ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2024

ADEM YAWAKUTANISHA WALIMU WAKUU 816 MKOANI RUVUMA KUWAPATIA MAFUNZO


Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kukuza sekta ya elimu hapa nchini Walimu Wakuu wametakiwa kufahamu majukumu, maono na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Aidha wakuu hao wamehumizwa kuweka misingi imara ya kutekeleza maagizo ambayo yanatolewa na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kwa lengo la kuwafundisha watoto kwa kuzingatia misingi ya weledi ambayo itawafanya waweze kuongeza kiwango cha ufaulu pamoja na kutimiza ndoto zao.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Maulid J. Maulid wakati wa kufunga rasmi mafunzo ya Walimu Wakuu wa shule za msingi wapatao 816 kutoka Mkoani Ruvuma ambayo yamefanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea.

“Sekta ya elimu ina jukumu la kuwaandaa Watoto ili kuleta maendeleo katika sekta zingine, hivyo walimu Wakuu mkatekeleze zana ya uongozi bora kwa kuwasimamia walimu shuleni kufundisha kwa ufanisi unaotakiwa ili wanafunzi watimize ndoto zao”. Amesema Dkt. Maulid.
Naye Afisa elimu Mkoa wa Ruvuma, Bi. Edith Mpenzile akizungumza na walimu wakuu hao amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya elimu hasa katika eneo la uboreshaji wa miundombinu ya elimu Mkoani Ruvuma.

Aidha Mwalimu Mpenzile amewasisitiza Walimu Wakuu hao kwenda kusimamia ustawi na usalama wa wanafunzi shuleni kwani Watoto wanapokuwa shuleni usalama na ustawi wao ni jukumu la mwalimu.

“Tukawe mfano na chanzo cha mabadiliko ya uongozi na usimamizi wa shule, tusimamie usalama na ustawi wa wanafunzi, nasisitiza tuipe taaluma kipaumbele lakini malezi ya watoto tusiache nyuma”. Amesema Mwl. Mpenzile
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu-ADEM umeendesha Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu 816 wa Mkoa wa Ruvuma kwa siku tatu kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba, 2024 yakilenga kuwajengea uwezo walimu wakuu kuhusu uongozi, usimamizi na uendeshaji fanisi wa shule katika halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.

Hii ni awamu ya tatu ya mafunzo hayo ambayo yanafanyika katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Ruvuma ikihusisha jumla ya Walimu Wakuu 8,551 yakiendeshwa na ADEM chini ya mradi wa BOOST.

No comments: