ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 5, 2024

WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU WATAKIWA KUENDELEZA NEEMA ZA AMANI NA UTULIVU


Waumini wa Dini ya Kiislamu na watanzania kwa ujumla kuendelea kuzishukuru neema zilizopo nchini zikiwemo amani na utulivu pamoja na maendeleo yanayofanya na viongozi wetu wakuu wa nchi.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid RAISA RASHED AL- FALASII uliopo TAVETA Wilaya ya Magharibi “B” mara baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema kuwa neema zilizopo nchini za amani na maendeleo yayofanya na kusimamiawa na viongozi wakuu wa nchi ni jambo la kuenziwa na kusimamiwa na kila mwananchi ili Allaha azidi kuwazidishia neema na Baraka sambamba na kuwatia moyo viongozi wakuu kama dini ilivyoelekeza kuzishukuru neema zote anazojaaliwa mwanaadamu.

Alhajj Hemed amesema maandiko katika vitabu vitakatifu vinaelezea umuhimu wa kudumisha umoja, upendo na mshikamono baina ya waumini hivyo amewasihi waumini hao kuacha kudharauliana na kubezana jambo ambalo hupelekea ugonvi na mifarakano katika jamii zetu.

Sambambana hayo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wazazi na walezi kuwasimamia vijana wao katika maadili na kuwapatia elimu zote mbili ya dunia na akhera kwa manufaa yao wenyewe na Taifa kwa ujumla jambo ambalo litapelekea kupata viongozi bora wa Serikali pamoja na wanazuoni wenye kuisimamia dini ya kiislamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni lazima kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha anawasimamia vijana wake ili kuwakinga na matendo maovu na machafu yatakayosababisha uvunjifu wa amani sambamba na kuwakinga na matendo ya uzalilishaji na madawa ya kulevya.

Mapema akitoa khutba ya sala ya Ijumaa, sheikh JUMA ZUBEIR SULTAN amewataka waislamu kuondosha tofauti zao za kidunia na kushirikamana katika kufanya Ibada ili kufikia lengo la kuumbwa kwao hapa duniani.

Sheikh ZUBEIR amesema Mtume Muhammad(S,A,W) ndio kigezo cha waumini wa dini ya kiislam hivyo waislamu wanapaswa kufuata nyanyo zake ili kuweza kupata radhi za ALLAH hapa duniani na kupata mafanikio makubwa kesho akhera.

Wakati huo huo makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed alimtembelea na kumjuulia hali Mzee Sukwa Said Sukwa aliekuwa katibu Mkuu UVCCM Taifa nyumbani kwake Mpendae Zanzibar.

No comments: