Thursday, July 11, 2024

KILIMO KUKUTANISHA WADAU LEO KUJADILI VIPAUMBELE MIFUMO YA CHAKULA


Wizara ya Kilimo inaandaa warsha kubwa ya kuwaunganisha wadau katika vipaumbele vya kuharakisha mifumo ya chakula na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo warsha hiyo itakayofanyika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam kesho Alhamisi pia inalenga kuweka mikakati ya kuharakisha maendeleo katika mipango ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kabla ya matukio muhimu yanayohusu mifumo ya chakula duniani mwaka huu.

Matukio hayo ni pamoja na Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFSF) 2024, Mkutano wa Maendeleo Endelevu UN ( Sustainable Development Impact Summit) na COP 29, ambayo yataendelea kuangazia uhusiano kati ya mifumo ya chakula, tabianchi na mazingira.

Mkutano huu unaendeleza kasi katika sekta ya kilimo kufuatia Mkutano wa Tabianchi Afrika, COP 28 na Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika 2023, ambalo Tanzania iliandaa kwa kaulimbiu "Kupona, Kujenga Upya, Kuchukua Hatua: Ufumbuzi wa Afrika kwa Mifumo ya Chakula".

Ni katika jukwaa hilo ambapo mpango wa "Kujenga Kesho Iliyo Bora" (BBT), mpango muhimu kwa vijana katika biashara ya kilimo, ulizinduliwa .

Lengo la mpango huo ni kuhamasisha ushiriki wa vijana wa Tanzania katika biashara ya kilimo kwa ajili ya maisha endelevu na bora.

Mkutano utgakaofanyika kesho unalenga kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika mipango kama hii huku ukiangalia kasi ya njia zake za mfumo wa chakula.

Tanzania imebadilisha mwelekeo wa sera za nchi katika kuhakikisha usalama wa chakula unapatikana kwa muda mfupi huku pia ikijenga mifumo ya chakula inayojumuisha zaidi ikiwa endelevu, yenye lishe na inayoweza kukabiliana na mabadiliko kwa muda wa kati huku ikilisha Bara la Afrika kibiashara.

Tukio hili, kwa hiyo, linaonyesha dhamira ya Wizara ya Kilimo katika kuongoza mipango ya mabadiliko katika sekta ya mifumo ya chakula, kuhakikisha Tanzania inabaki mstari wa mbele katika uvumbuzi wa kilimo na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

No comments: