ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 21, 2024

TAKUKURU SONGWE YATAHADHARISHA NA KUWAASA WAPIGA KURA.


Na Mwandishi wetu, Songwe.
Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu wa 2024, wananchi na wapiga kura mkoani Songwe wameaswa na kutahadharishwa wasikubali kutumika kama madaraja ya watu wasio na sifa za kuwa viongozi kupata uongozi sababu ya kupewa rushwa.

Wito na tahadhari hiyo ilitolewa jana mjini Mloo, mkoa wa Songwe na mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Songwe, Frida Wikesi wakati wa bonanza la kupinga rushwa lililoandaliwa na taasisi hiyo. Bonanza ambalo liliwashirikisha takribani wanafunzi 200 wa shule za sekondari na vyuo.

Amesema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi huo kuna watu ambao wanafahamu hawana sifa za kuwa viongozi, lakini wanataka waombe uongozi kwa kutegemea fedha ambazo watatoa rushwa wakati wa kura za maoni ndani ya vyama vyao na wakati wa uchaguzi. Hivyo kuwafanya wanachama wa vyama vyao na wapiga kura kuwa ni madaraja ya kuwapitisha ili wapate uongozi.

Aliwaasa wananchi mkoani humo wakumbuke na watambue kwamba kura zao zina thamani kuliko kitu chochote. Kwani kura zao ndizo zitatengeneza mwelekeo wa maisha yao katika maendeo, uchumi na huduma za jamii.

" Mkiwachagua watu wasio faa mtashindwa kuwaondoa hadi miaka minne mingine na kwakuwa walitoa rushwa hamtakuwa na uwezo wa kusema chochote juu yao," Wikesi alionya.

Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Songwe aliwaasa wananchi hao wa mkoa wa Songwe kwamba wanapiga kura watangulize uzalendo, masilahi ya taifa na maendeleo ya jumla badala ya masilahi yao binafsi. Huku akiwakumbusha kuwa rushwa ni dhambi kwa mujibu wa imani za dini, lakini pia nikosa kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwahiyo waepuke kujihusisha kwa njia yoyote vitendo vya rushwa.

Aidha Wikesi aliwaomba wananchi wahamasishane kuanzia katika ngazi ya familia kwenda kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura. Kwani bila kujiandikisha hawataruhusiwa kupiga kura. Hali ambayo itasababisha wapoteze haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Kwa upande wao washiriki wabonanza hilo(wanafunzi) waliiomba TAKUKURU kuandaa mabonza ya aina hiyo kila mwaka. Kwani yana umuhimu mkubwa kutokana na uzito wa elimu inayotolewa kupitia mabonanza hayo.

No comments: