ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 19, 2018

Wakati gani Tanzania inaweza kuomba msaada wa uchunguzi kwa vyombo vya nje?

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni wakati gani Tanzania inaweza kuomba usaidizi wa vyombo vya upelelezi vya nje kuchunguza matukio makubwa ya kihalifu ikiwamo ya watu kutekwa, kupotea au ugaidi?

Je, wakati umefika kuwashirikisha wataalamu wa kimataifa kuchunguza kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane; mwandishi wa habari, Azory Gwanda; kushambuliwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na hivi karibuni kutekwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’?

Maswali haya yameibuka kwa nguvu wiki hii kufuatia kutekwa kwa bilionea huyo katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay, Dar es Salaam, ikiwa ni miongoni mwa matukio ya utekaji ambayo yamelishtua Taifa miaka ya karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya polisi, Mo alitekwa alfajiri Oktoba 11 na Wazungu wawili waliotumia gari aina ya Toyota Surf na kutokomea naye kusikojulikana.

Tayari Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuf Masauni amekwishaweka wazi msimamo wa Serikali kuwa haipo tayari kuomba msaada wa wachunguzi kutoka nje.

Masauni alisema vyombo vya upelelezi vya ndani vina uwezo mkubwa wa kuchunguza tukio hilo na kutoa majibu.

Kauli ya Masauni imewaibua wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wanaodai kuwa wakati umefika kwa Tanzania kuomba msaada kutoka nje ya nchi wakitoa mifano ya matukio ya nyuma ambayo yamechukua muda mrefu kuchunguzwa bila majibu.

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga aliliambia Mwananchi jana kuwa, Sheria ya Msaada katika Masuala ya Jinai (Mutual Assistance in Criminal Matters Act) ya mwaka 1991 inaweza kutumika kuomba usaidizi toka nje.

Alisema sheria hiyo inaainisha mambo mbalimbali na jinsi Tanzania inavyoweza kuomba msaada wa upelelezi wa masuala fulani ya jinai katika nchi za Jumuiya ya Madola au mataifa mengine ya nje.

Kifungu cha 4 (c) cha sheria hiyo kinamwezesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuiandikia mamlaka ya nchi anayotaka msaada kuomba kuonyeshwa au kutambuliwa kwa mashahidi au watuhumiwa wa makosa ya jinai.

“Kama hujui kabisa ni nani na utambulisho wa aliyemchukua sheria hii inakuwa ngumu ku-apply (kutumika). Lakini kwa case (suala) ya Dewji (Mo) inaweza kutumika baada ya polisi kusema Wazungu ndiyo walihusika. Hii inatoa uhalali wa kuomba msaada kutoka nje ya nchi,” alisema Henga.

Alisema ingawa sheria hiyo haijataja muda gani nchi inaweza kuomba usaidizi, kushindwa kwa vyombo vya ndani kutoa majibu ya kutoweka kwa watu mbalimbali kunaonyesha umuhimu wa kuitumia.

“Kama matukio haya ya zamani na yanaendelea, tuombe wenye utaalamu mkubwa wa investigation (uchunguzi) waje. Chochote kifanyike kuwapata hawa ndugu zetu.”

Alipoulizwa jana ni wakati gani na katika mazingira gani Serikali itakuwa tayari kushirikisha wataalamu wa nje katika upelelezi, Naibu Waziri Masauni alikataa katakata kuzungumzia suala hilo.

“Sioni kama ni busara kuendelea kujadili hili suala, tunawaweka ndugu kwenye wakati mgumu zaidi, halina tija. Serikali inafanya kazi usiku na mchana kumtafuta Dewji, cha msingi ni matendo na si maneno, acheni vyombo vifanye kazi yake,” alisema Masauni.

Ombi la kwanza kwa Serikali kualika wachunguzi wa nje lilitolewa na viongozi Chadema pale walipoziomba mamlaka zilete wataalamu wa nje kuchunguza kupotea kwa kada wao, Ben Saanane. Saanane alitoweka Novemba 15, 2016.

Katika kikao cha Bunge mjini Dodoma Aprili, 2017, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliitaka Serikali ieleze kwa nini haioni umuhimu wa kuwashirikisha wachunguzi wa nje kama Scotland Yard (wa Uingereza) kupeleleza kupotea kwa Saanane.

Akijibu kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliweka wazi kuwa Tanzania bado inaweza kufuatilia, kuchunguza na kutoa majibu kwa matukio ya kutekwa na kupotea watu.

“Taifa letu lina uwezo wa kufanya ufuatiliaji wa kutambua matukio haya ya mtu kufa ama kupotea. Serikali haina kikomo cha uchunguzi kutegemea na nature (asili) ya tatizo lenyewe. Uchunguzi huu (wa Ben Saanane) utakapokamilika taarifa itatolewa,” alisema Majaliwa.

Wakati huo ilikuwa imepita miezi mitano tangu Saanane apotee na leo ni takribani miaka miwili.

Tukio lingine lililoibua shinikizo la kutaka wataalamu wa upelelezi wa nje waitwe ni lile la kushambuliwa risasi Lissu, Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.

Kama ilivyokuwa kwa Saanane, Serikali ilitoa msimamo ikisema kuwa halitachunguzwa na vyombo vya nje kwa kuwa vyombo vya ndani vina uwezo.

“Hawa watu wanafanya uhalifu hapa Tanzania, upelelezi utafanywa na vyombo vyetu, watakamatwa na vyombo vyetu…sasa ukimtoa mtu mbali bado atatakiwa awaulize watu wa hapa,” alisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.

Ingawa matukio kama ya kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda, Novemba 2017 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye, Julai mwaka huo, hayajawahi kupata shinikizo kubwa la kutaka wapelelezi wa nje, kuendelea kwa matukio hayo kunaamsha shauku ya kuitwa kwa wataalamu hao kusaidia kutoa majibu.

No comments: