Wawakilishi kutoka sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka nchi saba wanakutana leo jijini Dar es Salaam kuhudhuria kongamano linalolenga kuangalia namna ya kunufaika na 5G na teknolojia nyingine za kisasa za mawasiliano.
Kongamano hilo la siku tatu linafadhiliwa na Serikali ya Marekani na Taasisi ya Mafunzo ya Mawasiliano ya Simu ya Marekani (United States Telecommunication Training Institute –USTTI) kwa ushirikiano na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Tanzania. Naibu Waziri Kundo Mathew alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo, ambayo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright na Mwenyekiti wa USTTI Jim O’Conner.
Lengo la kongamano hili ni kuchangia mawazo na mbinu mbalimbali zenye ufanisi (best practices) za kutumia kikamilifu teknolojia zinazochipukia na kizazi kijacho cha teknolojia za mawasiliano ya kimtandao yasiyotumia waya (wireless networks) na wakati huo huo kushughulikia hatari na wasiwasi kuhusiana na usalama wa mtandao na faragha za watu. Semina zitakazotolewa zitaangazia mbinu bora za udhibiti (regulatory best practices), Mawasiliano ya Intaneti kuunganishwa na vitu mbalimbali (Internet of Things –IOT) na teknolojia ya satelaiti zinazozunguka zikiwa umbali mfupi kutoka uso wa dunia (Low Earth Orbit – LEO – satellite tecknology). Washiriki wa kongamano hili wametoka katika nchi za Msumbiji, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Marekani. Makampuni ya sekta binafsi yaliyowakilishwa ni pamoja na Walt Disney Company, Inmarsat, Qualcomm, American Tower, ICANN, Microsoft na Meta.
Katika hotuba yake, Balozi Wright alisema kuwa Marekani ingependa kuona kwamba duniani kote kuna uchumi imara wa kidijitali unaowawezesha raia wote kunufaika kutokana na faida nyingi za kizazi cha tano cha mawasiliano ya kimtandao (5G) na upatikanaji wa kuaminika wa mawasiliano ya intaneti.
“Kuna umuhimu mkubwa sana hivi sasa wa kuhakikisha usalama wa mitandao hii ya mawasiliano kuliko ilivyokuwa wakati mwingine wowote. Teknolojia za 5G na 6G zinaleta mageuzi makubwa mno na zitagusa kila nyanja ya maisha yetu, ikiwemo miundombinu muhimu kama vile usafiri na usafirishaji, huduma za kifedha, usambazaji wa umeme, huduma za afya na afya ya umma na huduma nyingine nyingi. Nchi na raia wanahitaji kuhakikishiwa na kuweza kuwa na imani kwamba makampuni ya mawasiliano na mamlaka za udhibiti hazita anzisha vitu vitakavyoleta hatari zitakazotishia usalama wa taifa, faragha au haki za binadamu,” alisema Balozi Wright.
Balozi Wright alisema pia kuwa kongamano hili ni mwanzo wa ubia wenye thamani ya takribani Dola za Kimarekani Milioni Moja kati ya Marekani na Tanzania katika masuala ya mawasiliano ya kimtandao unaolenga kutoa msaada wa kitaalamu/kiufundi katika teknolojia ya 5G, kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na kuimarisha usalama mtandaoni.
No comments:
Post a Comment