Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua nyaraka ya Tathmini ya Utekelezaji wa afya kwa Wote na Utayari wa Kukabiliana na Dharura Nchini, baada ya kuzizindua kwenye mkutano wa pamoja wa Mawaziri na Viongozi wa juu wa Shirika la Afya Duniani kuhusu hali ya Utekelezaji wa Afya kwa Wote na Utayari wa Kukabiliana na Dharura nchini, uliyofanyika katika Hotel ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Novemba 21, 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye mkutano wa pamoja wa Mawaziri na Viongozi wa juu wa Shirika la Afya Duniani kuhusu hali ya Utekelezaji wa Afya kwa Wote na Utayari wa Kukabiliana na Dharura nchini, uliyofanyika katika Hotel ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Novemba 21, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itasimamia na kutekeleza masuala yote yaliyoainishwa kwenye taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Afya kwa wote na Utayari wa Kukabiliana na Dharura.
Ameyasema hayo (Alhamisi, Novemba 21, 2024) alipofungua mkutano wa pamoja na Mawaziri na viongozi wa Juu wa Shirika la Afya Duniani kuhusu hali ya utekelezaji wa afya kwa wote na utayari wa kukabiliana na dharura nchini. Katika Mkutano huo Mheshimiwa Majaliwa alizindua taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Afya kwa wote na Utayari wa Kukabiliana na Dharura.
Pia amesema Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kushughulikia vipaumbele pendekezwa katika eneo la utawala, utendaji na rasilimali fedha. “Sina shaka kila eneo lenye changamoto litapatiwa ufumbuzi hususan kwa kuwa mkutano huu umetoa nafasi kwa waheshimiwa Mawaziri kujadili kwa kina na kwa pamoja masuala mbalimbali kuhusu afya kwa wote na kukabiliana na dharura”
Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amezitaka Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga fedha kwa ajili ya kutelekeza shughuli za vipaumbele kama zilivyoainishwa kwenye taarifa hiyo, kwa kuwa Serikali imeanza maandalizi ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025.
Pia, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Afya isimamie suala la kuhamasisha uwekezaji katika taasisi za kitafiti, maabara na mamlaka za dawa za binadamu na wanyama ili kuliwezesha Taifa kuendelea kuwa na uwezo wa kutambua uwepo wa vimelea vya magonjwa ya mlipuko kwa haraka.
Mbali na agizo hilo kwa Wizara ya Afya, pia Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za afya nchini ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na dharura.
“Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI hakikisheni huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma wakati wa dharura zinaendelea kuwa endelevu. Endeleeni kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili wananchi wapate huduma za msingi za afya.”
Waziri Mkuu Kassim amesema sambamba na uwepo wa mifumo thabiti ya menejimenti ya maafa, Watanzania wanatakiwa waelimishwe namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo milipuko ya magonjwa na majanga yanayotokana mabadiliko ya tabianchi ambayo athari zake zimeanza kuonekana.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema kuwa mkutano huo ni moja ya juhudi za kuhakikisha Serikali na jamii yote inashirikishwa ipasavyo katika utekelezaji wa afya kwa wote na utayari dhidi ya dharura.
“Hii itasaidia kujenga uelewa na ushiriki wa pamoja kwa jamii na Serikali kwa kutambua kuwa suala la mapambano dhidi ya milipuko ya magonjwa ni la sekta zote na kila mtu. Mikakati yote ya Afya iliyopo, yaani afya ya wanyama na mifugo, afya ya vyakula na afya ya mazingira yote inalenga afya ya mwanadamu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la afya Duniani Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya afya nchini ambayo imeiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi kinara katika kukabiliana na majanga na magonjwa mlipuko.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake