ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 25, 2020

Kimenuka Chadema! Mdee, Wenzake Waitwa Kujieleza

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakiwatambui wabunge wanawake 19 wa viti maalumu wa chama hicho wakiwemo Halima Mdee, Esther Matiko, Esther Bulaya na wengine walioapishwa jana Novemba 24, 2020 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, jijini Dodoma kwa madai kuwa wameapishwa bila ridhaa ya chama hicho.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Novemba 25, 2020 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam huku akitoa wito wa kuwataka wabunge hao kufika katika ofisi hizo keshokutwa Ijumaa, Novemba 27, ili kuhojiwa na Kamati Kuu ya Chama kutokana na kitendo walichokifanya.

“Tumewaita kuwaeleza kwamba Chadema hakijateua wabunge wa viti maalum wala hakijawasilisha orodha yoyote Tume Uchaguzi ya uteuzi wa wabunge wa viti maalum. Kwa katiba ya Chadema mamlaka ya uteuzi wa wabunge yako kwa kamati kuu ya chama, na kamati kuu ya chama haijawahi kufanya kikao cha uteuzi wa majina ya wabunge wa viti maalum na mimi Katibu Mkuu sijawahi kuwasilisha orodha yoyote Tume ya Uchaguzi.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilituandikia barua Novemba 10, 2020 kutueleza haijapokea majina ya wabunge wa viti maalum na kutuomba kuyawasilisha ikiwemo fomu namba 8D inayopaswa kuwa na idhini ya katibu mkuu wa chama na mimi sijajaza yoyote. Niliiandika baada ya Mkurugenzi wa NEC kunukuliwa na vyombo vya habari kwamba Chadema imewasilisha orodha ya wabunge wa viti maalum na yeye amekwishaipeleka bungeni.

“Mimi kama Katibu Mkuu hakuna fomu yoyote niliyowahi kuijaza popote kuthibitisha uteuzi wa yeyote, hii fomu pia ina sehemu ya kiapo cha hakimu, kwa tafsiri nyepesi kilichofanyika ni biashara haramu ya kughushi na wameenda kuapishwa bila baraka ya chama.

“Tumeitisha kikao cha kamati kuu Ijumaa, Novemba 27, 2020, Dar es Salaam, na tutawaandikia wahusika ili kisitokee kisingizio hakupata taarifa, natangaza wito kwa wanachama wetu 19 walioshiriki kuapishwa kufika makao makuu Kinondoni Ijumaa saa 2:00 asubuhi,” alisema Mnyika.

Aidha, amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ataongoza kikao cha kuwahoji wanachama walioapishwa kuwa wabunge wa viti maalum akiongeza kwamba si mara ya kwanza wao kufanya vikao vya kinidhamu na walioapishwa wameshiriki kukihujumu chama.

“Kauli iliyotolewa jana na kumhusisha Freeman Mbowe haina ukweli. Mbowe ataongoza kamati kuu na itawasikiliza wahusika. Kati ya walioapishwa kuna wajumbe wa kamati kuu wanafahamu uteuzi haukufanyika na wanajua wameshiriki biashara haramu.

“Chama hiki kitaendelea na kitapita salama. Kitaendelea kujipanga kwenda kushika dola. Chadema kimekuwa kikiwaita viongozi wakubwa, kuhojiwa na kuchukuliwa hatua na bado kikavuka salama,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Natangaza wito (public notice), kupitia vyombo vya habari kwa wanachama wetu 19 walioshiriki kwenda kula kiapo jana, kufika makao makuu ya chama bila kukosa siku ya Ijumaaa ya Novemba 27, 2020, saa 2:00 asubuhi, kutoka popote pale walipo.”

No comments: