Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akikagua kazi mbali mbali zilizofanywa na Wanafunzi waliopatiwa Mafunzo ya Sayansi na Ubunifu kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea(KOICA) katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Kitaifa katika Mashindano ya Sayansi na Ubunifu kwa wanafunzi wa Skuli za Sekondari Zanzibar yaliyofanyika katika Ukubi wa Madinat Al Bahr Mbweni jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Mradi wa Kuimarisha Ubora wa elimu ya Sekondari Zanzibar unaodhaminiwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) unalenga kuimarisha ubora wa elimu kwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunza kwa kuwajengea uwezo walimu katika kutekeleza mbinu za umahiri wa kufundishia.
Ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Kitaifa katika Mashindano ya Sayansi na Ubunifu kwa wanafunzi wa Skuli za Sekondari Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahri Mbweni jijini Zanzibari.
Amesema kupitia Mradi huo jumla ya Maabara kumi(10) za Kisayansi zimejengwa katika skuli mbali mbali za Sekondari Unguja Pemba ambazo zinawasaidia wanafunzi kujifunza masono ya Sayansi kwa vitendo jambo ambalo limesaidia kuongezeka ufaulu kwa wanafunzi wa kada ya sayansi.
Makamu wa Pili wa Rais amesema Jumla ya walimu 2, 276 wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kingereza pamoja na wenyeviti wa skuli 2,288 wamepatiwa mafunzo ya kuimarisha uwezo ambayo yamechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha 4 Zanzibar.
Aidha Mhe.Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kuweka mazingira bora kwa wadau wa elimu kili kutekeleza na kufanikisha miradi mbali mbali ikiwemo mradi wa Sayansi na Ubunifu Sambamba na kuutaka uongozi wa Wizara ya Elimu Zanzibar kuhakikisha wanasimamia ipasavyo malengo ya mradi huu.
Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira ya kufundishia na kujifunza hususan ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi na kufikia lengo la Serikali la kuwa wanafunzi wote waweze kuingia skuli kwa mkondo mmoja wa asubuhi kwa idadi ya wanafunzi 45 kila darasa ifikapo mwaka 2025.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea ( KOICA ) wamewekeza katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuleta mageuzi ya elimu nchini kwa kuhamasisha, na kutoa mafunzo ya sayansi na ubunifu ambayo yamewawezesha walimu kufundisha kwa njia za kisasa na wanafunzi kujifunza kidijitali zaidi.
Mhe. Lela amesema jitihada kubwa zilizofanywa na KOICA kwa kushirikiana na GNTZ, UNOPS na NIRAS kwa kujenga maabara za kisasa zenye vifaa vya kisasa, kutoa Mafunzo kwa viongozi wa kamati pamoja na walimu wa sayansi zimetoa mafanikio chanya hasa katika kukuza kiwango cha ufauli Zanzibar.
Amesema Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itaendelea kutoa mashirikiano kwa Shirika la KOICA na mashirika mengine ili kuhakikisha Sekta ya elimu inazidi kutanua wigo mpana wa mafanikio na kufikia malengo ya Serikali ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) Bwana MANSHIK SHIN amesema Korea itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya Elimu kwa kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia katika Skuli za Zanzibar sambamba na kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu nchini.
Mkurugenzi MANSHIK SHIN amesema KOICA imeweza kutoa mafunzo ya Sayansi na Ubunifu kwa zaidi wa walimu 1500 kutoka skuli mbali mbali za Unguja na Pemba, kujenga maabara 10 zilizojitosheleza kwa masomo ya Sayansi pamoja na kufanikiwa kuwarudisha skuli wanafunzi ambao waliacha skuli kwa sababu mbali mbali za kijamii.
Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya skuli 33 ambapo skuli 11 ziliingia katika hatua ya Fainali na Skuli ya Mpapa Sekomdari kuibuka mshindi wa Mashindano hayo kwa mwaka 2024 na kuzawadiwa Cheti, TV, laptop na vishkwambi kwa ajili ya wanafunzi walioshinda.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea na kukagua kazi mbali mbali za ubunifu zilizofanywa na wanafunzi hao hasa katika sekta ya uchumi wa Bluu.
No comments:
Post a Comment