Mwalimu Mary Mapembe akieleza faida ya mafunzo waliyopatiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, kabla ya Dkt. Msonde kufunga rasmi mafunzo hayo.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akiwa katika picha ya pamoja na walimu wa elimu ya awali, maafisa elimu kata na Walimu Wakuu wa Mkoa wa Shinyanga na Simiyu walioshiriki mafunzo yaliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji pamoja na watendaji wa ofisi yake, mara baada ya kufunga mafunzo ya walimu wa elimu ya awali, maafisa elimu kata na Walimu Wakuu wa Mkoa wa Shinyanga na Simiyu.
Na: James Mwanamyoto – OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amesema taifa linawategemea walimu wa elimu ya awali na msingi kuwajengea msingi bora wa malezi watoto ili wawe na maadili mema yatakayowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Msonde amesema hayo wakati akifungunga mafunzo ya walimu wa elimu ya awali 202, Maafisa Elimu Kata 36 na Walimu Wakuu 36 wa Mikoa ya Shinyanga na Simiyu yaliyolenga kuwajengea uwezo watendaji hao kutoa elimu bora kwa watoto.
Dkt. Msonde amesema, Serikali inatambua mchango wa walimu wa elimu ya awali na msingi na ndio maana kupitia mradi wa BOOST inajenga miundombinu ya elimu na kuandaa mafunzo yatakayowaongezea umahiri katika kutoa elimu bora kwa watoto.
Ameongeza kuwa, Serikali imejipanga kuboresha elimu kufikia kiwango cha juu ndani ya muda mfupi ili kuwa na taifa imara lenye rasilimaliwatu yenye tija.
“Nimejionea zana na kuelezwa namna mlivyofundishwa kutumia na kutengeneza zana za kufundishia watoto, na mwalimu mzuri ni yule anayeweza kubuni zana za kufundishia kutokana na mazingira aliyopo,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Mwalimu Mary Mapembe amesema wamejifunza zana 11 za kufundishia watoto akitoa mfano wa zana ya mti wa namba na irabu ambayo itawasaidia kuwafundisha watoto kusoma na kuhesabu.
Naye, Mwezeshaji Mkuu, Bi. Alphoncina Pembe amesema walimu hao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuwajumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalum ndani ya madarasa ya kawaida na kuongeza kuwa, wamefundishwa namna ya kuchopeka masuala mtambuka wakati wa kufundisha.
No comments:
Post a Comment