ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 7, 2024

MAFUNZO KWA MAFUNDI MCHUNDO WA MAJOKOFU NA VIYOYOZI


Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa (katikati) akizungumza na baadhi ya mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu wa jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Washiriki wakiwa katika mafunzo kwa mafundo mchundo wa viyoyozi na majokofu kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) cha Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Mhandisi Goodluck Rulagora akitoa mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya mafundi mchundo na viyoyozi kutoka Jijini Dar es Salaam ambao wanashiriki warsha ya mafunzo kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na baadhi ya mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu wa jijini Dar es Salaam baada ya kufungua warsha ya mafunzo kuhusu utekelezaji wa wa Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imetoa rai kwa mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu kuzingatia matumizi salama ya kemikali wakati wa kuhudumia vifaa hivyo ili kuepuka kusambaa angani kwa kemikali au gesi hizo na kusababisha uharibifu wa tabaka la ozoni au ongezeko la joto duniani.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kamilembe Mutasa wakati akifungua mafunzo kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni leo Mei 06, 2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa mafundi hao kuhusu matakwa ya itifaki hiyo ambapo wanasayansi walivumbua kemikali hizo mwanzoni mwa miaka ya 1970 ambazo hujipenyeza angani na kumong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni kwa kuruhusu mionzi au miale ya jua kufika katika uso wa dunia na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Bi. Kemilembe ametaja madhara hayo kuwa ni magonjwa ya saratani ya ngozi, uharibifu wa macho unaosababisha upofu na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine.

Amesema kemikali zinazoharibu tabaka hilo zinatumika katika majokofu na viyoyozi, vifaa vya kuzima moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na kilimo cha maua na hifadhi ya nafaka katika maghala.

Kutokana na changamoto hiyo, Bi. Kemielembe amesema juhudi zimeendelea kufanyika tangu mwaka 1985 baina ya Serikali kitaifa na kimataifa kukubaliana kuanzisha Mkataba wa Vienna na Hifadhi ya Tabaka la Ozoni na hatimaye Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni ambapo shabaha yake kuu ni kusitisha utengenezaji na utumiaji wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni.

Ameongeza kuwa Itifaki ya Montreal imekuwa ikifanyiwa marekebisho mbalimbali kutokana na tafiti zinazoainisha kemikali mbalimbali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni au kuwa na athari zingine za kimazingira kama kusababisha ongezeko la joto duniani.

Hivyo, mafunzo hayo yanayohusu njia bora za kuhudumia vifaa ikiwemo majokofu na viyoyozi pasipo kuathiri mazingira yanatolewa na Mtaalamu wa Kimataifa wa viyoyozi na majokofu kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa la Mazingira (UNEP) Bw. Freeborn Taruvinga kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Bagamoyo Mhandisi Goodluck Rulagora pamoja na Bw. Said Mziwanda koka kutoka Chuo cha Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe, jijini Dar es Salaam chini ya shughuli wezeshi ya kujenga uwezo wa kitaasisi katika kutekeleza Itifaki ya Montreal inayotekelezwa na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.


No comments: