Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maebdeleo Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika katika kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga.
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, amewahamasisha wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika Kata ya Masekelo, Manispaa ya Shinyanga, Novemba 20,2024 Ntobi amesisitiza kwamba CHADEMA ni chama kilicho na dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Ntobi amesema ni muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi waadilifu watakaosimamia maslahi yao na maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
"CHADEMA tumesimama imara kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake. Tunasimamia sera ambazo zitahakikisha huduma bora kwa wananchi wetu, bila kubagua mtu yeyote. Tutahakikisha miundombinu ya afya, barabara, elimu na huduma za jamii zinaboreshwa",ameeleza Ntobi.
Ameeleza kuwa uchaguzi huu ni fursa muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi watakaosimamia maslahi yao kwa ufanisi, na kwamba CHADEMA ni chama pekee kinachoweza kuleta mabadiliko ya kweli.
"Tunaomba wananchi wachague viongozi wa CHADEMA, viongozi wa haki, viongozi watakaowatumikia kwa dhati," amesema Ntobi.
Aidha, Ntobi amekosoa viongozi wa CCM kwa kushindwa kutimiza ahadi zao na kuwataka wananchi kuwa makini katika uchaguzi huu.
"Tumechoshwa na CCM. Hatuwezi kuwa na viongozi wanajali maslahi yao binafsi. Tujitokeze kwa wingi na kuchagua mabadiliko ya kweli," amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Ntobi amewakumbusha wananchi kuhusu jukumu lao la kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa haki na amani.
"Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unakuwa wa haki na amani. Hatutakubali kuona udanganyifu wala uingiliaji wa uchaguzi",amesema
Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, na CHADEMA inahamasisha wananchi wote wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa ufanisi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake