ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 28, 2020

KAMATI YA USALAMA WILAYA YA IKUNGI SINGIDA YAKAGUA MIRADI YA ELIMU NA AFYA

Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakijadiliana wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Elimu na Afya wilayani humo. Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.
Moja ya chumba cha darasa kilicho kaguliwa na kamati hiyo.
Baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa.
Muonekano wa vyoo vya Shule ya Msingi vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Ukaguzi ukiendelea. 

Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua ujenzi wa Chuo cha Veta. Kushoto mbele ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.
Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Moja ya chumba cha darasa cha shule ya sekondari kilicho kaguliwa na kamati hiyo.
Jengo la Maabara lililokaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa vyoo vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Ikungi

KAMATI ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Elimu na Afya ambapo mbali na kupongeza usimamizi wa fedha zilizoletwa na Serikali juu ya miradi hiyo, iliwataka baadhi ya wasimamizi wa miradi hiyo kukamilisha kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wa miradi ya Elimu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, alisema ni lazima madarasa na vyoo vikamilike kwa wakati ili yaanze kutumika mapema mwakani na kuondoa changamoto ya vyumba vya madarasa iliyokuwepo kwenye shule hizo .

Aidha pamoja na mapungufu machache yaliyobainishwa na kamati wakati wa ukaguzi, kamati iliridhishwa na miradi hiyo kwa kuwa thamani ya fedha za serikali katika miradi inaonekana ambapo pia ilimtaka Mhandisi wa Halmashauri kuhakikisha anasimamia maboresho na mapungufu yaliyojitokeza na kutoa msaada wa kitaalamu kwa kila mradi uliokutwa na dosari.

Kwa shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, Mpogolo alizielekeza Serikali za vijiji na Kamati za Maendeleo ya Kata kuanza mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo na kuongeza kuwa serikali itaunga mkono katika ukamilishwaji wa majengo ya shule hizo huku akiagiza afisa Mipango Miji na Mhandisi wa wilaya kukagua na kupima maeneo yote yenye shule shikizi na kupeleka mapendekezo katika vikao vya halmashauri juu ya ukamilishwaji wa shule hizo.

Katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Mpogolo, aliitaka kamati ya ujenzi iliyoteuliwa na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya usimamizi wa mradi ambao unaendeshwa kwa mfumo wa “Force Account” kuhakikisha wanakuwepo eneo la mradi kila siku kwa ajili kushauri kitaalamu na kusikiliza changamoto ambazo mafundi wanakumbana nazo wakati wa ujenzi.

Alisisitiza mradi huo, ambao ulitengewa kiasi cha sh. Bilioni 1.5 unatakiwa ukamilike kwa wakati na kwa thamani halisi kama ambavyo iliagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, katika ziara yake ya kampeni, ambapo alitoa siku 60 ili kukamilika kwa mradi huo na kuahidi kufika kwa ajili ya uzinduzi.

Katika ziara hiyo ya siku tatu, kamati pamoja na wataalamu wa halmashauri walitembelea na kukagua miradi yote ya Afya na Elimu inayotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi katika mwaka wa fedha 2019/2020 na yote ikiwa na thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 4.5.

Wakati huo huo, mkuu wilaya hiyo amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kuchunguza taratibu zote za ujenzi wa Madarasa Matatu na vyoo vya Shule ya Msingi Matongo baada ya kubainika ukiukwaji wa taratibu mbalimbali za ujenzi.

Ukiukwaji huo ulibainika baada ya kamati ya usalama kufika katika shule hiyo kukagua ujenzi unaoendelea wa madarasa na vyoo hivyo na kubaini mapungufu mengi na hivyo, Mpogolo kuagiza kufanyika kwa uchunguzi na ikibainika hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika wote wa usimamizi wa mradi huo na katika kipindi hicho cha uchunguzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo amtafute mwalimu atakaekaimu nafasi ya mwalimu mkuu.

Hata hivyo, Kamati ya Usalama ilimshukuru Rais Magufuli kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya 4.5 bilioni za maendeleo kwa muda mfupi. Pia imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justice Kijazi, kwa kuendelea kusimamia vizuri fedha ya serikali katika miradi inayoletwa katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari na msingi, mabweni, mabwalo, ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyoo, maabara na ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Veta

No comments: