Saturday, July 27, 2024

WAZIRI NDEJEMBI ATAKA WATENDAJI ARDHI KUONDOA URASIMU NA KUTOA HATI KWA WAKATI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo alipokutana na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara katika makao makuu ya wizara Mtumba jijini Dodoma tarehe 27 Julai 2024.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara katika makao makuu ya wizara Mtumba jijini Dodoma tarehe 27 Julai 2024.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na watumishi wa wizara ya ardhi alipowasili makao makuu ya wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea ua mara baada ya kuwasili makao makuu ya wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma tarehe 27 Julai 2024. Katikati ni Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda.Waziri was wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara, wajumbe wa Menejimenti pamoja na viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi mara baada ya kufanya kikao katika makao makuu ya wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma tarehe 27 Julai 2024.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha na Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga (Kulia) na Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera (kushoto) alipowasili kwa mara ya kwanza makao makuu ya wizara tarehe 27 Julai 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi amewataka Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Ardhi kuondoa urasimu na kutoa hati milki za ardhi kwa wakati.

“Tuondoe urasimu, kama mtu ana nyaraka zote zinazohitajika, tuwape hati zao na tukumbuke sisi ni watoa huduma kwa wananchi n ani wizara wezeshi, hati zitolewe kwa wakati na hati zilizotayari wananchi wajulishwe waje wachukue hati zao” amesema Mhe. Ndejembi.

Mhe. Ndejembi amesema hayo Julai 27, 2024 wakati wa kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo mara baada ya kupokelewa Makao Makuu ya Wizara yaliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kufanya kazi kwa weledi na kusimamia vizuri mifumo ya TEHAMA na Mawasiliano ili wananchi wapate haki yao katika sekta ya ardhi.

“Sijaja kutengua kazi mnazoendelea kuzifanya, nimekuja kuongeza nguvu. Tuzidi kufanya kazi vizuri na kuhakikisha mifumo yetu ya kiwizara kuanzia wilaya, mikoa na wizara ifanye kazi vizuri. Ni vizuri tusimamie haki ya wananchi na mifumo ifanye kazi yake kutoa haki,” amesema Waziri Ndejembi.

Aidha, ameendelea kusisitiza kuendelea kwa Klinik za Ardhi ambapo amesema kasi katika klinik hizo lazima iongezwe kwa kuwa wakati mwingine wananchi inakuwa vigumu kuwafikia makamisha wa ardhi wasaidizi wa mikoa.

Akimkaribisha Waziri Ndejembi kwenye kikao na Menejimenti ya Wizara hiyo, Naibu Waziri Geofrey Pinda amesema Wizara hiyo ina ofisi katika halmashauri zote nchini na kumhakikishia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ili kuwahudumia wananchi katika sekta ya Ardhi.

Awali Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga akimkaribisha Waziri wa Ardhi wizarani amemuelezea muundo wa wizara na kuainisha idara na vitengo vya wizara hiyo sambamba na taassisi zilizo chini ya wizara hiyo.

No comments: