Tuesday, November 26, 2024

TUZO ZA UTALII DUNIANI WTA KWA BARA LA AFRIKA KUFANYIKA TANZANIA 2025

 


Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema Tanzania inakwenda kuandaa Tuzo za Utalii duniani (World Travel Awards, WTA) kwa Bara la Afrika kwa mwaka 2025.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo Novemba 26, 2024 wakati akiongea na Vyombo vya Habari mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kutoka nchini Ureno ambapo Tanzania ilitwaa Tuzo ya Dunia ya Sehemu Maridhawa Zaidi kwa Utalii wa Safari 2024 (World’s Leading Safari Destination) usiku wa kuamkia jana.

Dkt. Abbasi amefafanua kuwa Tanzania imepata Tuzo hiyo kutokana na ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali wa Utalii nchini katika kutangaza vivutio vya utalii.

Aidha, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour na Amazing Tanzania imesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

Ameongeza kuwa Tuzo hizo ni ishara ya kwamba wageni wamekuwa na imani kubwa na vivutio vya utalii na ukarimu ambao wamekuwa wakipata wakati wanapokuja kutembelea vivutio hivyo na kuwataka kuendelea kuwa wakarimu.

Ametoa wito kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuhifadhi vivutio vya utalii na raslimali zilizopo ili viweze kuchangia kwenye uchumi wa taifa.

 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru amesisitiza kuwa kwa sasa Tanzania inakwenda kutangaza mazao mapya ya utalii ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii na hivyo kuwafanya wageni kuongeza siku za kukaa na kutumia wakifika nchini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi amesisitiza wadau wote nchini kuzingatia sera na kanuni mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili sekta ya utalii nchini iendelee kukua.



No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake