Advertisements

Friday, March 22, 2024

MAKAMU WA RAIS AONGOZA SIKU YA MISITU DUNIANI NA UPANDAJI MITI KITAIFA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua muongozo wa Kitaifa wa Upandaji na Utunzaji miti wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mdodoma katika Shule ya Sekondari Same wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimwagilia maji mti aina ya Mdodoma aliyoupanda katika Shule ya Sekondari Same wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsilikiliza Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Manyinga ya mkoani Morogoro Jackline Eliabi akielezea uhifadhi wa mazingira kupitia mradi wa Eco School, wakati Makamu wa Rais akikagua mabanda katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua bidhaa mbalimbali zinazotokana na taka ngumu zilizotengenezwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Manyinga ya mkoani Morogoro kupitia mradi wa uhifadhi mazingira wa Eco School, wakati Makamu wa Rais akikagua mabanda katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua bidhaa mbalimbali zinazotokana na misitu katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wakati Makamu wa Rais akikagua mabanda katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ...

Evavani Vamgothi. Mrevedi? Jamithi?

Vamcheku. Herehoa. Ningeni Mbure

Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake kwa kutuwezesha kukusanyika hapa Same, nchi yetu na Mkoa wetu ukiwa na amani na utulivu. Napenda kuanza hotuba yangu kwa kuwaletea salamu wananchi wa Same na Mkoa wote wa Kilimanjaro kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Anawapongeza sana kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika Mkoa huu kutokana na uchapakazi wenu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Aidha, anawashukuru kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano katika Mkoa huu na Taifa kwa ujumla. Anasubiri kwa hamu kuja katika Mkoa huu ili kushiriki katika sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru. Nimefika katika Mkoa wenu jana ambapo wananchi wengi walinikaribisha kwa mapenzi makubwa. Asanteni sana. Jana tulizindua mradi wa maji wa Kikafu-Bomang’ombe na kupokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa. Leo nimekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi mliousubiri kwa miaka mingi, mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe na sasa niko hapa. Baada ya mkutano wetu huu nitakwenda kuwasalimia jirani zenu wa Wilaya ya Mwanga. Kwa ujumla, nimefurahishwa sana na niliyoyaona, nami naungana na Mheshimiwa Rais kuwapongeza kwa juhudi zenu katika kujiletea maendeleo. Kilimanjaro Oyeee! Same Oyeee!



Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 21 Machi ya kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani kwa madhumuni ya kukuza uelewa kuhusu umuhimu wa misitu na miti katika kuwezesha kuendelea kuwepo kwa sayari dunia na kuendeleza maisha ya binadamu na hivyo kuadhimishwa na kila Nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya misitu duniani kwa mwaka huu 2024 ni: “Misitu na Uvumbuzi: majibu mapya kwa dunia iliyo bora (Kwa kipare: Forests and Innovations: New solutions for a better world).



Aidha, hapa Tanzania kupitia Waraka Na. 1 wa Waziri Mkuu wa mwaka 2009, tarehe Moja Aprili ya kila mwaka iliidhinishwa kuwa Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ili kuelimisha na kuhamasisha Umma wa Watanzania kupanda na kutunza miti. Mwaka huu, Serikali iliamua kwamba maadhimisho haya yaunganishwe ili kuongeza msukumo na ufanisi katika usimamizi na utunzaji wa rasilimali misitu, na kuongeza hamasa kwa jamii kupanda miti na kuitunza kwa kutambua faida na umuhimu mkubwa wa misitu na miti katika maisha ya mwanadamu na uendelevu wa uhai katika sayari dunia. Aidha, Serikali iliamua kwamba maadhimisho haya, ambayo yalifanyika mara ya kwanza Wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza tarehe 21 Machi, 2022, mwaka huu yafanyike hapa Wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro. Napenda kushukuru Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kunialika kushiriki maadhimisho haya adhimu na kunipa heshima kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi. Vilevile, nawapongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro na Viongozi wa Wilaya ya Same kwa maandalizi mazuri na wananchi na wadau kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki kwenye maadhimisho haya.



Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Uhai na maisha ya binadamu sambamba na wanyama, ndege, wadudu na viumbe wengine, yanategemea misitu. Misitu ndiyo inayozalisha hewa safi ya oksijeni tunayovuta. Misitu pia ni chanzo cha maji tunayokunywa na kutumia kwa shughuli nyingine mbalimbali majumbani, mashambani na viwandani. Aidha, misitu inatupatia chakula, fursa za ajira na riziki (livelihood) kwa mabilioni ya watu duniani. Kutokana na misitu, tunapata vilevile bidhaa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na malighafi kwa ajili ya ujenzi, viwanda, nishati, madawa na chakula cha wanyama, ndege na wadudu. Vilevile, misitu ni makazi ya viumbe mbalimbali lakini pia hufyonza hewa ya kaboni na kuimarisha mifumo ikolojia, huzuia mmomonyoko na kurutubisha udongo. Misitu na miti inatupatia kivuli na sehemu za kupumzikia au burudani, na inatumika kupendezesha miji na mazingira kwa ujumla. Aidha, misitu huchangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mvua na ni rasilimali muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, misitu ina umuhimu mkubwa kwa baadhi ya shughuli za jadi au kimila kama vile matambiko na sherehe (mfano jando). Kama hayo hayatoshi, bidhaa zinazotokana na misitu zimetuzunguka na tunazitumia kila wakati pengine bila kutambua kuwa zinatokana na misitu. Mifano ni pamoja na samani za majumbani, ofisini na shuleni kama madawati, meza, viti, mbao za kufundishia, vitabu na madaftari. Pia, magazeti, vifungashio vya vyakula, mapambo, milango, boti na mashua, kabati na majeneza vyote vinatengenezwa kutokana na mazao ya misitu. Kwa kuzingatia yote hayo, ni dhahiri kuwa maisha duniani bila misitu na miti hayawezekani.





Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Hapa Tanzania, rasilimali misitu inakadiriwa kuwa na ukubwa wa takriban hekta milioni 48.1 ambayo ni sawa na ukubwa wa Mkoa wa Kilimanjaro mara 36. Mchango wa misitu wa moja kwa moja katika Pato la Taifa ni 3.5% tu lakini kwa hakika mchango wake usio wa moja kwa moja ni mkubwa. Mchango wa sekta hii katika bidhaa zote zinazouzwa nje ni 11%. Aidha, inakadiriwa kwamba sekta ya misitu na bidhaa zinazotokana na misitu inatoa ajira kwa Watanzania takriban milioni 4. Mbali ya kuimarisha maendeleo ya kilimo na utalii, misitu ina mchango mkubwa katika kukuza rasilimali nyingine za asili hususan maji na udongo. Si hivyo tu, rasilimali ya misitu hivi sasa inatoa huduma ya utalii ikolojia kama zao jipya la utalii ambalo linachochea uhifadhi wa misitu na upandaji miti. Hivi sasa, misitu mitano ya mazingira asilia ndiyo inatumika kwa utalii ikolojia, ambayo ni Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, Nilo na Amani katika Mkoa wa Tanga, Kazimzumbwi - Pugu na msitu wa Chome uliopo hapa Wilayani Same. Hivyo, ni dhahiri kuwa rasilimali misitu katika nchi yetu ni kubwa na ina umuhimu wa pekee katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na uendelevu wa uhai wa viumbe.



Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Licha ya manufaa hayo mengi, katika nchi yetu kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa hifadhi za misitu na ukataji holela wa miti unaotokana na shughuli za binadamu zikiwemo kilimo, makazi, uchomaji moto, ufugaji, uvunaji haramu wa mazao ya misitu, uchimbaji haramu wa madini na kusambaza magonjwa ya miti na mimea. Mathalan, katika bara la Afrika watu wapatao billioni 3 hutegemea kuni, mkaa, makaa ya mawe na kinyesi cha wanyama (hususan ng’ombe) kama nishati ya kupikia. Kwa Tanzania, inakadiriwa kwamba katika kila kaya 10, kaya 9 zinatumia nishati chafu yaani kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia. Matumizi hayo ya kuni na mkaa yana athari nyingi ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa kutokana na kuvuta moshi mwingi wenye viwango vikubwa vya sumu. Magonjwa hayo ni pamoja na kansa ya mapafu na magonjwa mengine ya mapafu (kama emphysema – unaoathiri mfumo wa upumuaji). Wastani wa kaya 1 tu kati ya kila kaya 10 hapa Tanzania ndiyo inayotumia nishati safi ya gesi na umeme kwa ajili ya kupikia majumbani. Mbaya zaidi matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia husababisha takriban hekta 469,420 za misitu kupotea kila mwaka, ambazo ni sawa na takriban nusu ya ukubwa wa Wilaya yote ya Same. Hali hii ndiyo chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari mbaya ikiwa ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji, kuenea kwa ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, magonjwa, joto kali, vifo vya mifugo kutokana na kukosekana kwa malisho na maji, kuanguka kwa uzalishaji katika kilimo cha mazao n.k. Hivyo, kwa kuongeza kasi ya kupanda miti na kutunza misitu iliyopo pamoja na kuondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia tutakuwa tumeongeza uhakika wa mvua na kuwezesha uendelevu wa uhai wa binadamu na viumbe vingine pamoja na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.









Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Naomba kuhitimisha hotuba yangu kwa kusisitiza mambo yafuatayo:



Kwanza, ni kuhusu kutumia uvumbuzi katika kutatua changamoto za uharibifu wa rasilimali misitu. Serikali inazisisitiza Taasisi za utafiti wa misitu nchini kama Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo cha Misitu Olmotonyi – Arusha na Tanzania Forests Research Institute (TAFORI) ziongeze kasi ya kufanya tafiti zinazolenga kutumia teknolojia kunusuru misitu katika nchi yetu na kuongeza ustawi wake. Jitihada hizi zijumuishe tafiti kuhusu nishati safi ya kupikia ya gharama nafuu, nishati mbadala ya kukaushia tumbaku, kubuni bidhaa mbadala wa zile zinazotokana na miti au misitu na kuhuisha mbegu za miti ya asili. Ninaitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na kituo cha Taifa cha kufuatilia hewa ya kaboni (National Carbon Monitoring Centre) na OR-TAMISEMI kushirikiana na wadau ili kupata na kuasili teknolojia za kisasa za kurahisisha ufuatiliaji na utoaji wa taarifa kwa wakati kuhusu uharibifu wa misitu (monitoring and reporting).



Pili, Ibara ya 69 (g) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 inatutaka pamoja na mambo mengine kuendeleza programu mbalimbali za upandaji miti ili kutunza mazingira na kuongeza kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Ili kufikia lengo hilo, ninazikumbusha Halmashauri zote nchini kuendeleza jitihada za kuanzisha na kuhifadhi maeneo mapya ya hifadhi ya misitu; kuhamasisha na kutekeleza kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka; kuendeleza kampeni ya kuifanya Tanzania ya Kijani; kuongeza ukubwa wa eneo la mashamba ya miti; pamoja na kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa misitu. Upatikanaji wa miche ya miti ni muhimu katika uhifadhi endelevu wa rasilimali ya misitu. Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) uhakikishe kuwa kila Halmashauri inaanzisha na kutunza vitalu vya miche ya miti katika ngazi ya Halmashauri, kata na vijiji. TFS pia ikamilishe mwongozo/kanuni za matumizi ya misumeno ya minyororo (chain saw). Aidha, ninazitaka Halmashauri za Miji, Wilaya na Majiji kuanza kuchukua hatua za kuanzisha bustani za kijani (green parks) katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupumzika, burudani na mazoezi ya viungo kwa wananchi. Aidha, bustani hizo ni muhimu katika kupendezesha miji;



Tatu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kote waandae na kusimamia utekelezaji wa Mpango kazi wa kuhakikisha lengo lililoelekezwa na Mhe. Rais la kuondoa matumizi ya nishati chafu ya kupikia ifikapo mwaka 2030 linatimia. Taarifa ya utekelezaji iwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu kila baada ya miezi sita. Kwa nafasi hii naomba tumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa na kujitoa kuwa kinara wa kueneza matumizi ya nishati safi katika nchi yetu na bara lote la Afrika. Mheshimiwa Rais pia amefanya kazi kubwa ya kulinda rasilimali misitu na kuongoza kampeni za kitaifa za kupanda na kutunza miti Tanzania bara na Tanzania Zanzibar.



Nne, Halmashauri zifanye jitihada za kujifunza kuhusu fursa na changamoto zilizopo katika biashara ya kaboni pamoja na uendeshaji wa biashara hiyo kutoka halmashauri zinazofanya vizuri kama vile Halmashauri za Tanganyika, Karatu na Mbulu. Aidha, ninaitaka OMR - Mazingira kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kukamilisha kanuni na taratibu zinazosimamia biashara ya kaboni hapa nchini haraka iwezekanavyo.



Tano, nimepata taarifa juu ya changamoto ya Ziwa Jipe (ambalo ndiyo chanzo cha maji cha Bwawa la Nyumba ya Mungu) kujaa magugu maji. Tatizo hili linachangiwa kwa kiasi fulani na matumizi ya ardhi yasiyozingatia uhifadhi na kusababisha mmomonyoko ambapo udongo huingia ziwani humo. Nawaomba wananchi wazingatie maelekezo na ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuhifadhi ardhi. Ninafahamu kuwa OMR- Mazingira imetenga bajeti kukabiliana na suala la magugu maji katika Ziwa Jipe. Simamieni utekelezaji ipasavyo ili kumaliza changamoto hiyo kwenye Ziwa Jipe.





Sita, vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa na hamasa katika utunzaji misitu na miti. Ninavitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kuhabarisha umma kuhusu upandaji na utunzaji wa miti, pamoja na kufichua vitendo vya uharibifu wa misitu ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za udhibiti haraka.



Saba, viongozi wa Serikali ya Mkoa, Chama Cha Mapinduzi na Mheshimiwa Mbunge wamenijulisha juu ya changamoto kadhaa katika Wilaya hii ya Same na Mkoa kwa ujumla. Naomba nitoe maelekezo kuhusu changamoto hizo kama ifuatavyo:
(i) Kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe. Mradi huu umesuasua kwa muda mrefu takriban miaka kumi. Muda mfupi uliopita nimetoka kukagua maendeleo ya mradi huu na napenda kuwajulisha wananchi wa Mwanga, Same na Korogwe kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza mradi huu uanze kutoa maji kwa wananchi ifikapo mwezi Juni mwaka huu bila kukosa. Hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Timu yako kuanzia leo hakuna kulala kabisa. Watu wako wapige kambi kwenye eneo la mradi. Msimamieni Mkandarasi katika kila hatua. Agizo hili la Amiri Jeshi Mkuu litekelezwe ili kilio cha maji cha wananchi hawa kihitimishwe. Mkimzingua Mama kwa hili, msubiri taarifa ya Zuhura Yunus usiku.
(ii) Kuhusu changamoto ya umeme kukatikakatika, naitaka TANESCO chini ya usimamizi wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuchukua hatua za haraka kupunguza na kuondoa kabisa mgao wa umeme kadiri uzalishaji wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unavyoongezeka. Na hili liende sambamba na kazi ya kuimarisha usambazaji wa umeme kwa kubadilisha nguzo ambazo zimeoza.
(iii) Changamoto ya wanyama kuharibu makazi na mashamba ya wananchi na hata kusababisha vifo. Serikali itaongeza nguvu na uwezo wa Taasisi za uhifadhi (TAWA na TANAPA) kuendesha doria za kudhibiti wanyama hao, kutoa mafunzo na vifaa kwa wananchi katika vijiji vinavyokumbwa mara kwa mara na kadhia hiyo kwa ajili ya kufukuza wanyama pori kwenye maeneo ya wananchi. Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya Fedha kulipa kifuta machozi kwa wahanga wa uharibifu wa makazi na mashamba baada ya kufanya uhakiki. (iv) Changamoto ya ubovu wa barabara hasa za milimani. Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti ya TARURA kutoka takriban Shilingi milioni 660 (2021/2022) hadi Shilingi bilioni 7.4 (2023/2024). Hivyo, nawasisitiza TARURA kufanya kazi kwa karibu na Madiwani ili kuchagua barabara muhimu zinazohitaji matengenezo ya haraka. (v) Kuendelea kuwepo kwa kilimo cha mirungi na bangi katika kata za Tae, Saweni na Kirangare. Licha ya jitihada za kudhibiti kilimo hiki (kuteketeza mashamba ya mirungi na bangi, kuwakamata wahusika na mirungi/bangi yenyewe pamoja na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, bado baadhi ya wananchi wanaendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi ambayo ni dawa za kulevya. Napenda kusisitiza kuwa matumizi ya mirungi/bangi yana madhara makubwa kwa binadamu na hasa vijana. Iko hatari ya vijana wetu hao kugeuka mazezeta. Kwa hiyo nawasihi watumiaji wa mirungi/bangi waachane nayo ili kujiepusha na madhara hayo ya muda mrefu. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na madawa ya kulevya na Wananchi wazalendo, waendeleze operesheni za kudhibiti biashara ya mirungi na dawa nyingine za kulevya katika Mkoa huu. Pia, naielekeza Wizara ya Kilimo itumie Wataalam wa Kilimo waliopo Mkoani na Taasisi zake za Utafiti kubuni mazao mbadala ya kibiashara yanayolipa vizuri na yanayoweza kulimwa kwenye kata hizo.



Nane, Huu ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa. Maendeleo ya haraka kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kuwepo kwa aina ya viongozi tunaowachagua. Hivyo, ninawaomba wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa mingine nchini kujiandaa kushiriki katika kuwachagua viongozi waadilifu na wenye uwezo. Nawaomba pia wananchi wote wenye sifa za uongozi kujitokeza kuomba kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi. Hii ni hatua muhimu sana katika kuimarisha demokrasia katika nchi yetu wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.





Wahe. Viongozi, Wageni Waalikwa na Wananchi Wenzangu;



Mwisho, nawashukuru ninyi nyote mliotenga muda wenu ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa hapa Wilayani Same. Hakika maadhimisho haya yamefana sana. Natoa rai kwa Watanzania wote kuendeleza jitihada za kupanda miti na kuitunza ili kuweza kukabiliana na ukame, mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo hivi karibuni yamekuwa yakiyakumba maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kusababisha madhara makubwa. Aidha, navitaka vijiji vyote kutunza misitu ya asili iliyoko katika maeneo yao.



Baada ya kusema hayo, nawashukuru kwa dhati kabisa kwa kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa kwa mwaka 2024. Nawatakia usimamizi mzuri wa rasilimali misitu.

No comments: