Wednesday, November 20, 2024

BALOZI MBUNDI AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA USHIRIKIANO WA KIKANDA WA UJERUMANI



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi amekutana kwa mazungumzo na Mkuu wa Ushirikiano wa Kikanda wa Ujerumani, Bi. Julia Kronberg katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 19 Novemba, 2024.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo katika eneo la biashara, ujenzi wa miundo mbinu, afya, kujenga uwezo wa rasilimali watu, kuwainua wanawake na vijana kiuchumi.
Aidha, katika mazungumzo hayo Balozi Mbundi ameeleza kuwa Tanzania na Ujerumani zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika miradi ya maendeleo ambapo Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ limekuwa likichangia shughuli mbalimbali nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

‘’ Ushirikiano uliopo ni ishara ya kuendelea kukua kwa Jumuiya imara ya Afrika Mashariki kwakuwa ushirikiano huo kwasasa unatimiza miaka 20 tangu uanzishwe na umewezesha kutekelezwa kwa miradi yenye mafanikiao kupitia utaratibu maalum uliowekwa na pande zote mbili’’, alieleza Balozi Mbundi.
Pamoja na masuala mengine Balozi Mbundi ameainisha maeneo yanayohitaji usaidizi katika Jumuiya hiyo. Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kuwawezesha vijana katika shughuli za kilimo, kujenga uwezo kwa sekta binafsi ili kuwapa uelewa juu ya utafutaji wa masoko na usafirishaji wa bidhaa za biashara, utunzaji wa mazingira, matumizi ya nishati safi, na kuongeza thamani ya bidhaa za biashara kama vile ngozi.

Naye, Bi. Julia Kronberg amesisitiza kuwa GIZ kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inaendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano wake na EAC kwa kufadhili miradi mbalimbali katika ukanda huo.

‘’GIZ inashirikiana na Baraza la Biashara Tanzania ambapo imekuwa ikipata fursa ya kukutana na sekta binafsi katika ukanda wa EAC na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara mipakani’’, alisema Bi. Julia.

Pia, ameeleza kuwa GIZ kwa upande mwingine imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kusaidia jitihada za kuimarisha huduma za sekta ya afya katika ukanda wa EAC na imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Umoja wa Ulaya ili kuweka nguvu ya pamoja katika kusukuma maendeleo ya Ukanda wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake