ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, October 9, 2019
KONGAMANO LA KUMBUKUMBU YA MIAKA 20 YA KIFO CHA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE
By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametaja sifa alizokuwa nazo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akisisitiza kuwa “kiongozi ni sawa na mtu mwingine na haikufanyi uwe na haki zaidi kuliko mtu mwingine”.
Kikwete pia amesema miongoni mwa urithi wa Mwalimu Nyerere ni kutotishwa na hoja na mara kadhaa akisema “hoja haipigwi rungu”.
Alisema hayo jana wakati wa Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Nyerere na ingawa hotuba yake haikurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio, ilisambaa kwa kasi mitandaoni kutokana na watumiaji kutuma vipande vya nukuu.
Nyerere, ambaye aliongoza harakati za uhuru uliopatikana bila ya kumwaga damu, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 akiwa Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza.
Kikwete alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyokuwa inaongozwa na mada kuu “Urithi wa Mwalimu Nyerere Katika Uongozi, Maadili, Umoja na Amani katika Ujenzi wa Taifa”.
Kikwete ambaye alikuwa Rais kati ya mwaka 2005 na 2015, alisema mwaka 1978 kulikuwa na maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu waliokuwa wanapinga wabunge kujiongezea mshahara.
“Baada ya kujiongezea masilahi walifanya kikao cha wabunge Pemba, wakapigwa picha wako kwenye mabembea. Maana pale Mzee (Abeid Amani) Karume alijenga viwanja vya kustareheshea watoto. Kwa hiyo wabunge nao wakaingia humo, (gazeti la) Daily News likatoa ile picha front page (ukurasa wa kwanza),” alisema Kikwete.
Alisema baada ya kuona picha hiyo kwenye gazeti, wanafunzi wakaamini wabunge wamekwenda Pemba kusherehekea baada ya kujiongezea maslahi, hivyo wakaamua kuandamana.
Alisema maandamano hayo yalizuiwa na polisi maeneo ya Manzese wilayani Kinondoni na wanafunzi hao walifukuzwa chuo akiwemo Anselm Magige ambaye ni mtoto wa Mwalimu.
Alisema kutokana na maandamano hayo, Mwalimu aliitisha vikao vya CCM na katika kikao cha Kamati Kuu aliwaeleza wajumbe kwamba kwenye maandamano hayo kulikuwa na makaratasi yenye hoja za kisiasa; kuwa na vyama vya siasa, vyama huru vya wafanyakazi na wafanyakazi wawe na uhuru wa kugoma.
Kikwete alisema kwenye kikao hicho, Mwalimu aliwapa makaratasi na kuwataka watoe majibu, karibu wote walisema huo ni “uhaini”, wanafunzi hao “wakamatwe na wawekwe kizuizini”.
“Mwalimu akawaambia hivi ‘mawazo hayapigwi rungu. Mawazo yanashindwa na mawazo yaliyo bora zaidi. Maadam wamejenga hizi hoja. Sisi hoja zetu za kuwajibu ni zipi? Alikuwa hatishwi na hoja. Hoja zikitoka anasema lazima zijibiwe. Hoja haipigwi rungu, hoja inashindwa na hoja iliyo bora zaidi ya ile iliyotoka,” alisema Kikwete akimnukuu Mwalimu.
Alisema Mwalimu alimhoji aliyekuwa waziri mkuu wakati huo, Rashid Kawawa akisema: “Rashid, wewe si ulikuwa TFL? Si mlikuwa mnagomesha watu? Umeingia serikalini kugoma ni marufuku? Hawa wanataka maelezo. Wakati wa kudai uhuru mlikuwa mnagomesha watu, sasa baada ya kupata uhuru hamtaki watu wagome?” alisema.
Mbali na sifa hiyo, Kikwete pia amewataka viongozi kujishusha kama Mwalimu Nyerere alivyoonyesha thamani ya utu.
“Mwalimu ukikaa naye hupati ile hofu kwamba umekaa na Rais, mtu ambaye anaweza kuamuru weka ndani na ukawekwa ndani. Mwalimu hakuwa hivyo, unakaa naye anakwambia ‘hujambo, Jakaya kumbe na wewe kigogo’. Ndivyo alivyokuwa,” alisema Kikwete.
“Mwalimu alikuwa akisisitiza utu, lakini kuna dhamana ya uongozi.
“Dhamana ya uongozi haikufanyi wewe uwe ni mtu zaidi ya raia wengine wowote waliopo pale. Haikufanyi wewe uwe na haki zaidi kuliko mtu mwingine ambaye si kiongozi. Anao wajibu wake wa uongozi kwako na wewe unao wajibu wako kwa kiongozi wako.
“Na hili ni jambo kubwa kwa viongozi kutambua kwamba kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi. Kujimwambafai mwambafai (kujifanya mwaba) hivi wala hakukufanyi uwe kiongozi zaidi. Una wakati wa kutekeleza majukumu yako lakini unapokuwa na binadamu wenzako ni wanadamu kama wewe.”
Pia alieleza jinsi Nyerere alivyoishawishi CCM ikubaliane na matokeo ya ripoti ya Tume ya jaji Francis Nyalali kuhusu mfumo wa siasa unaotakiwa wakati dunia ikiwa katika mageuzi ya kuelekea vyama vingi.
Alisema pamoja na asilimia 80 kuonyesha kuwa Watanzania walitaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja, Nyerere, ambaye wakati huo alikshang’atuka lakini akaendelea kuwa mwenyekiti wa CCM alisema “tuwasikilize wachache”.
Kikwete alitaja pia sifa ya kujitolea akitoa mfano wakati Nyerere alipoacha kazi ya kuajiriwa ya ualimu na kwenda kupigania uhuru kupitia Tanu.
“Inahitaji ujasiri wa kuamua kuacha kazi yenye mshahara na kubaki kuwa Rais wa Tanu, (kazi) isiyo na mshahara na kubaki kuzunguka kudai uhuru ambao haujulikani utapatikana lini. Kwa moyo wake wa upendo aliamua kujitoa yeye kwa ajili ya masilahi ya wengi,” alisema.
Sifa nyingine alizotaja ni pamoja na Mwalimu Nyerere kutafuta uhuru kwa mazungumzo badala ya kumwaga damu, kuunganisha Tanganyika na Zanzibar akishirikiana na Abeid Karume, kujenga taifa lenye amani na mshikamano, kupenda kuwashirikisha vijana katika uongozi na kupigania uhuru wa nchi nyingine za Afrika.
Mbali na Kikwete, viongozi wengine waliotoa mada ni pamoja na katibu mkuu mstaafu wa CCM, Wilson Mukama aliyezungumzia nafasi ya maadili katika uongozi.
Huku akinukuu kauli za Mwalimu Nyerere, Mukama aliwataka viongozi kujiheshimu na kuzingatia miiko na maadili ya uongozi.
“Ukipewa uongozi ni lazima ujiheshimu. Huwezi ukapewa kazi ya kuongoza nchi halafu ukaongoza nchi kihunihuni,” alisema Mukama.
Naye Dk Haruni Kondo alisema Taifa limeiacha misingi ya Mwalimu Nyerere na kuingia kwenye janga la rushwa.
“Mwalimu alitaja maadui watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi. Lakini tunaongeza adui wa nne; rushwa. Tulitoka kwenye reli baada ya kuacha Azimio la Arusha na kwenda kwenye Azimio la Zanzibar,” alisema akimaanisha uamuzi wa CCM uliolegeza masharti yaliyobana viongozi.
Alisema baadaye viongozi waliuza mashirika ya umma na kusababisha ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kongamano hilo lililoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment