Advertisements

Tuesday, September 29, 2020

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA IMEFANIKIWA KUKAMATA DAWA ZA KULEVYA AINA YA MIRUNGI(KILO 343.7) NA HEROIN (GRAMU 448.14)


NA EMMANUEL MBATILO

Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na taasisi na vyombo vya usalama nchini wamefanikiwa kukamata takribani kilo 343.7 za dawa za kulevya aina ya mirungi pamoja na heroin yenye uzito wa gramu 448.14 katika matukio mawili tofauti septemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji amesema mamlaka ilimkamata Mary Edson Mtambo (25) mkazi wa Tegeta kwa Ndevu ambaye alikuwa akisafirisha kifurushi cha vitabu viwili ambavyo ndani yake kuliwekwa unga wa dawa za kulevya aina ya Heroin wenye uzito wa gramu 448.14.

Aidha Kamishna Jenerali Kaji amesema Mamlaka iliwakamata watuhumiwa George Justine Mathew (21) mkazi wa Kigoma Mjini akiwa na maboksi mawili yenye jumla ya Kilo 16.05 ya majani makavu ya dawa za ya kulevya aina ya Mirungi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa Kilo 32.2 kwenye eneo la kutuma na kupokea vifurushi Posta Mkoani Kigoma.Pia walimkamata Alex Benedicto Ntiruka (31) Mkazi wa Kasulu Mkoani Kigoma ambaye alikamatwa akiwa na maboksi mawili yenye jumla ya vifurushi nane vya majani makavu ya dawa za kulevya aina ya Mirungi yanayokadiriwa kuwaq na uzito wa Kilo 16 akiwa anafanya maandalizi ya kwenda kuyatuma.

Pamoja na hayo amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba Mamlaka hiyo ilibaini kuwepo kwa maboksi ya majani makavu yanayotumwa kupitia Mkoa wa Kigoma mpaka Jijini Dar es Salaam, kwenda nchi za Ulaya na kukamata jumla ya Kilo 279 iliyokuwa ikitumwa kutoka Kigoma.

“Mtumiwa Alex Benedicto Ntiruka aliyekamatwa na Kilo 16.05 yupo kwqenye mtandao wa wanaopokea na kutuma kiwango Kikubwa cha dawa za kulevya aina ya Mirungi ilizokamatwa Kigoma na Dar es Salaam na baada ya kufuiatilia walibaini kuwa ni dawa za kulevya aina ya Mirungi ambayo pamoja na Kilo hizo 48.25 maboksi haya yanakuwa jumla ya Kilo 343,7 ambazo watuhumiwa wake wengine tunaendelea kufatilia”. Amesema Kamishna Jenerali Kaji.

Pamoja hayo Mamlaka hiyo inawashukuru wasafirishaji vifurushi kwa ushirikiano katika vita ya dawa za kulevya na bado wanataka wananchi na jamii kwa ujumla kushiriki katika vita dawa za kulevya kwa kuwafichua wahalifu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapowaona.

No comments: