Advertisements

Monday, October 19, 2020

Mwalimu aliyekatwa kichwa kwa kuonesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Muhammad alitishwa kabla ya kuuawa


PARIS, UFARANSA

MWALIMU aliyekatwa kichwa katika mtaa nchini Ufaransa alikuwa amepokea vitisho baada ya kuwaonesha wanafunzi vibonzo tata vya Mtume, vimeripoti vyombo vya habari vya Ufaransa.

Awali Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema ukatwaji wa kichwa wa mwalimu katika kitongoji kilichopo kaskazini magharibi mwa mji wa Paris -Ufaransa ni Shambulio la ugaidi wa uislamu.

Mwalimu huyo anasemekana kuwa alikuwa akiwaonesha wanafunzi vibonzo tata vya Mtume Mohammad.

Mshambuliaji alipigwa risasi na kuuawa na polisi .

Macron amesema kuwa mwalimu huyo ambaye hajatambuliwa jina lake aliuawa kwasababu alifundisha uhuru wa kujieleza.

“Hawatashinda… Tutachukua hatua,” alisema rais alipokuwa katika eneo la tukio.

Shambulio hilo lilitokea Ijumaa saa kumi na moja jioni kwa saa za Ufaransa karibu na shule.

Polisi wa kukabiliana na ugaidi wanafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mshambuliaji aliyekuwa na kisu alipigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakijaribu kumkamata baada ya shambulio hilo.

Polisi bado hawajatoa ripoti kuhusu utambulisho wake, ingawa ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa vinasema kuwa alikuwa na umri wa miaka 18 mwenye asili ya Chechnya ambaye alizaliwa Moscow Urusi.

Kesi inaendelea mjini Paris juu ya mashambulio ya mwaka 2015 ya wanamgambo wa kiislamu dhidi ya Jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo, ambalo lililengwa na washambuliaji kwa kuchapisha katuni za Mtume Mohammad.

Wiki tatu zilizopita, mwanaume aliwashambulia na kuwajeruhi watu wawili nje ya ofisi za zamani za gazeti hilo.

Mwanaume aliyekuwa amebeba kisu kikubwa alimshambulia mwalimu katika mtaa wa Conflans-Sainte-Honorine, na kukata kichwa chake.

Duru za polisi zilisema walioshuhudia walimsikia mshambuliaji akisema “Allahu Akbar”, au “Mungu ni mkubwa”, kulingana na shirika la habari Reuters.

Mshambuliaji alitimua mbio, lakini polisi waliofahamishwa na umma walikimbilia katika eneo la tukio haraka.

Maofisa walikabiliana na mwanaume huyo katika wilaya iliyopo karibu ya Éragny.

Walipaza sauti kumwambia ajisalimishe, inasemekana aliwatishia.

Polisi wakampiga risasi ambapo alikufa muda mfupi baadae.

Kwa sasa eneo la tukio limefungwa, huku uchunguzi ukiendelea.

Watu tisa, akiwemo mtoto, wamekamatwa, duru za mahakama zimeviambia vyombo vya habari vya Ufaransa .

Waliokamatwa wanaripotiwa kuwa ni pamoja na ndugu wa mshambuliaji na wazazi wa mtoto anayesoma katika shule aliyekuwa akifundisha mwalimu huyo.

Kwa Mujibu wa gazeti la Le Monde mwalimu aliyeuawa alikuwa akifundisha masomo ya Historia na Jiografia, na alikuwa akizungumza na wanafunzi kuhusu uhuru wa kujieleza kuhusiana na vibonzo vya Mtume Muhammad , jambo lililosababisha hasira miongoni mwa baadhi ya Waislamu wakati Charlie Hebdo lilipochapisha vibonzo hivyo.

Mwalimu huyo anadaiwa kuwa alikuwa amewashauri wanafunzi Waislamu kuondoka darasani iwapo wangehisi somo hilo lingewakwaza.

Mapema mwezi huu, baadhi ya wazazi Waislamuwalilalamikia shule kuhusu uamuzi wa mwalimu huyo wa kutumia katuni moja au zaidi ya moja kama sehemu ya majadiliano kuhusu kesi ya Charlie Hebdo, kulingana na vyombo vya habari vya Ufaransa

“Kulingana na mwanangu wa kiume, alikuwa mwalimu mzuri sana, rafiki mkubwa, na mwema sana ,” mzazi kutoka shule hiyo , Nordine Chaouadi, ameliambia Shirika la habari la AFP.

Akizungumzia kuhusu shambulio hilo la Ijumaa Charlie Hebdo alitweet : “Kutovumiliana kumefikia kiwango kipya na inaonekana hakuna lolote la kuzuwia ugaidi kuingia nchini mwetu .”

Kama itafahamika kweli kuwa sababu ya kuua ilikuwa ni hiyo, litakuwa ni jambo la kushitusha sana kwa Ufaransa , anasema mwandishi wa BBC wa Paris Hugh Schofield.

Wataliangalia shambulio kama si shambulio la kikatili, bali ni shambulio la ukatili dhidi ya mwalimu kwa kufanya kazi yake ya kufafanua jambo.

Ufaransa imeshuhudia wimbi la ghasia za kiislamu tangu shambulio la mwaka 2015 dhidi ya Charlie Hebdo ambalo liliwauwa watu 12, wakiwemo wachoraji maarufu wa vibonzo.

Ufaransa inasema nini kuhusu shambulio?

Mauaji yanaonesha kuwa ni shambulio la ugaidi la kiislamu, Macron aliwaambia waandishi wa habari katika eneo la tukio.

“Mmoja wa raia wetu ameuawa leo kwasababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi kuhusu uhuru wa kujieleza ,” alisema.

Bunge la Ufaransa na wabunge walisimama kwa muda kutoa heshima zao kwa mwalimu aliyeuawa Ijumaa na kulaani shambulio la mauaji.

Waziri wa elimu Jean-Michel Blanquer alitweet kwamba mauaji ya mwalimu ni shambulio kwa Jamuhuri ya Ufaransa.

Alisema yuko pamoja na familia ya mwalimu , na umoja na mshikamano ndio jibu pekee kwa ugaidi wa kiislamu .

No comments: