Wednesday, August 11, 2021

MHE.OTHUMAN MASOUD AWATAKA WANACHAMA WA ACT KUHAKIKISHA WANAKILINDA CHAMA HICHO

Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wanachama wa ACT kuendelea kuungana katika kuhakikisha chama hicho kinaendelea na hatua za kufikia dhamira yake.

Ameyasema hayo leo (Agosti 10) ikiwa ni siku ya pili na ya mwisho ya ya ziara yake ya kichama iliyofanyika katika mikoa minne ya kichama kisiwani Pemba ambayo iliwashirikisha viongozi wakuu wa chama, Viongozi Wa Majimbo na Matawi ya Chama cha ACT Wazalendo, yenye lengo la kuwafikishia maazimio ya kikao cha Kamati Kuu Kilichofanyika (Agost 8) Mjini Unguja.

Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu Wa Kwanza Wa Rais Wa Zanzibar, amesema nidhamu kubwa iliyooneshwa na wanachama hao katika kusimamia amani na haki katika chama hasa wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo uliofanyika katika jimbo la Konde ndio nyenzo kubwa itakayo kisaidia chama kupiga hatua pamoja na kufikia adhma ya kuibadilisha Zanzibar Katika upande wa siasa na uchumi.

Aidha, Mhe. Othman aliwasisitiza wanachama hao kuendeleza imani yao kwa chama jambo litakalochochea mabadiliko makubwa kwa chama pamoja na kuongeza kasi katika kufikia dhamira ya chama hicho.

Mhe. Othman alitumia fursa hio kuwahimiza viongozi wa chama hicho kwamba waendelee kusimamia malengo ya kuibadilisha Zanzibar na kuhakikisha kila Mwananchi anapata haki yake kwa lengo la kuona wananchi wa Zanzibar Wanafikia maendeleo endelevu.

Mapema kiongozi wa chama hicho Ndugu Zitto Zubeir Kabwe, akawahikikishia wanachama hao kuwa chama hicho kitaendelea kusimamia makubaliano yaliyopo kati yao na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati walipojiunga na Serikali umoja wa kitaifa ili kuona haki inatendeka nchini.

Katika makubaliano hayo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo yaliasisiwa na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barara la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi. Ndugu, Zitto Kabwe amesisitiza kuwa wataendelea kusimamia uundwaji wa tume ya maridhiano, mabadiliko ya sheria ya uchaguzi pamoja na kubadilishwa kwa tume ya uchaguzi kwa lengo la kubadilisha hali ya kisiasa nchini ili kuona haki inapatikana wakati zinapofanyika uchaguzi nchini.

“Tunataka tuweke mazingira mazuri ya kinchi na mshikamano ili hata baada ya uchaguzi Wazanzibari wabaki kuwa wamoja” alieleza Zitto.

Akigusia uchaguzi mdogo wa Konde unaotarajiwa kurudiwa kutokana na kujiuzulu kwa Mbunge mteule Ndg. Sheha Mpemba Faki katika uchaguzi uliofanyika mapema mwezi wa saba jimboni humo, Ndg. Zitto amesema chama hicho kimeazimia kuingia katika uchaguzi wa marudio wa jimbo hilo huku wakiitaka Serikali kuwawajibisha watendaji waliohusika katika uchaguzi uliopita kwa lengo la kuona haki na usawa inatendeka katika uchaguzi unatarajiwa kufanyika.

Kwa nyakati tofauti naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Zanzibar, Ndg. Juma Duni Haji, amesema Chama cha ACT Wazalendo kimekuwa ni chama cha waungwana na chenye kudai haki hasa kwa njia za amani na hii ni kutokana na dhamira yao ya kuifanya Zanzibar kuifikia mamlaka kamili.

Akimalizia ziara hio mkoa wa Wete kichama, takriban Wanachama 45 wamekabidhiwa kadi za za kujiunga na chama hicho.



Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake