Friday, December 13, 2024

BENKI YA DUNIA YAIPATIA TANZANIA SHILINGI BILIONI 248 KUSAIDIA MAENDELEO YA WANAWAKE NA KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (katikati) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakisaini Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, wakishuhudiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Onesphoro Gwajima (Mb), katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakibadilishana Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.


Na Farida Ramadhani na Chedaiwe Msuya, WF - Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wamesaini mikataba miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104, sawa na takriban shilingi bilioni 248, kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia nchini Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete.

Akifafanua kuhusu mikataba hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa mkataba wa dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada na Mkataba wa dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu.

Alisema mradi wa PAMOJA uliosainiwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na Zanzibar.
‘’Hili litatimizwa kupitia uimarishaji vikundi vya wanawake kwa kuwajengea ujuzi wa biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko, kuongeza fursa za mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, kuwaongezea upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha pamoja na kuimarisha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia”, alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba,

Alisema mradi huo utawanufaisha moja kwa moja wanawake wapatao 319,850 na walengwa wengine 399,000, wakiwemo wanafamilia za wanufaika.

Alisistiza kuwa kukuza usawa wa kijinsia si suala la wanawake pekee bali ni msingi wa Taifa la kidemokrasia, lenye haki na linalostawi na kuongeza kuwa kuondoa tofauti za kijinsia kunaboresha uzalishaji na kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi.

“Mradi wa PAMOJA ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa 2021/22 - 2025/26, Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 na pia ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amelipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia”, alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Alisema utekelezaji wa mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikaliya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (hususan Lengo la 5) na kuonesha nia thabiti ya kufanikisha ukuaji wa uchumi unaowajumuisha wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete, alisema kuwa mradi huo utatatua changamoto za kijinsia za kijamii na kiuchumi kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kubainisha mila potofu ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Aliiomba Serikali kuzikutanisha pamoja Wizara zote za kisekta zinazohusika katika utekelezaji wa mradi huo kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na Watoto.
Alisema wanatarajia mradi huo utaanza kutekelezwa mapema na kuona matokeo ya utekelezaji pamoja na faida watakazo zipata walengwa wa mradi huo.

Kwa upande wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), alimpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazofanya kuwainua wanawake kiuchumi ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi wa PAMOJA.

Alisema katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo, Wizara yake imeshazindua Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake pamoja na Mkakati wake ambao uwezeshaji wanawake kiuchumi ni miongoni mwa malengo yake.

Alisema mradi huo umekusudia kujenga nyumba salama 10 kwa ajili ya kuwahifadhi Watoto wanaokumbana na ukatili wa kijinsia pamoja na kujenga vituo 200 vya malezi salama na makuzi ambapo vituo 184 vitakuwa Tanzania Bara na 16 vitajengwa Zanziber.

“Afisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wamekuwa wakihangaika kupata ofisi za kufanyiakazi na kutoa huduma pamoja na vifaa kazi ikiwemo usafiri, sasa kwa kutumia fedha hizi watapata Ofisi 40 za maafisa Maendeleo ya Jamii na Ofisi 40 za Maafisa Ustawi wa Jamii”, alifafanua Mhe. Dkt. Ngwajima.

Alisema fedha hizo zitasaidia kuwachangamsha wanawake kiuchumi, kupata elimu ya kibiashara, mitaji pamoja na kufanya biashara wakiwa na uelewa mpana kwa sababu wataalam wamewezeshwa kuwafikia popote walipo.

Aliahidi kuhakikisha fedha hizo zitatumika kikamilifu kwenye mradi iliyokusudiwa na kuleta matokeo Chanya.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake