ANGALIA LIVE NEWS
Sunday, January 3, 2021
Wafanyabiashara marufuku kuchanja mifugo, mikataba yao kuvunjwa
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga, MTANZANIA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutotumia wafanyabiashara kuchanja mifugo na kutaka kuvunjwa kwa mikataba hiyo mara moja.
Waziri Ndaki amebainisha hayo juzi Desemba 31 alipofanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga.
Akiwa katika josho la kuogeshea mifugo la Kijiji cha Mipa kilichopo Wilaya ya Kishapu mkoani humo kushuhudia uogeshaji mifugo na utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, wafugaji wamemlalamikia kuwa baadhi ya ng’ombe wamekuwa wakivimba na wengine kufa baada ya kupatiwa chanjo.
Waziri Ndaki ambaye ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amesema kuanzia sasa chanjo zote nchini zitatolewa na wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa.
Waziri huyo amegoma kushuhudia zoezi la uchanjaji lililokuwa limeandaliwa baada ya kukasirishwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kutokuwa na takwimu yoyote ya idadi ya ng’ombe waliovimba na wengine kufa baada ya kuchanjwa.
“Halmashauri zote kuanzia sasa ni marufuku kutumia wafanyabiashara kuchanja mifugo yetu, zitumie wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa waweze kuchanja mifugo ya wananchi wetu, hao wafanyabiashara kama mmeingia mikataba nao ivunjeni haraka hatuwezi kuchezea akili za watu namna hii hatuwezi kutuma wafanyabiashara waende kuchanja ng’ombe wanavimba na wanakufa halafu taarifa hatuna,” amesema Ndaki.
Aidha, Waziri Ndaki amefika katika mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya minada inayosimamiwa na wizara na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kumuondoa mara moja mhasibu wa halmashauri hiyo anayefanya kazi katika mnada huo kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka hali inayosababisha wizara na halmashauri kukosa mapato stahiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amesema amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa kuihusisha pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili ifanye ufuatiliaji kwa kuwa serikali haiko tayari kuwa na watu wenye tabia ya namna hiyo.
Waziri huyo pia amepata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wafugaji ikiwemo ya kuzuiwa kuondoa mifugo mnadani kabla ya saa 12 jioni hali inayohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa fisi wengi kwenye maeneo ya mashamba wakati wa kurudi nyumbani majira ya jioni hali na kuutaka uongozi wa mnada utafute utaratibu wa kuwaruhusu wafanyabiashara kuondoka kabla ya muda huo wakiwa wamemaliza shughuli zao.
“Mtu amemaliza biashara yake mkagueni vizuri kwenye mlango wa kutokea aende zake akimaliza hapa akikaa saa mbili aondoke, akikaa dakika 15 aondoke ili mradi amemaliza shughuli zake siyo unawaleta unawafungia humu haka kamekuwa kajela kadogo? Hapana hiyo,” amesema.
Akiwa Mkoani Shinyanga waziri huyo na naibu wake, Gekul wametembelea ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika Manispaa ya Shinyanga unaogharimu Sh bilioni 5.5 ambapo tayari zimelipwa Sh bilioni 5.1 na umefikia asilimia 97.
Machinjio hayo yanayotarajiwa kukamilika Februari mwaka huu yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment