Mlimbwende (Miss) Karagwe mwaka 2021 Regina Kokurama akiingia uwanjani na kombe la ligi ya Bashungwa Cup mapema kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali ya ligi hiyo uliopigwa Septemba 12 katika uwanja wa Michezo Kayanga Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.
Picha ya pamoja kabla ya Mchezo baina ya timu mbili ambazo ni Bugeni FC na Nyabiyonza FC zilizocheza mchezo wa fainali katika ligi ya Bashungwa Cup 2021.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na mgeni rasmi katika kilele cha mashindano ya Bashungwa CUP 2021 akizungumza na wakazi wa Mkoa Kagera mapema kabla ya mchezo wa fainali kuanza.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Karagwe na mwandaaji wa mashindano ya Bashungwa Cup 2021 akizungumza katika kilele cha mashindano hayo.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na mgeni rasmi katika kilele cha mashindano ya Bashungwa CUP 2021 akimkabidhi kombe mwakilishi wa timu ya Bugeni FC baada ya kuibuka washindi kwa mikwaju ya pemaliti dhidi ya washindani wao FC katika fainali za Bashungwa Cup 2021.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ametoa rai kwa wabunge hapa nchini kuziomba mamlaka zinazowazunguka kuboresh miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na viwanja vya michezo katika maeneo yao ili kuwa katika viwango vinavyotakiwa.
Mhe. Aweso amefafanua kwamba endapo viwanja vya michezo vitakuwa katika viwango vinavyotakiwa, hali hiyo itawafanya vijana wengi kushawishika kushiriki michezo mbalimbali.
Rai hizo amezitoa jana (Septemba 12) wakati akihitimisha ligi ya Bashungwa Cup iliyokuwa ikizishirikisha timu 23 kutoka kata 23 za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Kauli ya Waziri Aweso inafutia ombi la wakazi wa wilaya ya Karagwe waliozungumza kwa nyakati tofauti tofauti wakiomba Halmashauri ya wilaya hiyo kuufanyia ukarabati uwanja wa mpira wa Kayanga ili uwe na viwango vya kuruhusu mashindano makubwa ya ngazi ya mkoa na hata taifa kufanyika uwanjani hapo.
Akizungumza katika fainali hizo mwandaaji wa mashindano hayo ambaye ni mbunge wa Jimbo la Karagwe na Waziri anayesimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada za kukuza michezo katika safari ya kukuza vipaji vya vijana.
“Wote tunaamini kwenye umoja, ninamaanisha tukiungana tunaweza, Serikali inafanya kila kinachowezekana kukuza sekta ya michezo nchini, lakini si dhambi kwa mdau yeyote kutuunga mkono popote unapoweza katika kutimiza ndoto ya vijana wetu wenye vipaji vya michezo.” Alisema Waziri Bashungwa.
Fainali hiyo iliyozikutanisha timu mbili ambazo ni Bugeni FC na Nyabiyonza FC zote za wilayani Karagwe. Timu ya Bugeni FC imeibuka mshindi kwa mikwaju ya penaliti na kubeba kombe pamoja na zawadi ya shilingi milioni mbili na laki tano huku timu ya Nyabiyonza ikishika nafasi ya pili na kubeba kitita cha shilingi milioni moja laki mbili na elfu 50, huku mshindi wa tatu ambaye ni Kihanga FC akiibuka na shilingi laki saba na elfu hamsini.
Mashindano ya Bashungwa Cup yalizinduliwa rasmi mwaka 2017 na yamekuwa yakiwakutanisha vijana kila mwaka kushindania zawadi mbalimbali, lengo likiwa ni kuwaunganisha wakazi wa wilaya ya Karagwe na kuibua vipaji vya vijana kupitia mchezo wa soka.
No comments:
Post a Comment