Friday, November 22, 2024

MAELEKEZO YA RAIS SAMIA YAANZA KUTEKELEZWA KATAVI


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa vijiji vya ntilili na igalukiro baada ya kuwakabidhi hati miliki za kimila 691 tukio lililofanyika tarehe 21 Novemba 2024 katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Kasansa iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Mizengo Pinda akizungumza na wananchi wa vijiji vya ntilili na igalukiro katika tukio la kuwakabidhi hati miliki za kimila 691 lililofanyika tarehe 21 Novemba 2024 katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Kasansa iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Baadhi ya wananchi wa vijiji vya ntilili na igalukiro wakishangilia taarifa ya kukabidhiwa hati miliki za kimila 691 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Mizengo Pinda katiks tukio lililofanyika tarehe 21 Novemba 2024 katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Kasansa iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amekabidhi jumla ya Hati za Hakimiliki za kimila 691 kwa wanachi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika leo tarehe 21 Novemba 2024 katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kasansa na kuhudhuriwa na wataalam wa Ardhi kutoka ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Katavi.

Naibu Waziri Pinda amesema kuwa hatua ya kukabidhi hati hizo ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupima ardhi ya nchi nzima.

"Hizi zote ni juhudi za Mama Samia Suluhu Hassan, anataka nchi nzima hii ipimwe, watu wake wawe na hivi vibali vya ardhi yao" amesema Naibu Waziri Pinda.

Mhe. Pinda amesema kuwa vijiji vya Ntilili na Igalukiro vimenufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia ufadhili wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira umezesha uandaaji wa hati za kimila 691.

"Kupita mradi huu, Ofisi ya Makamu wa Rais imetufadhili tupime vijiji vinavoambatana na Mradi wake hapa juu (Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Uhifadhi wa Banowai) kwa hiyo wanufaika ni Ntilili na Igalukiro ambapo tumayarisha hati 691 zote zipo hapa" ameongeza Mhe Pinda.

Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Katavi ndg Chediel Mrutu amewaasa wanakijiji hao kuhifadhi hati hizo sehemu salama kwani zikiharibika si Rahisi kupata nakala Mbadala.

"Hizi hati ukiweka kwenye eneo ambalo linavuja itaharibika na ikiharibika siyo rahisi kupata nakala yake"

"Zamani watu walikuwa wanafanya lamination, hii hairuhusiwi, tafuta kibegi cha zuri na salama iweke na itunze" amesema Kamishina Mrutu.

Naye Afisa Mipangomiji Flavian wakati akisoma taarifa ya mpango wa matumizi bora ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe amesema mpango huo umewezesha kutoa elimu ya ardhi na kutenga maeneo muhimu kwa ajili ya matumizi ya bora ya ardhi pamoja na kuandaa hati za ardhi.

"Vijiji vimewezeshwa kutenga maeneo ya matumizi mbalimbali ya kilimo, makazi vyanzo vya maji hifadhi za misitu maeneo ya malisho pamoja na kutunga sheria ndogondogo za kusimamia maeneo yaliyopangwa"

Kwa upande wao wanakijiji Joyce Mataluma na Robert Kasale wamefurahi kupata hati hiyo na kuahidi kuitunza vema

Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi na uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila katika halmashauri ya Mpimbwe unaowezeshwa na Tume ya Taifa ya Matumizi bora ya Ardhi kwa ufadhili wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kupitia Mradi wa urejeshwaji endelevu wa Mazingira na uhifadhi wa banowai umewezesha kuandaa jumla hati miliki za kimila 691 ambapo kijiji cha Igalukiro zimeandaliwa hati 277 na Ntilili zimeandaliwa hati 414 sambamba na kupatiwa daftari la usajili la kijiji, cheti cha ardhi cha kijiji, ripoti maalumu ya maalumu ya matumizi bora ya ardhi, ramani ya mipaka ya kila kijiji pamoja na mhuri wa moto kwa ajili ya kusaidia kijiji kutoa hati kwa watu wasio na hati.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake