Na WAF - DOM
KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kuwa, Serikali haitaendelea kuvumilia tabia ya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya vyuo vya afya nchini, kwani tabia hizo hupelekea kupata Watumishi wasio na ubora na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi.
Prof. Makubi amesema hayo Mei 10, 2022 wakati akifungua Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya wenye kauli mbiu ya "Huduma bora za Afya ni matokeo ya uwepo wa vyuo bora nchini," uliofanyika Jijini Dodoma.
"Hatuwezi kuwa na Watumishi bora wa Afya kwa kuvumilia baadhi ya vyuo vinavyoendekeza tabia ya udanganyifu kwenye uendeshaji wa mafunzo, hali hii inarudisha nyuma juhudi za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi." Amesema Prof. Makubi.
Amesema, hali ya udanganyifu ni kinyume cha Sheria, maadili, utaratibu na mbaya zaidi udanganyifu huu umeendelea hadi kwenye mazoezi ya mitihani ya ndani na ile ya Kitaifa kwa kuwahusisha baadhi ya wanafunzi na walimu katika maeneo yao, hii haikubaliki.
Sambamba na hilo, Prof. Makubi amewaelekeza Wasajili wa Mabaraza ya kitaaluma kuchukua hatua hatua stahiki kwa wakufunzi wanaoshiriki kwenye udanganyifu kwa kuwafutia leseni na hatua nyingine kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Aliendelea kusisitiza kuwa, Wizara haitasita kuchukua hatua kali kwa chuo chochote kitachoenda kinyume na utaratibu wa uendeshaji wa mafunzo na upimaji wa wanafunzi, ikiwa na sehemu ya uboreshaji wa utoaji huduma.
Katika kulinda ubora wa Wahitimu, Prof. Makubi ameelekeza kusitisha usajili kwa vyuo ambavyo havijakidhi utaratibu kama vile kutokuwa na miundombinu ya kufundishia ikiwemo hospitali na maabara za mafunzo kwa vitendo, msongamano wa vyuo vingi katika eneo moja hali inayopelekea wanafunzi kukosa eneo la kufanyia mafunzo kwa vitendo.
Aidha, amewapongeza Wakuu wa vyuo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya licha mazingira magumu yanayokutana nayo katika maeneo yao ya utendaji, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika utatuzi wa changamoto hizo ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Mbali na hayo, amewataka Wakuu wa vyuo kuwa Wazalendo na kuzingatia misingi ya uongozi bora kwa kushirikisha viongozi wengine katika ngazi ya maamuzi, ikiwemo katika matumizi ya fedha ili kuondoa misuguano inayoweza kuepukika.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Wakuu wa vyuo kuwa wabunifu katika utendaji wao, ikiwemo kushirikiana na Wadau mbalimbali wanaopatikana katika maeneo yao jambo litakalosaidia kupunguza changamoto katika vyuo vyao.
Naye,Mkurugenzi wa Mafunzo na rasilimali watu Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer amemshukuru Katibu Mkuu kwa kuendelea kusaidia vyuo vya mafunzo, na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyotoa ili kufikia lengo la Serikali la kuboresha huduma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment