Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufanya jitihada za kuboresha huduma za kifedha kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar ili kuondoa changamoto kwa wananchi na kuifanya Zanzibar kuwa na huduma nzuri za kifedha nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya watu wa Zanzibar Malindi Mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema kumekuwa na changamoto nyingi kwa wateja wanaotumia benki hiyo ikiwemo msongamano hivyo jengo hilo litasaidia katika kuboresha huduma za kibenki na kuwaondolea usumbufu wananchi wa Zanzibar.Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Maalim Seif Sharif Hamad akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Benki ya Watu wa Zanziba (PBZ) liliopo Malindi Mjini Zanzibar. Uzinduzi wa jengo hilo ni miongoni mwa maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuwa hatua hiyo ni kubwa kimaendeleo katika mji wa Zanzibar hasa mji Mkongwe ambayo pia itawasaidia wafanyakazi wa benki hiyo kuweza kufanya kazi katika mazingira mazuri kwa kutoa huduma bora na kwa ufanisi kwa wateja wakiwemo vijana wazee na wafanyabiashara hatimae kuifanya benki hiyo kuwa ya kupigiwa mfano Afrika Mashariki na kuweza kuingia katika ushindani na taasisi nyengine za kifedha duniani.
Alieleza kuwa ufunguaji wa matawi mbalimbali ya Benki ya watu wa Zanzibar katika maeneo tofauti ya Tanzania utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wajasiriamali wakiwemo wavuvi,wakulima na wafanya biashara wadogo na kuwawezesha kupata mikopo ili kujiendeleza kiuchumi na kuondoa kilio chao cha kutaka kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu.
“Serikali yetu inatambua juhudi ambazo Benki ya watu wa Zanzibar inazifanya katika kuwafikia wananchi na kutoa huduma bora ili kukidhi matakwa ya wananchi kwa kuendelea kufungua matawi mengine na vituo mbalimbali vya kutoa huduma” Alisema Makamo wa kwanza.
Aidha alisema Benki ya watu wa Zanzibar ilioanzishwa miaka 55 iliyopita ni miongoni mwa taasisi kongwe za kifedha Tanzania zilizoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma za kuwakomboa wananchi katika sekta zote za kiuchumi,hivyo katika kutimiza miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar Serikali inapenda kuiona Benki ya watu wa Zanzibar inatimiza malengo yake
Sambamba na hayo Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar amewashauri watendaji wa benki hiyo kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia ili kuboresha utendaji wa benki, kutafuta wafanyakazi waaminifu,kujitathmini kiutendaji mara kwa mara na kuisaidia Serikali katika nyanja zote za maendeleo ikiwemo afya,elimu na biashara.
Nae waziri wa Nchi Ofsi ya Raisi Fedha na Mipango Mh Jamal Kassim Ali amesema benki ya watu wa Zanzibar inaongoza katika kuchangia mapato ya serikali ambapo mwaka uliopita imelipa kodi ya serikali shilingi Bilioni 8.35 ambazo zimesaidia Serikali katika kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha waziri huyo amesema benki hiyo imeweza kukuza mtaji wake na imetengeneza faida ya shilingi bilioni 32 katika mwaka uliopita kutokana na mikakati madhubuti ya benki hiyo pamoja na ushirikiano mzuri wa serikali na taasisi mbalimbali nchini.
Jumla ya shilingi bilioni 4.6 zimetumika katika ujenzi wa jengo hilo la kibiashara lililopo Malindi Mjini Unguja ambalo limejengwa ili kupunguza gharama za kukodi majengo kwa ajili ya shughuli za benki pamoja na kukua kwa uendeshaji wa Benki hiyo nchini.
No comments:
Post a Comment