kutegemewa na familia zao.
Katika mazungumzo hayo Mkurugenzi wa uendeshaji wa Doctors’ Plaza, Bi. Sophia Byanaku alisema amefurahishwa sana na simulizi na Naibu Mkurugenzi huyo na kusema limempa msisimko mkubwa na ari mpya ya kufanyakazi.
Alisema akiwa kama mwanamke ameweza kujitambua katika mazungumzo hayo na kujiweka sawa katika kuhakikisha kwamba anawajibika katika kuwa mwanamke mzima yaani kuwa mama, mke na mtaalamu.
Naye Mkurugenzi Mkazi The Nature Conservancy, Bi.  Lucy Magembe alisema amepata furaha kubwa kuona jinsi Msuya alivyopambana kufikia hatua hiyo na kusema wanawake wana jambo la kujifunza kutoka kwake, hasa maana ya familia na uwajibikazi uliowazi katika kazi.

No comments: