Thursday, August 12, 2021

SERIKALI IMEDHAMIRIA KUFUFUA VYUO VYA UFUNDI STADI NA MAREKEBISHO KWA WATU WENYE ULEMAVU

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (katikati) akikagua bwalo la chakula cha wanafunzi wakati alipozindua Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Luanzari, Mkoani Tabora. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Prof. Jamal Katundu. Wa pili kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu na Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Halima Luguya.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (katikati) akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tabora wakimsikiliza Juma Masiroli (mwenye ulemavu) mnufaika wa mafunzo ya Ufundi stadi yanayotolewa katika Chuo hicho.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi taulo za kike kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Halima Luguya.na wanafunzi wa kike mara baada ya kuzindua Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Luanzari, Mkoani Tabora.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akieleza jambo kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Paul Chacha.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi Sabuni kwa vijana wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Luanzari, Mkoani Tabora. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Paul Chacha.
Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Halima Luguya akitoa taarifa fupi ya Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Luanzari wakati wa hfla hiyo ya uzinduzi wa chuo hicho Mkoani Tabora. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu.
Sehemu ya vijana wanufaika wa mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Luanzari wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.

PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)


Na; Mwandishi Wetu – Tabora

Imeelezwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kufufua Vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu ili kuendelea kutoa mafunzo kwa kundi hilo maalum na kuhakikisha wanawezeshwa kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri, kuajiri wenzao, kujiingizia kipato na kuchangia kwenye uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akifungua Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu Luanzari Mkoani Tabora kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama kufuatia maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kutaka Vyuo vyote vya wenye Ulemavu kufunguliwa ifikapo mwaka 2025.

Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha vyuo hivyo vinaendelea kutoa mafunzo ilikuwa ni kuwapa nafasi na kuwajengea uwezo wa kujiendeleza vijana wenye ulemavu katika mazingira mazuri ya kujifunza ili waweze kujiajiri hatimaye kuondokana na maisha tegemezi na kusaidia jamii kupata fani mbalimbali za ufundi stadi ikiwemo Ushonaji, Useremala. Kilimo, Umeme wa majumbani n.k

“Ofisi ya Waziri Mkuu hivi karibuni ilifanya tathmini ili kujua hali halisi ya vyuo maalum vya ufundi stadi na huduma za utengamao hapa nchini kwa lengo la kubaini changamoto zilizopo na kuchukua hatua muhimu katika kuviwezesha vyuo hivyo kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa,” alieleza Naibu Waziri Ummy

“Hatua hiyo ilipelekea kuwepo kwa haja kubwa ya kuendelea kuboresha miundombinu iliyopo kwenye vyuo hivyo vya ufundi stadi kwa kuifanyia ukarabati, kujenga mingine mipya kufikia lengo tarajiwa. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2021/2022 imetenga bajeti kwa ajili kuanza kutekeleza hayo, hivyo nitumie fursa hii, kuwaomba na kuwaalika wadau mbalimbali kushiriki kwa kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha zoezi hilo,” alisema Naibu Waziri Ummy.

Alieleza kuwa Chuo hicho cha Luanzari kina uwezo wa kupokea wanafunzi 48 wa bweni na wanafunzi wa kutwa 72 hivyo kina uwezo wa kudahili wanafunzi 120 kwa mwaka huku akibainisha kuwa malengo ya ofisi hiyo ni kukiwezesha kupokea wanafunzi wengi zaidi.

Pia aliwahimiza Halmashauri kuendelea kusimamia kikamilifu suala la uwezeshwaji wa mikopo kwa Watu wenye Ulemavu kupitia asilimia mbili ya mapato ya makusanyo ya ndani Halmashauri na kusisitiza kutofanyika urasimu wakati wa utoaji wa mikopo hiyo.

Katika hatua nyingine alihimiza uwepo wa takwimu sahihi za watu wenye Ulemavu kwa lengo la kuiwezesha serikali na wadau mbalimbali kutambua mahitaji yao akiwataka maafisa ustawi wa jamii kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa kuwa na programu ya kutembelea makundi maalumu Katika maeneo yao ili waweze kutambua aina ya Ulemavu walionao na namna ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi. Aidha alisisitiza pia juu ya suala la kujadili masuala ya watu wenye ulemavu katika vikao vya maamuzi.

“Elimu kwa kundi hili ibainishwe kulingana na aina ya Ulemavu alionao mtu au kijana ili kupelekwa Katika shule husika kupata elimu watimize ndoto zao na niwatake wazazi na walezi wasione aibu kuwatoa watoto wao nje wakajulikana hii itakusaidia kupata msaada haraka kuliko kumfungia mtoto ndani inachangia unyanyapaaji na kumuathiri kisaikolojia na kuua malengo yake,” alieleza Naibu Waziri huyo.

“Ofisi ina jumla ya vyuo 6 vinavyotoa huduma hii na vimegawanywa kwa kuzingatia Kanda zilizopo ambazo ni Kanda ya Mashariki mkoa wa Dar-es-Salaam, Kanda ya Kaskazini mkoani Tanga vile vile Kanda ya Kati mkoani Singida,Kanda ya Magharibi mkoani Tabora, Kanda ya Ziwa, Mwanza na Kanda ya Kusini mkoani Mtwara,”alisema.

Awali alisema Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1953 kilifungwa kwa miaka 20 hivyo kufunguliwa kwake ni sehemu ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025 inameelekeza kufufuliwa kwa vyuo vyote vya Watu wenye Ulemavu ambavyo vilikuwa vimesimama kutoa huduma.

Aidha aliwashukuru wadau mbalimbali.walioshiriki kwa uaminifu kuunga mkono serikali kwa hali na mali katika kuboresha na kuendeleza vyuo hivyo maalum vya ufundi stadi na huduma za utengamao hapa nchini.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Paul Chacha alifafanua kwamba mkoa umekuwa ukichukua hatua mbalimbalu kuwawezesha na kuwainua watu wenye ulamvu ndani ya mkoa huo ikiwemo kuwapa mikopo. Alibainisha pia Mkoa huo una watu wenye Ulemavu 8,776.

“Kama mkoa tumewatambua wenye Ulemavu wa viungo 3,275, wasiyosikia 1,436 wenye Ualbino 347, wasiyoona 1,186 na wenye matatizo ya akili 1,832 na Katia hili tumetoa mafuta na lotion 191 kwa waliogundulika kuwa na kansa ya saratani ya ngozi, viti mwendo 65, wenue Ulemavu 182 wamepewa msamaha wa matibabu,” alieleza Chacha.

Akitoa taarifa ya Chuo hicho Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Halima Luguya alieleza kuwa Chuo cha Luanzari kilichoanzishwa mwaka 1953 kilifungwa Mwaka 1997 hivyo kilikuwa akifanyi kazi kwa miaka 20, kufunguliwa kwake ni sehemu ya mikakati ya Serikali katika kurejesha matumaini kwa Watu wenye Ulemavu.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Mkoa wa Tabora, Bw. Amos Masoud alitoa wito kwa wenye Ulemavu kutumia fursa ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa katika vyuo hiyo ili kukuza na boresha vipaji vyao kwa kuwa vitawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwa msaada kwa wengine.

Kwa upande wa Kijana Dotto Lukundi Mnufaika na mafunzo katika chuo hicho ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwakumbuka Watu wenye Ulemavu katika kuwapatia ujuzi kupitia stadi za kazi ambazo zitawajengea uwezo wa kujiajiri, kuajiri wenzao na kujiingizia kipato kitakachowasaidia kujikimu.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake