ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 22, 2020

MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA AONGOZA MASHINDANO YA NBC MARATHON JIJINI DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza mashindano ya NBC Marathon Mwaka 2020 leo Novemba 22,2020 Jijini Dodoma yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama. Mashinda
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa kwenye maadhimisho ya mashindano ya NBC Marathon Mwaka 2020 yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama yaliyofanyika leo Novemba 22,2020 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimvisha Medali mshindi wa kwanza wa mashindano ya NBC Marathon Mwaka 2020 kilomita 42 Philipo Kipingu kutoka Uganda baada ya kushinda mashindano hayo yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama. Mashindano hayo yamefanyika leo Novemba 22,2020 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi fedha taslim mshindi wa kwanza wa mashindano ya NBC Marathon Mwaka 2020 kilomita 42 Wanawake Muruki Muruki kutoka Kenya baada ya kushinda mashindano hayo yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama. Mashindano hayo yamefanyika leo Novemba 22,2020 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi mfano wa Hudi ya Shilingi milioni mia moja 100,000,000. Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaitenanga iliyotolewa na Banki ya NBC kwa ajili ya kuchangia mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama kwenye Maadhimisho ya Mashindano NBC Marathon mwaka 2020 yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano zidi ya Saratani ya mlango wa Kizazi kwa akina mama yaliyofanyika leo Novemba 22,2020 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KATIKA MBIO ZA NBC MARATHON UWANJA WA JAMHURI JIJINI DODOMA


Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mbunge), Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Philip Isodory Mpango (Mbunge), Waziri wa Fedha na Mipango;

Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

Mheshimiwa Anthony Mtaka, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu;

Bwana Theobald Sabi, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NBC;
Waheshimiwa Wabunge;

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma;
Viongozi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi;

Wananchi wa Jiji la Dodoma;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;

Habari za Asubuhi.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutukutanisha hapa tukiwa wazima wa afya na kushiriki kikamilifu katika mbio hizi za NBC Marathon. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Uongozi NBC kwa kushirikiana na Shirikisho la Riadha Tanzania kwa kubuni wazo hili la Marathon ambapo ndege wawili watauliwa kwa jiwe moja.

Nimesema hivi nikimaanisha ushirikiano huu baina ya NBC na RT katika kuandaa marathon hii utasaidia kuwaandaa wanariadha wetu kwa mbio zijazo za Olympics lakini vilevile fedha jumla ya TZS 75 milioni zitakazokusanywa zitaelekezwa katika vita dhidhi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).

Napenda kupongeza wazo la kuandaa mashindano haya Jijini Dodoma. Hii ni hatua muafaka iliyokuja katika kipindi sahihi hasa ukizingatia ya kwamba Serikali ilishahamia rasmi katika Jiji letu la Dodoma. Aidha, Marathon hii pia itakuwa chachu ya kuufungua Mji wa Dodoma kwa fursa ya utalii.

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa,

Waswahili husema shughuli ni watu; na hakika umati huu ninaoushuhudia ni ushahidi tosha wa maandalizi mazuri yaliyofanyika na muitikio mkubwa wa wananchi na wakazi wa Jiji la Dodoma. Natambua kwamba kuandaa tukio kama hili linahitaji ubunifu mkubwa, moyo wa kujitolea, ushirikiano na nia njema kwa jamii inayotuzunguka. Yote hayo nimeyaona hapa uwanjani.

Hongereni sana NBC na RT bila ya kuwasahau wafadhili wote mliochangia kwa namna moja ama nyingine nawapongeza sana. Mniruhusu niwataje kwa uchache wao:
Sanlam Insurance
G4S Security
Coral Paints
Pepsi
Sequa Pure Drinking Water
SGA Security
Huduma ya Mabasi ya Kimbinyiko
Clouds Media Group
EATV/Radio
Mwananchi Communications Limited

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa,

Benki ya NBC ndiyo benki kongwe hapa nchini yenye miaka zaidi ya 50. Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limezaliwa mwaka 1954, wakati huo ikiitwa Tanzania Athletics Association (TAA), hivyo mashirikiano yanayooneshwa kati ya taasisi hizi mbili kongwe ni jambo la faraja. Ni matumaini yangu kwamba, ushirikiano huu utazaa mambo makubwa zaidi kwenye sekta yetu ya Riadha.

Nimepewa taarifa kuwa makubaliano haya ya ushirikiano ni kwa kipindi cha miaka mitano ambapo NBC itawekeza jumla ya milioni 300 kwa RT ili kukuza mchezo wa riadha nchini hasa katika mchezo wa mbio ndefu. Aidha, kutokana na mapato hayo RT itaweza kuwahudumia na kuwaandaa wanariadha waliofuzu kushiriki katika mashindano makubwa ya riadha kama vile Olimpiki, Jumuiya ya Madola, Mashindano ya Dunia na Mashindano ya Afrika. Ushirikiano huu baina ya NBC na RT unaenda sambamba na azma ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kukuza Sekta ya Sanaa, Michezo na Utamaduni ambayo inakua kwa kasi kubwa hivi sasa hapa nchini, kama alivyoainisha katika Hotuba yake ya kufungua Bunge la 12.

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa,

Kama nilivyosema hapo awali kuwa mbio hizi zimefana sana; hivyo basi, nichukue fursa hii kuwapongeza washiriki wote hususan washiriki wetu waliotoka nchi jirani. Nimepewa taarifa washiriki wote waliojiandikisha ni elfu tatu (3,000) na waliotoka nchi za jirani ni 35 kwa mtiririko ufuatao:

Kenya – 19;
Uganda – 12 na
Malawi – 4
Naamini kuwa wanariadha hawa wa nje wamevutika kushiriki Marathon hii kwa sababu ina utambuzi wa Kimataifa kama alivyosema Mkurugenzi Mtendaji. Viwango hivi vya Kimataifa vya mbio hizi ni jukwaa zuri la wanariadha wetu kujifua kwa ajili ya mashindano ya Olympics na Jumuiya ya Madola. Na uwepo wa wanariadha kutoka nje unasaidia kujipima na kujitathmini tunakosea wapi pamoja na kupata uzoefu kwa wenzetu ambao mara kwa mara wamekuwa wakiibuka kidedea kwenye mbio ndefu (nchi jirani ya Kenya ambao leo wapo hapa kwa wingi).

Ni matarajio yetu kwamba wanariadha hawa wa nje wameongeza ushindani na hivyo kuongeza ubora wa mbio hizi lakini pia kukutana kwenu leo iwe ni mwanzo wa kujuana na kujenga udugu na mshikamano.

Niweke mkazo kwenye hili kwa kukopa maneno ya mchezaji wa zamani wa Marekani aliyeshinda medali nne za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto huko Berlin-Ujerumani mwaka 1936 ambaye alisema hivi nanukuu:-

“Friendships born on the field of athletic strife are the real gold of competitions. Awards become corroded, but friends gather no dust”. Akiwa na maana kuwa urafiki unaojengwa kwenye medani za michezo ndiyo dhahabu ya mashindano kwa kuwa medali huota kutu lakini urafiki wa aina hii hudumu.

Ndugu Washiriki,

Kama nilivyosema hapo awali Marathon hii pia kupitia fedha zitakazokusanywa itasaidia kuchangia vita dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi. Suala la kurudisha fadhila kwa jamii inayotuzunguka kwa namna hii, ni kuonesha utu na ubinadamu wa hali ya juu.

Nimepewa taarifa kuwa Shilingi milioni 75 zitaelekezwa kwenye mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi. Fedha hizi ni zao la uzalendo wenu kwa kujitoa na kujumuisha nguvu zenu kwa pamoja. Umoja na ushirikiano huu ni kielelezo halisi cha uzalendo wenu. Hongereni sana!

Ndugu Washiriki,

Kama mnavyofahamu, saratani ni ugonjwa unaoathiri watu wa rika na jinsia zote. Takwimu mpya za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Agency for Research on Cancer-IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka nchini Tanzania kunakadiriwa kutokea wagonjwa wapya wa saratani wanaokadiriwa kufikia 9,772 hii ikiwa ni sawa na wastani wa wagonjwa 59.1 katika kila watu 100,000 na kati ya hao zaidi ya wagonjwa 6,695 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka.

Nchini Tanzania, tatizo la saratani limekuwa likiongezeka na kukua siku hadi siku. Takwimu za hospitali za Tanzania za mwaka 2019, zinaonesha kwamba wagonjwa wapya wa saratani 13,215 walihudumiwa, ambao ni sawa na asilimia 31 ya wagonjwa wote wapya kwa mwaka 2019. Takwimu hizi zinaonesha ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ndiyo unaongoza, na kwa kina mama unachukua zaidi ya asilimia 47 ya wagonjwa wote waliohudumiwa. Ni wazi kuwa tatizo hili ni kubwa na iwapo hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani litaongezeka na kuwa kubwa zaidi.

Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 75 ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi hufika katika Hospitali wakiwa katika hatua za juu za Ugonjwa wa saratani (hatua ya 3 na ya 4) hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kupona maradhi yao.

Tanzania imeongeza juhudi za kuhakikisha kuwa huduma za saratani zinaimarishwa na zinapatikana karibu na wananchi. Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wote kwa kupambana na tatizo la saratani. Tayari kuna mpango wa Kitaifa wa kutoa chanjo ya kukinga virusi vinavyosababisha saratani mbalimbali ikiwepo saratani ya mlango wa kizazi inayosababishwa na virusi vya HPV tangu mwezi April 2018 nilipoizindua chanjo hii. Chanjo hii inatolewa kwa wasichana walio shuleni kuanzia miaka 14 na walio darasa la 4. Ninafarijika kuona kuwa mpaka sasa chanjo hii imewafikia zaidi ya asilimia 81.5 ya walengwa na hivyo itasaidia sana kupunguza au kutokomeza kabisa saratani ya mlango wa kizazi hapa nchini.

Nitoe rai kwa akina mama wenzangu kuwa na ratiba ya kufanya uchunguzi mara kwa mara ili ugongwa uweze kugundulika katika hatua za mwanzo na hivyo kutibika kwa urahisi.

Ndugu Wananchi,

Serikali imeendelea kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchi nzima. Hii imethibitika kwa kuhakikisha kuwa huduma za uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi yanapatikana na kuwafikia wananchi wote wa mijini na vijijini. Hadi kufikia Juni 2020 takribani vituo vya Afya 649 vinatoa huduma za uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa kizazi. Jumla ya wanawake 406,785 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wanawake 127,188 kwa mwaka 2015. Lengo ni kuongeza idadi ya wanawake wanaofanyiwa uchunguzi mara mbili zaidi na kufikia 1,000,000 ifikapo 2025.

Ndugu Washiriki,

Niwahakikishie watanzania wote kuwa tutaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za upimaji na matibabu ya saratani. Huduma za matibabu ya saratani kwa sasa zinapatikana kwenye hospitali zote za kanda Mwanza-Bugando, Mbeya, Dodoma – Benjamin Mkapa, Kilimanjaro – KCMC, na Dar-es-salaam. Aidha, kwa upande wa upatikanaji wa dawa za kutibu saratani umeongezeka pia kutoka asilimia 4 mwaka 2015 hadi asilimia 95% mwaka 2019, na hatua ya kuweka machine za kisasa za matibabu ya saratani za LINAC katika Taasisi ya Ocean Road imerahisisha upimaji kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na hayo, Serikali inaendelea na Mradi wa kimkakati wa kufunga mashine ya kisasa ya vipimo ya PET CT scan katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road iliyogharimu Shilingi bilioni 14.5. Fedha hizi zimetolewa na Serikali ikiwa na lengo la kuhakisha wagonjwa wote wa saratani wanapata huduma bora hapa nchini na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa kupeleka wagonjwa nje kama ilivyokuwa awali.

Mbali na jitahada nilizozitaja, nitumie fursa hii kupongeza mabenki yetu kwa kushirikiana na Shirikisho la Riadha Tanzania kuandaa mbio za aina hii zinazosaidia kukusanya fedha zinazopelekwa kwenye Taasisi mbali mbali za Afya zinazoshughulika na maradhi mbali mbali kwa madhumuni ya kuimarisha na kusogeza huduma za Afya kwa wananchi. Mwezi Agosti mwaka huu nilifanya shughuli kama hii iliyoandaliwa na benki ya CRDB.

Ndugu Washiriki,

Napenda kuwashukuru wadau wote mnaounga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inaboresha maisha na Afya ya Watanzania. Ni wazi kuwa mchango wenu utaisaidia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kuendelea kujengea uwezo hospitali na vituo vya Afya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi nchini. Nawapongeza kwa dhati uongozi wa NBC kwa kuweka azma ya kuendelea kuchangia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Nimetaarifiwa kuwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki NBC itachangia eneo jingine lakini itakuwa katika sekta ya afya. Niwaombe muangalie eneo lenye uhitaji zaidi na unaogusa moja kwa moja watanzania maskini. Shirikianeni na Wizara ya Afya ili kutambua uhitaji upo wapi.

Nimalizie kwa kutoa rai kwa Taasisi, Mashirika na Makampuni kuiga mfano huu wa NBC kwa kuhakikisha wanarudisha fadhila kwa jamii kwenye maeneo yenye uhitaji. Ni ndoto yangu kuona kuwa mashirikiano haya baina ya NBC na RT yanazaa matunda kwenye mbio za Olympics, Jumuiya ya Madola na mbio nyingine za Kimataifa. Muda umefika sasa kama nchi tukazalisha kina Filbert Bayi wengi zaidi. Leo nimeshuhudia wanariadha wazuri sana ila huwa najiuliza swali tukifika kwenye medani za kimataifa tunakwama wapi? Niwatakie wanariadha wetu kila la kheri na maandalizi mema kuelekea mashindano yajayo ya olympics. Niwaombe waende kufuta machozi ya Watanzania ya muda mrefu, na kurudi na medali za kutosha nyumbani.

Kwa mara nyingine tena nawashukuru wote kwa kushiriki marathon hii. Shukrani zangu ni kwa wale wote ambao kwa njia moja au nyengine walihusika katika kupanga na kuandaa shughuli hii, na shukrani za dhati kwa waliojitolea kuchanga ili kufanikisha yaliyokusudiwa. Sasa nipo tayari kugawa medali kwa washindi wetu, na kwa washiriki wengine nawapongeza sana kwa uthubutu wenu nanyi pia ni washindi.

Dodoma Oyee!
NBC Oyee!
Riadha Oyee!
Afya yangu ndio mtaji wangu!

Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments: