Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa mfano wa hatifungani mara baada ya kuwekeza shilingi milioni 100 katika Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) mara baada ya uzinduzi uliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela. Tarehe 29 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (kulia) pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela mara baada ya kuwasili Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam katika Uzinduzi wa Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) leo tarehe 29 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau waliowekeza katika Hatifungani ya Samia ya Miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond) mara baada ya kuzinduliwa katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Benki ya CRDB kuhakikisha uzinduzi wa Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa umma kwa lugha rahisi kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji katika fursa kama hizo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya Samia ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond) iiliyobuniwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Benki ya CRDB katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Amesema uelewa wa wananchi wengi kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji bado ni mdogo ambapo Utafiti uliofanywa na FinScope mwaka 2017 na 2023, unaonesha kuwa watanzania wanaotumia akiba zao kuwekeza katika fursa mbalimbali kama hii ya hatifungani ni 18% tu hivyo ni muhimu elimu kuendelea kutolewa.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa mifuko ya hifadhi za jamii, mifuko ya bima, vyama vya kuweka na kukopa, VICOBA, Makampuni, Taasisi na mwananchi mmoja mmoja kuchangamkia fursa zinazoambatana na Hatifugani ya Samia ya Miundombinu ambayo ni fursa nzuri ya uwekezaji kwa Watanzania, ambapo moja ya faida zitokanazo na uwekezaji wake ni riba ya asilimia 12 kwa kila mwaka kwa miaka mitano.
Vilevile Makamu wa Rais amehimiza Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ambao ni wanufaika wa hatifungani hiyo, kubuni na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika ujenzi wa barabara na madaraja ili kupunguza gharama na kuongeza ubora. Aidha amesisitiza umuhimu wa TARURA kutafuta vyanzo vingine vya mapato hususan mikopo ya masharti nafuu ikiwa ni pamoja na ile inayotolewa kupitia dirisha la mabadiliko ya tabianchi na vilevile mchanganyiko wa mikopo na mitaji pamoja na kuingia ubia na sekta binafsi katika kugharamia miradi ya kuendeleza miundombinu vijijini na mijini.
Makamu wa Rais amesema Hatifungani hiyo itaiwezesha TARURA kuongeza mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika ugharamiaji wa miradi ya miundombinu, kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi na kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara zinazosimamiwa na TARURA, unafanyika kwa wakati ili barabara hizo ziweze kutumika katika kipindi chote cha mwaka. Vilevile itasaidia kukabiliana na mahitaji ya dharura ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu unaosababishwa na uharibifu wa mvua kubwa na mafuriko.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali. Amesema mtandao wa barabara za lami nchini umeongezeka kutoka kilomita 13,235.1 mwaka 2020 hadi kufikia kilomita 15,366.36 mwaka 2024. Aidha, bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuongezeka kutoka Sh. bilioni 414.5 mwaka 2019/20 hadi Sh. bilioni 841.2 mwaka 2024/25.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema lengo kuu la kuanzisha hati fungani hiyo ni kuwasaidia wakandarasi wazawa kukabiliana na changamoto za kifedha wanazokutana nazo na kuwawezesha kushiriki katika miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara. Amesema utaratibu huo wa kifedha utawasaidia wakandarasi kupata fedha za kutosha ambazo zitawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi na kulipwa kwa wakati kulingana na mikataba ya kazi wanazofanya na hivyo kuimarisha ustawi kwa njia endelevu.
Mchengerwa amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kutatua changamoto za miundombinu hasa kupitia wakandarasi wazawa na hatua ya uzinduzi wa hatifungani hiyo ni ishara ya mafanikio ya juhudi za utekelezaji wa maelekezo ya kutatua kero mbalimbali zilizowakabili wakandarasi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Benki ya CRDB imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika sekta ya fedha na katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kushiriki katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji na uwezeshaji kwa kuhakikisha kwamba miradi ya kimkakati inafanyika kwa usahihi.
Amesema Benki ya CRDB imekua ikifanya kazi karibu sana na serikali pamoja na taasisi zake hasa katika miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi, usafirishaji, miradi ya nishati, n.k.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake