ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 24, 2024

SERIKALI ITAENDELEA KUONGEZA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuifungua Skuli ya Sekondari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ufunguzi huo uliyofanyika 23-10-2024, ikiwa ni Wiki ya kumpongeza Rais wa Zanzibar Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa mafanikio ya Miaka Minne ya Uongozi wake wa Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwani ni sekta ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Skuli mpya ya Sekondari ya ghorofa tatu, Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya kupongeza juhudi za Serikali ya awamu ya nane kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa miaka minne ya Dk. Mwinyi.

Amefahamisha kuwa uzinduzi wa skuli hiyo ni kuimarisha mifumo na miundombinu ya elimu ili kufanikisha mageuzi makubwa yanayoendana na teknolojia ya sasa ulimwenguni.

“Hii ni dunia ya teknolojia, hivyo tunaweka kipaumbele katika kuimarisha teknolojia ili vijana waende sambamba na mabadiliko ya dunia na kuongeza ufaulu wao” ameeleza Rais Dk. Mwinyi.

Amesema fungu kubwa la bajeti hiyo litaelekezwa zaidi kwenye kuimarisha mifumo ya elimu, ujenzi wa miundombinu ya skuli za kisasa ikiwemo maabara, vyumba vya kompyuta, maktaba, kumbi za mikutano ambazo hutumika kwa kufanyia mitihani ya wanafunzi.

Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa hadi sasa Wizara ya Elimu imetengewa bajeti ya shilingi bilioni 830 ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia shilingi Trilioni moja kutoka bajeti ya miaka mitatu nyuma ya bilioni 83.

Aidha, amebainisha, tayari Serikali imejenga madarasa 2738 kwa kuvuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025 ambayo ilielekeza kujengwa madarasa 1500, hatua hiyo inakusudia kutekeleza adhma ya Serikali ya kuona wanafunzi wanasoma kwa mkondo mmoja chini ya wanafunzi 45 katika darasa moja huku serikali ikiweka mkazo zaidi kwenye masomo ya hisabati na sayansi.

“Kuanzia sasa lazima darasa lisizidi watoto 45 nchi nzima” alisisitiza Dk. Mwinyi.

Kuhusu maslahi ya walimu Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuongezaa hasa kwa wanafanyakazi wenye mazingira magumu, huku akiwasisistiza vijana kusoma zaidi kwani Serikali yao inaendelea kuwajengea mazingira mazuri.

Akizungumzia ajira mpya za walimu, Dk. Mwinyi ameeleza tayari Serikali imeajiri walimu 3600 na inalenga kuongeza ajira za walimu zaidi hasa kwa kada za sayansi na hesabati.

Hata hivyo, ameeleza kufarajika kwake na mafanikio makubwa katika sekta ya Elimu ambayo yamechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kufikia asilimia 96.6 kwa kidato cha sita na asilimia 88 kwa kidato cha nne kutoka asilimia 55 kabla ya miaka minne ya uongozi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema, ujenzi wa Skuli za ghorofa, Kaskazini, Unguja umewaletea Faraja wazazi na wanafunzi wa mkoa huo kwa tatizo la umbali wa kufuata elimu katika skuli za mjini.

Amenasihi kuwa njia sahihi ya kuleta uchumi imara na maendeleo kwa Taifa ni kuwekeza kwenye elimu kwa wote kwani maedeleo hayana Chama, kwa mustakbali mwema wa kuyatunza na kulinda. Hivyo, amewasisitiza wazazi na walezi kufanya kazi za ziada kusimamia elimu ya watoto wao kwani suala la kuipatia elimu jamii sio la chama ni la wote, sambamba na kuionya jamii kuepuka upotoshwaji unaofwanywa na watu wasioitakia nchi maendeleo ambao wamekua wakisambaza taarifa potofu.

Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, amemsifu na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kubeba jukumu la kuiletea mageuzi makubwa Sekta ya Elimu, kwa kuweka Fedha nyinyi za kutekelezwa miradi mbalimbali ya elimu.

Amesema, jitihada hizo ikiwemo kuwekeza vifaaa na miundombunu ya kisasa ya kufundishia zitasaidia kwenye mchango wa maendeleo ya taifa kwa kutoa wataalamu wakutosha watakaokuwa tayari kushindana katika soko la ajira ulimwenguni.

Akitoa taarifa ya kitaamu ya ujenzi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mkokotoni ya ghorofa tatu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said amesema, ulianza mwezi Mei 2023 na kukamilika Oktoba 2024 umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.1, una madarasa 42, vyoo 52, chumba cha kompyuta, maabara, maktaba. Skuli hiyo itachukua wanafunzi 1890 kwa mkondo mmoja.

Mkuu wa Mkoa Kaskazini, Unguja, Rashid Hadid Rashid amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga shilingi bilioni 50.2 kwaajili ya miradi ya Elimu tu kwa Mkoa huo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 40.9 zimetumika kwa ujenzi wa skuli sita za ghorofa kwa maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ikiwemo Skuli ya ghorofa ya Bumbwini Misufini iliyogharimu bilioni 6.1, Skuli ya Donge shilingi bilioni 4.6, Tumbatu bilioni 7.025 na ujenzi wa Skuli ya Ghorofa Gamba unaoendelea utagharimu bilioni 11.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments: