WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Mhe William Lukuvi akizingumza wakati akifungua maonyesho ya saba ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi mkoani Singida leo Septemba 10, 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi amefungua rasmi Maonesho ya Saba ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoani Singida ambayo yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)
Wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Mheshimiwa Lukuvi amesema kuwa maonesho hayo yatafungua fursa za Kiuchimi kwa wafanyabiashara, wakulima na wafanyabiashara wa Singida na Mikoa ya Jirani.
Waziri Lukuvi Aliongeza kuwa, Maonesho hayo yatawezesha wananchi kupata huduma za uwezeshaji ikiwemo mitaji, mikopo nafuu, dhamana za mikopo, vifaa, mashine au mitambo, urasimishaji ardhi,urasimishaji biashara, huduma za msimbomilia, ujuzi, ithibati ya bidhaa, huduma za sheria, huduma za ushirika, huduma za ushauri wa kitalaam, elimu rasmi na elimu ya ufundi stadi, kuunganisha wananchi na fursa,na ukaguzi wa bidhaa.
Mhe. Lukuvi alibainisha kuwa, Maonesho hayo ni muhimu kwa kuwa yanakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji wakiwemo, Wizara, Mikoa, Halmashauri; Taasisi zinazosimamia Mifuko na Programu za Uwezeshaji, Taasisi za Fedha, Wafanyabiashara, Kampuni, Taasisi za Elimu na Tafiti, Wakulima, Wafugaji na Wajasiriamali.
Aliongeza kuwa, Maonesho hayo yana lengo la kuhakikisha kuwa washiriki wanabadilishana ujuzi, maarifa, uzoefu na teknolojia mbalimbali ambazo zinatumika katika kukuza ushiriki wa wananchi katika shughulli za kiuchumi.
“Nina imani kuwa, Maonesho haya yatatoa fursa nyingi kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na Mikoa mingine.” Alisisitiza
Akiongea kwa Niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge naa Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Bw. Condrad Milinga amesema kuwa pamoja na maonesho hayo kutoa fursa mbalimbali kwa wajasailiamali, wananchi pia watapata mafunzo na ujuzi kuhusu masuala mbalimbali kutoka kwa Washiriki wa Maonesho na kutoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho hayo.
Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (NEEC), Bi Beng’ Issa amesema kuwa kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa lengo la kujenga uchumi na kuwaondoa wananchi katika umaskini.
“Juhudi hizo ni pamoja na kuanzisha mifuko na program za uwezeshaji mbalimbali kwa lengo la kutoa mikopo au dhamana ya mikopo kwa wananchi kwa masharti nafuu, kutoa ruzuku pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi ili waweze kukopesheka au kuhudumiwa na wadau wengine.” Alibainisha
Aliendelea kufafanua kuwa, mpaka sasa Baraza linaratibu Jumla ya Mifuko ya Uwezeshaji na Programu 72 ambayo 62 ipo Serikalini na 10 ipo Sekta binafsi, hivyo Lengo kuu la Maonesho haya ni kutoa uelewa wa fursa za Mifuko kwa Wananchi ambapo ilionekana mifuko mingi haifahamiki kwa wananchi hivyo kuchelewesha kufikisha huduma za uwezeshaji kwa wananchi.
Maonesho hayo ya siku Saba yaliyofunguliwa leo Mkoani Singida yana Kaulimbiu inayosema “Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Unufaike na Fursa za Uwezeshaji”
No comments:
Post a Comment