ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 30, 2020

WADAU WASHAURI MBINU ZA KUINUA SEKTA YA KILIMO NCHINI

NA MWANDISHI WETU

WADAU nchini wameshauri kurahisishwa kwa upatikanajii wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa kulingana na eneo husika na kuongezwa kwa fungu la mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima wadogo, kwamba kufanya hivyo kutaongeza thamani katika sekta ya kilimo nchini.

Wamesema pamoja na mambo mengine pia ni muhimu kuwawezesha wakulima wadogo vitendea kazi ili kurahisisha shughuli zao, kadhalika wahusishwe katika safari za mafunzo na kujengewa uwezo mara kwa mara ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na masoko.

Ushauri huo ulitolewa jana na afisa miradi wa mtandao wa kitaifa wa asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabianchi (FORUMCC) Sarah Ngoy, alipozungumza na Uhuru kuhusu utekelezaji wa mradi wao kwa kushirikiana na PACJA (Pan African Climate Justice Alliance) .

Alisema kilimo ni miongoni mwa sekta zinazokumbwa na athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuwepo kwa mvua nyingi ama chache, hali ya ukame au mafuriko, mvua zisizotabirika, kuzuka kwa magonjwa ya mazao na wadudu waharibifu.

Sarah, alisema ili kukabiliana na changamoto zote zinazoikumba sekta ya kilimo na kufikiwa kwa adhma ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, ni muhimu jukumu hilo lisiachwe kwa serikali pekee.

Alisisitiza ni muhimu kuwepo kwa jitihada za pamoja katika ngazi zote na ushirikishwaji mpana wa wadau wengine ikiwemo sekta binafsi, mashirika ya umma na asasi za kiraia.

Kwa mujibu wa Sarah, uzalishaji duni usio na tija, vikwazo na mienendo ya masoko ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha mipango ya kupunguza umasikini na kuboresha lishe nchini kwani yanaathiri maamuzi ya wakulima katika uchaguzi wa aina ya mazao, kiwango cha uzalishaji na lishe.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo na kufikia Malengo Endelevu ni muhimu kuboresha tija na kipato cha wakulima wadogo kwa kukuza upatikanaji sawa wa ardhi, teknolojia na kuboresha huduma za ugani.

“Nashauri kuongezwa kwa bajeti itakayochochea tafiti na matumizi ya teknolojia sahihi ili kusaidia uwepo wa pembejeo za kutosha na bora, kadhalika kutengenezwa kwa mfumo wa upelekaji taarifa muhimu na fursa kwa wakulima wadogo”.

Aliongeza, “Ni jukumu la wakulima kuanzisha ama kuimarisha shughuli mbadala za kujiingizia kipato nje na kilimo ikiwa ni njia ya kuongeza uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Afisa miradi huyo, alisisitiza kuboreshwa kwa tafiti kulingana na mabadiliko yanayojitokeza, pia wakulima wapatiwe mrejesho wa tafiti hizo, huku sekta binafsi ikipaswa kuongeza ushiriki katika kuzalisha mbegu bora ili kusaidia wakulima kuzipata kwa gharama nafuu zaidi na kwa wakati.

“Kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuimarisha mnyororo wa thamani ni moja ya vitu vikubwa vinavyoweza kuchangia maendeleo endelevu kwa wakulima wadogo,” alisema.

Moses Mfinanga, ni Mkulima Mdogo katika Kijiji cha Makanya Wilayani Same, alisema hitaji lao ni kutengenezewa mazingira rafiki ya upatikanaji na umiliki wa teknolojia za kuhifadhia mazao kwa muda mrefu na zana za kuandalia mashamba.

Alitaja mengine kuwa ni vifungashio vyenye ujazo rafiki na vinavyoweza kukidhi mahitaji ya mkulima mdogo, ujuzi wa kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, kutengenezwa kwa mfumo mzuri wa masoko ili waweze kuuza mazao kwa wakati na kupata faida kulingana na gharama za uzalishaji.

Miongoni mwa malengo ya maendeleo endelevu ya agenda 2030 (SDGs) ni kutokomeza umasikini wa aina zote kila mahali, kutokomeza njaa, kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora na kukuza kilimo endelevu, kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari zake.

Malengo haya yana kanuni za uendelevu wa kiuchumi, kijamii na mazingira; zinazoleta tija katika kushughulikia sababu kuu za umaskini na njaa kutokuacha mtu yeyote nyuma, kuhamisha ulimwengu kuingia katika uendelevu na uhimilivu, wenye utulivu na mabadiliko katika viwango vya maisha.

Malengo haya yanalenga mpaka ifikapo 2030 kuisaidia jamii kumiliki na kutumia teknolojia bora, kuitengenezea jamii mazingira wezeshi ya kupata kwa urahisi huduma za kifedha, kuhakikisha zana na pembejeo za kilimo zinapatika kwa urahisi, kwa wakati na gharama nafuu zaidi, kuboresha uvunaji na uhifadhi wa mazao, upatikanaji wa masoko yenye uhakika, kuendelea kuijengea jamii uwezo ili kuwaimarisha na kuboresha hali yao ya uchumi, kuwaondoa katika mazingira yaliyo duni na hatarishi, kukuza mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula inayoongeza tija na uzalishaji, inayodumisha mifumo ya ikolojia, kuboresha ardhi na udongo, kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake zitokanazo na ukame, mafuriko.

Licha ya kuwepo kwa malengo haya, wakulima wadogo ambao hutegemea kilimo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya kila siku, na ambao ndio wenye mchango mkubwa katika pato la taifa; bado ni miongoni mwa kundi linaloathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi ambazo kwa kiasi kikubwa husababisha uzalishaji duni na mara nyingine kukosekana kabisa kwa mavuno.

Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa hakiko sambamba na kiwango cha kupunguza umaskini na changamoto za lishe na usalama wa chakula nchini Tanzania. Katika sekta ya kilimo wakulima wakubwa ndio wanaonufaika zaidi ukilinganisha na wakulima wadogo.

No comments: